TANAPA yatakiwa kutumia teknolojia ya kisasa katika ulinzi wa maeneo ya hifadhi

NA HAPPINESS SHAYO

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limetakiwa kutumia teknolojia ya kisasa kulinda na kuhifadhi maeneo yake kwa lengo la kuzuia ujangili na uvamizi wa maeneo hayo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ameyasema hayo Oktoba 28,2023 alipokuwa akizungumza na menejimenti ya TANAPA katika Ofisi za Makao Makuu ya TANAPA jijini Arusha.

"Kuhusu kukabiliana na ujangili pamoja na kufanya doria hifadhini tuendelee kuwa na matumizi ya vifaa vya teknolojia ya kisasa kuhakikisha doria na ulinzi wa maeneo yetu unafanikiwa kwa asilimia mia,"amesema Mhe. Kairuki.

Amesema kwa kufanya hivyo, itawarahisishia utendaji kazi na kuwezesha ulinzi wa maeneo ya hifadhi kwa njia ya kisasa zaidi.

Aidha, ameitaka TANAPA kuendelea kutangaza vivutio vya utalii kidijitali ili kufikia idadi ya watalii milioni tano kama ilivyokusudiwa.

"Muendelee kujiimarisha katika matumizi bora na sahihi ya kidijitali na pia mjikite katika kupata mrejesho wa huduma zinazotolewa kwa watalii ili tuweze kuboresha huduma hizo,"Mhe. Kairuki amesema.

Aidha, amewataka watumishi wa TANAPA kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo na kwa kutumia busara ili kulifanya shirika hilo lisonge mbele.

Amefafanua kuwa ni vyema watumishi hao kutoa huduma bora za haraka, zenye ufanisi na zenye matokeo makubwa ya kuvutia watalii.

Mhe. Kairuki pia ameitaka menejimenti ya shirika hilo kushughulikia migogoro kati ya hifadhi na wananchi kwa kuhakikisha inapatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo na kuendelea kuwa na mahusiano mazuri na wananchi kwa kuboresha ujirani mwema.

Naye, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Mussa Juma amesema atahakikisha anafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na kuwa wabunifu kuhakikisha shirika hilo linasonga mbele

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news