TARURA yafungua barabara 10 zenye urefu wa kilomita 34.6 Mafia

PWANI-Wakala ya Barabara za Vijijiji na Mijini (TARURA) Wilaya ya Mafia mkoani Pwani kwa mwaka wa fedha 2023/24 imefungua jumla ya barabara mpya 10 zenye urefu wa kilomita 34.6 ili kuwezesha wananchi kuyafikia maeneo yaliyokuwa hayafikiki.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Mafia, Mhandisi Maneno Makorongo wakati wa ukaguzi wa miradi inayotekelezwa wilayani humo.

"TARURA Wilaya ya Mafia hadi sasa tumefungua barabara mpya 10 kwa mwaka huu wa fedha na hii ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wetu wa kuhakikisha tunafungua barabara kufika kusikofikika,"amesema Mhandisi Maneno.
Naye Diwani wa Kata ya Baleni, Mhe. Darweshi Abedi amesema kuwa, barabara hiyo ina mchango mkubwa kwa wananchi kwani itasaidia katika shughuli za kijamii na kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuwezesha wananchi kusafirisha mazao kwa urahisi kuelekea sokoni.

"Barabara hii ya Zawiani-Mlola ni muhimu kwa uchumi wetu maana ukiacha kusafirisha mazao bado kuna shughuli za kijamii zinazotegemea uwepo wa usafiri wa uhakika kwa kipindi chote cha mwaka," amesema Mhe. Darweshi.
Kwa upande wake Bi. Mwanaisha Omary ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kungwi ameeleza kuwa suala la kuifungua barabara ya Zawiani-Mlola yenye urefu wa kilomita 2.6 imeleta fursa kwa wananchi kijamii na kiuchumi na kwamba eneo hilo halikuwahi kuwa na barabara.

"Mwanzoni hatukuamini juu ya ufunguzi wa barabara hii lakini sasa shughuli za kiuchumi zinaendelea vizuri na hata zile za kijamii kwani ni rahisi kuzifikia huduma za afya na elimu tofauti na awali, tunaipongeza serikali kwa kuuona umuhimu wa barabara hii,"amesema Bi.Mwanaisha.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA ) katika Wilaya ya Mafia mkoani Pwani hadi sasa inasimamia mtandao wa Barabara zenye urefu wa kilomita 208 lengo likiwa ni kuendelea na ujenzi na matengenezo ya barabara hizo ili kuwezesha wananchi kufika kusiko fikika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news