Same waanza kujihami na El-nino, waomba msaada kwa wadau

KILIMANJARO-Wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikitangaza ongezeko la mvua za vuli kuzidi kiwango ikiambata na upepo mkali 'El-nino', Serikali wilayani Same mkoani Kilimanjaro imeanza kuchukua tahadhari juu ya madhara yake.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Same, Yusto Mapande akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi wenye mahitaji maalumu Same, Niwaeli Uwajia (kulia) sehemu ya vitanda 80 vilivyotolewa na Benki ya NMB vyenye thamani ya shilingi milioni 25.6, wengine kulia ni Katibu Tawala Wilaya ya Same, Upendo Whela akifuatiwa na Meneja wa Kanda ya Kaskazini NMB, Baraka Ladislaus,Meneja tawi la Same, Emily Mkenda na meneja mahusiano Kanda ya kaskazini, Christabel Hizza.

Tahadhari ya mvua hizo zilizotolewa na TMA, zinaonyesha kuwa mvua hizi zitakazoanza mwezi Oktoba hadi Desemba,mwaka huu zitakuwa za juu ya wastani na zitaambatana na upepo mkali na magonjwa ya mlipuko.

"Mvua hizi kawaida mbali na magonjwa, lakini pia yataleta mafuriko hivyo sisi kama Wilaya ya Same tumeanza kujiandaa na madhara yatakayoweza kujitokeza ikiwemo kusaka vifaa vya uokozi na uokoaji," amesema Katibu Tawala Wilaya ya Same, Upendo Whela.

Whela aliyasema hayo Oktoba 4, 2023 wakati akipokea vitanda 80 vya Shule ya Msingi Same (40) na Kimara Sekondari (40) vilivyotolewa na wadau wa maendeleo kutoka Benki ya NMB.

"Tunashukuru sana kwa msaada huu, lakini kwa sababu kitengo cha majanga pia mnasaidia tutaleta andiko rasmi kuomba vifaa vya kutoa huduma kwa ajili ya tahadhari za mvua hizi kubwa zilizotabiriwa hivyo msituchoke,"amesema.

Akikabidhi vitanda hivyo, Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus alisema kuwa, vitanda hivyo vya juu na chini (double decker) ni majibu ya maombi waliyoletewa na shule ya msingi Same inayolea watoto wenye mahitaji maalumu lakini pia Shule ya Sekondari Kimara.

"Kutokana na elimu ni moja ya kipaumbele cha Benki yetu ya NMB, ndio maana tumejibu haraka maombi yenu ya vitanda na leo tumeleta 80 vya kusaidia wanafunzi 160 kulala vyenye thamani shilingi milioni 25.6 ikiwa ni muendelezo wa kurudisha faida yetu katika kuhudumia jamii."

Alisema kuwa, Benki ya NMB mwaka huu wametenga kiasi cha shilingi bilioni 6.2 kwa ajili ya kuhudumia jamii katika sekta ya mazingira, Afya, Elimu na Majanga mbalimbali hivyo kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuisaidia serikali kutatua changamoto mbali mbali.

"Tunatambua juhudi kubwa za serikali chini ya Rais wetu Samia Suluhu za kusimamia upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi, na sisi kama wadau tunao wajibu wa kuunga mkono, kusaidia na kuwa mstari wa mbele katika kuchagia utatuzi wa changamoto zinazojitokeza katika jamii hivyo hatutachoka kuendelea kutoa misaada hii mara kwa mara itakapohitajikai,"alisema Baraka.

Wakipokea msaada huo, Mkuu wa Shule ya Msingi Same, Niwaeli Uajia alisema kuwa, vitanda hivyo vitatumika na wanafunzi wenye mahitaji maalum katika bweni walilojengewa na serikali hivi karibuni kwa fedha za Uviko-19.

"Tulijengewa bweni hili kutokana na mahitaji makubwa yaliyoonekana ya wanafunzi hawa lakini hakukuwa na vitanda hali iliyoshindikana kupatumia, hivyo tunaishukuru Benki ya NMB kwa msaada huu ambao utaongeza tija kubwa ya masomo shuleni kwetu hasa uwezo wa kuwalaza wanafunzi wanaotoka mbali."

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Same, Yusto Mapande alitumia nafasi kutoa shukrani kwa uongozi wa NMB kwa msaada huo akidai utaongeza jitihada za elimu katika kata zote zinazotegemea shule hiyo.

"Asanteni sana NMB kwani mliona haifai kuishia kufanya biashara pekee bali kurudisha kwa jamii kile kinachopatikana,..hakika ni upendo mkubwa,"alisema na kuongeza.

"Suala hili lilikuwa jukumu la Serikali na wananchi wake, lakini hawakutimiza kutokana na uwezo mdogo wa kufanya kila kitu hususani mambo yaliyoko kwenye mahitaji, ndio mkaja nyie hakika mmetupiga teke zuri na kutuvusha hiki kigingi na Mungu awabariki."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news