RUVUMA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Petamiho amesema, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma imedhamiria kufungua shamba kubwa la miwa na kiwanda cha kuzalisha sukari katika Kijiji cha Muhukuru.
Hayo ameyabainisha Septemba 30,2023 katika Kijiji cha Lupokea mkoani Ruvuma katika Maadhimisho ya Siku ya Kahawa yaliyoandaliwa na Kampuni ya Aviv, wawekezaji wa mashamba ya kahawa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
“Tunaamini tukifungua shamba jingine Muhukuru tunaweza kuzalisha ajira nyingine nyingi na kuongeza mapato ya halmashauri na pato kwa wananchi,”alisisitiza.
Wawekezaji wa Kampuni ya Aviv wanazalisha asilimia 4.5 ya kahawa yote inayozalishwa nchini ambayo inauzwa nje ya nchini, na wanasaidia nchi kupata fedha za kigeni, ambazo zinawezesha serikali kujenga miradi ya maendeleo kwa wananchi.

Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mkazo katika kufungua kilimo ili kusaidia kuchochea uchumi na kutoa ajira ili kuhakikisha kilimo kinakuwa na faida katika kufungua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
“Wananchi ni mashuhuda wa uwekezaji uliofanywa na Kampuni ya Aviv katika kilimo cha kahawa; ulivyowezesha kufanya mabadiliko ya kijamii, uchumi na mabadiliko ya mwenendo wa maisha ya wananchi katika vijiji vinavyozunguka mradi,” alifafanua.
Ameongeza kuwa, mwekezaji wa Kampuni ya Aviv anashiriki katika ujenzi wa miradi mingi katika vijiji vinavyozunguka mradi kama utaratibu wa serikali unavyoelekeza kwa Wawekezaji, kwamba washirikiane na wananchi katika kurudisha mchango wa kile walichokivuna kama faida. Amewaomba wananchi kutobweteka na badala yake kuendelea kujitoa katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Meneja wa Shamba la Kampuni ya Aviv Tanzania, Bw. Hamza Kassim amesema siku ya leo tunadhimisha siku ya kahawa duniani, maadhimisho ambayo yanayofanyika kila tarehe 01 ya mwezi wa 10, kila mwaka.
Ameongeza kuwa,Kampuni ya Aviv wamefanikiwa kuwa na uzalishaji endelevu kwa sababu ya kujenga miundo mbinu ya umwagiliaji ambayo imeleta tija katika kuchangia miradi mabalimbali ya maendeleo kwa jamii.
“Kampuni ya Aviv inaendelea kujenga uwezo kwa wananchi ili waweze kuwa wakukulima wa kilimo cha kahawa chenye tija zaidi,”alifafanua.
Awali, Bi.Rose Choma Mkulima amesema Mradi wa kampuni ya Aviv wamesaidia wakulima katika kuwapa wananchi mbegu zenye ubora na kutoa ajira kwa wazawa ambazo zimesaidia kuinua pato kwa wananchi.