ARUSHA-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kukuza na kulinda haki za wanawake na kuhakikisha wananufaika na haki za binadamu na watu kwa kuzingatia matakwa ya Itifaki ya Maputo ya mwaka 2003.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Richard Kilanga kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu wa Wizara hiyo, Bi. Nkasori Sarakikya akitoa maelezo ya nchi kuhusu hali ya haki za wanawake wakati wa vikao vya Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu vinavyofanyika jijini Arusha. Kikao hicho kilichofanyika tarehe 22 Oktoba 2023 pamoja na mambo mengine kilipokea Taarifa ya Hali ya Haki za Wanawake barani Afrika iliyowasilishwa na Mtaalam kutoka Tume hiyo Mhe. Mhe. Janet Ratatouille Sallah-Nji.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 22 Oktoba 2023 na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Richard Kilanga wakati akitoa maelezo ya nchi kuhusu hali ya haki za wanawake nchini ikiwa ni mwendelezo wa vikao vya Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu vinavyofanyika jijini Arusha.
Bw. Kilanga ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Biandamu katika Wizara hiyo, Bi. Nkasori Sarakikya amesema Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria mbalimbali zinazopinga unyanyasaji dhidi ya wanawake ikiwemo sheria ya kupinga mila potofu ya ukeketaji wanawake
Amesema katika kukabiloana na vitendo vya ukeketaji, Serikali imeandaa na inatekeleza Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji wa mwaka 2020/21-2024/2025 na Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ambayo imetaja ukeketaji kama kosa la jinai.
“Tunapongeza taarifa ya Mtaalam wa Haki za Wanawake kutoka Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na tunaunga mkono maoni na ushauri wake kwamba ukeketaji ni kati ya mila ambazo zinamnyima mwanamke haki zake. Katika hili, Tanzania imechukua hatua mbalimbali za maksudi ili kutokomeza kabisa vitendo vya ukeketaji ikiwemo kutekeleza mpango wa taifa wa kutokomeza ukeketaji,” amesema Bw. Kilanga.
Pia ameongeza kusema kuwa, katika kulinda na kutetea haki za wanawake hapa nchini, Jukwaa la Kitaifa la Haki za Mwanamke lilizinduliwa tarehe 06 Juni 2023 likiwa na lengo la kurahisisha upatikanaji wa haki za mwanamke kwa wakati kwa wanawake wa mijini na vijijini.
Pia amesema katika kukabiliana na na ukatili kwa wanawake na watoto Serikali imekuwa ikitekeleza Mpango kazi wa Kitaifa wa Kuzuia Ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017/18-2021/2022. Amesema katika utekeelzaji wa mpango huu sheria mbalimbali zimetungwa ikiwemo Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21 ambapo suala hili limepata sura ya kitaifa na linatekelezwa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia.
Kwa upande wa Zanzibar, Serikali inatekeleza Mpango Mkakati wa Kupinga ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kwa kuanzisha Mahakama Maalum zinazoshughulikia masuala ya udhalilishaji.
Awali akiwasilisha Ripoti Maalum ya Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kuhusu Haki za Wanawake, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo ambaye pia ni Mtaalam wa Haki za Wanawake, Mhe. Janet Ratatouille Sallah-Njie ameipongeza Tanzania kwa jitihada mbalimbali inazochukua katika kusimamia haki za wanawake na watoto na kuitaja kuwa miongoni mwa nchi chache za Afrika zilizofanikiwa na za mfano wa kuigwa.