Salamu za Jumapili: SHANGWE MFANYIE BWANA

NA LWAGA MWAMBANDE

REJEA katika Bibilia Takatifu kitabu cha Zaburi 100:1-2..."Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote; Mtumikieni Bwana kwa furaha; Njoni mbele zake kwa kuimba."

Mbali na hayo, neno la Mungu linafundisha kwamba watu wote wameumbwa kwa mfano wa sura ya Mungu, licha ya sisi binadamu kukabiliana na vikwazo zikiwemo changamoto mbalimbali, bado Mungu anakusudia mambo mema kwenye maisha yetu.

Ndiyo maana mimi na wewe ni tunu ya Mungu na tumejaliwa na Mungu kufanya kazi ambayo Mungu ametuandalia. Moja ya mambo bora tunayotakiwa kufanya maishani ni kutambua kazi gani nzuri tuliyoandaliwa na Mungu kwenda kuifanya.

Licha ya majukumu tunayoyatekeleza kila wakati maishani, mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anaendelea kusisitiza kuwa, Mungu ndiye katuumba, na sisi tu watu wake, hivyo tuendelee kumrudishia sifa na utukufu. Endelea;


1.Shangwe mfanyie Bwana, enyi wa dunia yote,
Mtumikieni Bwana, onyesha furaha yote,
Imba mbele zake Bwana, sifa azipate zote,
Mungu ndiye katuumba, na sisi tu watu wake.

2.Vipi wamfanyia shangwe, ulipo pale popote?
Au ni hadi upangwe, kwa utumishi wowote?
Kuimba unayo ngwe, kwa kusanyiko lolote?
Mungu ndiye katuumba, na sisi ni watu wake.

3.Shangwe haumfanyii, unaona si chochote,
Wala hauangalii, wafanyao wakuvute,
Waambiwa husikii, unaziacha zipite,
Mungu ndiye katuumba, na sisi tu watu wake.

4.Kutumika husikii, hunayo kazi yoyote,
Kwako hakuna utii, Neno la Mungu lolote,
Lazidi halitulii, neema isikupite,
Mungu ndiye katuumba, na sisi tu watu wake.

5.Na hata kuimbaimba, sifa za Mungu zozote,
Kusimama ukatamba, tuone vipawa vyote,
Nako unayumbayumba, sawasawa na matete,
Mungu ndiye katuumba, na sisi tu watu wake.

6.Andiko lote la Mungu, usikize lisipite,
Ni mafundisho ya Mungu, yatufae sisi sote,
Wala kusiwe kiwingu, kwamba hayo yatupite,
Mungu ndiye katuumba, na sisi tu watu wake.

7.Neno la Mungu laonya, laja kwako likusute,
Lengo hasa kukuponya, baraka kwake uchote,
Fanya maamuzi chanya, chagua kazi yoyote,
Mungu ndiye katuumba, na sisi tu watu wake.

8.Neno ndilo laongoza, tufanyapo mambo yote,
Ndio linatueleza, sisi duniani kote,
Shangwe apate Muweza, na yetu furaha yote,
Mungu ndiye katuumba, na sisi tu watu wake.

9.Ndugu uwe na adabu, Neno hili lisipite,
Shangwe furaha wajibu, utumishi ukupate,
Anzaanza taratibu, hadi moto uupate,
Mungu ndiye katuumba, na sisi tu watu wake.
(Zaburi 100:1-2, 2 Timotheo 3:16-17)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news