Serikali kuendelea kutenga miradi ya ujenzi kwa wakandarasi wanawake

DAR ES SALAAM-Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, amesema Serikali itaendelea kutenga miradi ya ujenzi kwa ajili ya wakandarasi wanawake ili kuwawezesha wakandarasi hao kupata uzoefu, kukuza mitaji na kutoa fursa kwa Watanzania.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya akikabidhi tuzo kwa baadhi ya wadau waliowezesha kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Wakandarasi wanawake uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Oktoba 12, 2023.

Akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wakandarasi Wanawake jijini Dar es Salaam, Eng. Kasekenya amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wakandarasi wanawake wanaimarika na kutekeleza miradi mingi ya Serikali ambayo inatekelezwa nchini.

“Chapeni kazi, pia kamilisheni miradi kwa wakati ili Serikali iwaamini na kuwatengenezea mazingira mazuri ya kupata kazi nyingi zitakazowainua kiuchumi kama walivyo makandarasi wengine,”amesema Eng. Kasekenya.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Wakandarasi wanawake uliofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam leo Oktoba 12, 2023.

Aidha, amewataka wakandarasi wanawake kuwa waaminifu na waadilifu ili kuaminiwa na taasisi mbalimbali ikiwemo taasisi za kifedha na kuweza kupata mikopo kwa urahisi hatimaye kukuza mitaji yao.

Amezungumzia umuhimu wa Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali kuwajengea uwezo wakandarasi wanawake ili wamudu kutekeleza miradi mbalimbali nchini ikiwemo miradi midogo na mikubwa.
Baadhi ya wakandarasi wanawake wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya (hayupo pichani) kwenye Mkutano Mkuu wa Wakandarasi hao uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Oktoba 12, 2023.

“Awamu ya Sita imejipanga kutekeleza miradi mingi ya miundombinu hivyo unganeni jengeni uhusiano mzuri na taasisi mbalimbali ili mpate kazi,” amesema Kasekenya.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wakandarasi Wanawake, Eng, Judith Odunga, ameishukuru Serikali kwa namna inavyotoa vipaumbele vingi kwa wakandarasi wanawake na kusisitiza utaratibu huo ukiendelea uchumi kwa wakandarasi wanawake utakuwa na kuchochea maendeleo ya nchi.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya akikabidhi tuzo kwa baadhi ya wadau waliowezesha kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Wakandarasi wanawake uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Oktoba 12, 2023.

Huu ni mkutano Mkuu wa Tatu kufanyika kwa wakandarasi wanawake, ambapo mkutano huu hufanyika mara moja kwa mwaka lengo likiwa ni kuwakutanisha pamoja, kujadili changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news