NA GODFREY NNKO
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (Tanzania Shipping Agencies Corporation-TASAC) limewashauri Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara na usafirishaji majini hapa nchini.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Nelson Mlali amesema, kupitia sekta hiyo kuna fursa nyingi ambazo Watanzania wakiweza kuzitumia kikamilifu zitawanufaisha wao na Taifa kwa ujumla.
Ameyabainisha hayo leo Oktoba 5, 2023 katika kikao kazi kati ya wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Leo katika kikao hiki TASAC ni taasisi ya 19 kati ya mashirika na taasisi ambazo zipo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ambazo tayari zimekutana na wahariri kuelezea zilipotoka, zilipo, zinapoelekea na mafanikio yake.
“Zipo fursa nyingi katika sekta ya usafirishaji wa majini.Ipo fursa ya kusajili meli kwa njia rafiki na fursa ya kuwekeza katika vituo vya kufanya matengenezo ya vyombo vya majini.”
Mlali amesema,miongoni mwa sababu zinazowafanya kuzidi kuwa kinara katika sekta ya usafiri majini ni kutokana na ushirikiano mkubwa walio nao na wadau.
“Pia tunawakaribisha katika kuanzisha maegesho kwa ajili ya vyombo vya majini hususani boti, uanzishaji wa viwanda vya malighafi za utengenezaji wa boti za plastiki, fursa za uanzishwaji wa bandari za uvuvi, fursa ya kukidhi mahitaji ya visiwa vya Comoro.
“Kumekuwa na changamoto kadhaa wakati mwingine wa kushindwa kukidhi mahitaji ya watu wa Comoro, hivyo kuna fursa katika eneo hili.”
Amesema, Comoro wanategemea huduma nyingi kutoka nje ya nchi ambapo Tanzania ina bahati kubwa ya kuwa karibu na visiwa hivyo hususani kupitia Bandari ya Mtwara.
Mlali amesema, mahitaji kama mifugo hususani mbuzi, ng’ombe na samani mbalimbali kutoka nchini zina mahitaji makubwa nchini Comoro.
“Hivyo, kuna umuhimu wa kuwekeza katika eneo hili na hata umiliki wa vyombo vya usafirishaji majini, kwani tukiwa tayari kuwekeza kuhudumia watu wa Comoro ninadhani na hata wao watafarijika kuliko kuendelea kuagiza bidhaa kutoka mbali huko.”
Pia, amesema wamedhamiria kuweka msukumo wa kuhamasisha vijana wa Kitanzania ambao watasomea fani mbalimbali zinazohusiana na sekta ya biashara na usafirishaji majini.
“Na moja wapo ya jitihada ambayo tunafanya ni kukamilisha mifumo ya TEHAMA katika kuwezesha uhudumiaji wa meli, na kuendelea kutoa elimu kwa umma ili waweze kuifahamu kwa kina sekta ya usafiri majini.”
Pia, amesema shirika linashiriki kikamilifu katika kufanikisha fursa za kukuza uchumi nchini.Katika hatua nyingine, Malali amesema, wamefanikiwa kuongeza idadi ya kaguzi ya meli za kigeni.
“Kaguzi hizi zina faida nyingi, lakini kubwa zaidi ni kuhakikisha usalama, kwa hiyo tunakagua na tunatoa taarifa ambazo zinaheshimiwa hata katika bandari ambazo meli hizo zinakwenda.”
Amesema,licha ya TASAC kuwa ni taasisi changa imekuwa na mchango mkubwa katika uchangiaji wa mfuko mkuu wa Serikali kutoka shilingi bilioni 9 hadi zaidi ya shilingi bilioni 40.
Pia,wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kudhibiti bandari bubu ambazo ni hatari kwa usalama wa Taifa na wananchi.
“Huku tusipokuwa makini, inaweza kusababisha kuingiza wahamiaji haramu, lakini pia kuingiza bidhaa ambazo zipo chini ya viwango, hivyo sisi kama vinara wa usafiri wa majini tumekuwa tukishirikiana na wadau wengine kudhibiti hilo na zile ambazo zinakidhi vigezo zinapewa vibali.”
Vile vile, amesema kupitia kanuni na ufuatiliaji mzuri wamefanikiwa kudhibiti umwagikaji wa mafuta majini jambo ambalo linaendelea kuyafanya mazingira ya majini kuwa salama.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania limeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania Sura ya 415 na kuanza kutekeleza majukumu yake rasmi kuanzia Februari 23, 2018 kufuatia Tangazo la Serikali Na. 53 la Februari 16, 2018.
“Majukumu ya shirika ni kusimamia na kudhibiti sekta ya usafiri wa majini, kuwezesha biashara ya usafirishaji majini na kufanya biashara ya uwakala wa meli.”
Amesema, misingi mikuu ya kuanzishwa kwa shirika ni kuwajibika kwa Taifa na kwa wadau katika kutekeleza mamlaka na makujumu yaliyo chini ya dhamana ya shirika.
Pia,kuwa mfano wa kuigwa katika mwenendo wa kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu kwenye shughuli zote.“TASAC inatoa huduma kwa weledi na kuhakikisha wateja wanapata huduma iliyo bora na kwa wakati.
“Huduma zinazotolewa na TASAC ni biashara ya usafirishaji,usalama wa usafiri wa majini, usajili wa vyombo vya majini na udhibiti wa uchumi.”
Aidha, amesema kazi kuu za msingi za shirika kisheria ni kuboresha huduma za usafirishaji wa majini,kuboresha usalama wa usafiri wa majini.
Vile vile kusimamia usalama na ulinzi na utunzaji wa mazingira ya bahari na maziwa pamoja na huduma za biashara za meli.
“Katika jukumu la wakala wa forodha, shirika linahakiki nyaraka za wateja na kuratibu vibali mbalimbali, kufuatilia nyaraka za kodi, kufuatilia nyaraka za usafiri na usafirishaji.
“Maeneo ya kiforodha ni mengi, kwani hata mipakani tunahusika na katika viwanja vya ndege kuna baadhi ya mizigo tunaifuatilia.”
Tags
Habari
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Ofisi ya Msajili wa Hazina
Tanzania Shipping Agencies Corporation-TASAC
TASAC Tanzania