
Katika mijadala iliyowasilishwa, nchi wanachama zimesisitizwa kuzingatia uwekezaji endelevu unaozingatia utunzaji wa mazingira, kuimarisha uwekezaji katika eneo la mafunzo na matumizi ya teknolojia ili kuendelea kuboresha sekta ya utalii na ukarimu
Aidha, nchi wanachama zimesisitizwa kuendelea kuboresha miundombinu ili kuvutia watalii wengi zaidi.
Waziri Kairuki pia alitembelea maonesho ya utalii yaliyokuwa yakifanyika sambamba na Jukwaa la Uwekezaji na kujionea vivutio na maendeleo ya utalii nchini Uzbekistan na kushauri wadau wa utalii nchini Uzbekistan kutangaza utalii na bidhaa zao nchini Tanzania ikiwemo kuchangamkia fursa ya maonesho ya kimataifa yanayofanyika nchini Tanzania.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri alikutana na kufanya mazungumzo na Bw. Raximov Jurabek Raximovich, Gavana wa Jimbo la Khorezm, ambalo limepiga hatua kubwa katika utalii wa utamaduni na ubunifu katika kazi za sanaa za mikono (handcrafts).
Kupitia mazungumzo hayo, Mhe. Kairuki alitoa pendekezo kwa nchi mbili kushirikiana katika kukuza utalii ikiwemo kubadilishana uzoefu katika kukuza utalii wa utamaduni, kuimarisha usafiri wa anga kati ya nchi mbili ili kurahisisha watalii kutembelea nchi zote mbili pamoja na kuimarisha ushirikiano wa wadau wa utalii kutoka sekta binafsi kwa lengo la kukuza utalii katika nchi zote mbili.