Tanzania inatekeleza kwa vitendo Tamko la Dar es Salaam-Rais Dkt.Mwinyi

NA BEATRICE LYIMO
MAELEZO

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kuchukua hatua katika kutatua migogoro mbalimbali na kutekeleza kwa vitendo Tamko la Dar es Salaam kuhusu Amani, Usalama, Demokrasia na Maendeleo katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
Hayo yamebainishwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Kawaida cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, leo Oktoba 20,2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.

“Kwa mfano, hivi sasa Tanzania inashiriki katika Jeshi la Umoja wa Mataifa, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (Stabilization Mission) na Jeshi la Kulinda Amani (MONUSCO),” ameomgeza Dkt. Mwinyi.
Aidha, Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa, katika kuepusha uvunjifu wa haki za binadamu unaotokana na vita, kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania inashiriki katika Jeshi la pamoja la kulinda amani madhariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na pia imeshiriki katika ulinzi wa amani katika nchi mbali mbali ikiwemo huko Darfur Sudan na Visiwa vya Comoro.

“Naona fahari kwa Majeshi yetu kwa kazi yao nzuri wanayoifanya; nitoe wito kwa nchi zetu za Afrika kuendelea kushirikiana katika kuyakabili matukio mbalimbali yanayohitaji msaada wa kibinadamu katika Bara letu,” ameongeza Dkt. Mwinyi.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana, amebainisha kuwa, Kikao hicho cha 77 cha Kamisheni za Haki za Binadamu na Watu kimelenga kujadili na kubadilishana uzoefu katika kusimamia masuala ya haki za binadamu na watu.

Aidha, ameongeza kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Afrika nzima kama jinsi ambavyo imekuwa ikishirikiana nao tangu enzi za uongozi wa Awamu ya Kwanza chini ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“Utaratibu wa kutambua haki za binadamu nchini Tanzania umekuwa ni utamaduni tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere wakati nchi inapata uhuru. Tutakuwa na wajibu wa kuhakikisha ndugu na majirani zetu ndani ya Afrika wanapata uhuru,” amebainisha Balozi Dkt. Chana.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman ameeleza kuwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, anatekeleza kwa vitendo masuala ya Sheria, Utawala Bora na Haki za Binadamu na pia ameendeleza huduma mbalimbali za elimu, afya, maji na miundombinu kwa ajili ya wananchi.
Takribani wadau 1000 wa masuala ya haki za binadamu wanashiriki Kikao cha Kawaida cha 77 cha Kamisheni ya Haki za Binadamu na Watu kutoka Serikali za Afrika, Wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa, Wawakilishi kutoka Umoja wa Afrika, Taasisi za Kitaifa za Haki za Binadamu, Mabalozi kutoka nchi mbalimbali, Asasi za Kiraia, Viongozi wa Kidini na kimila na watu wengine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news