TIB yafanikisha uwekezaji wa bilioni 988.7/- nchini

NA GODFREY NNKO

BENKI ya Maendeleo Tanzania (TIB) imesema hadi Septemba, 2023 imefanikisha uwekezaji wa shilingi bilioni 988.7 katika miradi ya Serikali na sekta binafsi ambayo ni ya muda mrefu.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 16, 2023 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Lilian Mbasse kupitia kikao kazi kati ya benki hiyo na wahariri wa vyombo vya habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema, fedha hizo zimeenda katika sekta mbalimbali ikiwemo miradi ya nishati, kilimo, madini, afya, maji na mingineyo ikizingatiwa kuwa TIB ni benki ya kisera.

Mbasse amefafanua kuwa, chini ya uwekezaji huo asilimia 93 ni katika miradi ya sekta binafsi na asilimia saba ni miradi ya sekta za umma. Vile vile,miradi ya asilimia 80 ni ya muda mrefu ambayo inadumu hadi zaidi ya miaka mitano.

Ameishukuru Ofisi ya Msajili wa Hazina, kwa kuratibu vikao kazi hivi muhimu ambavyo vinawezesha umma kupata taarifa sahihi kuhusiana na taasisi na mashirika yao hapa nchini.

Amesema, lengo la kuanzishwa kwa TIB ni kujenga Tanzania ya maendeleo ya kiuchumi. “TIB kwa mujibu wa sheria inahakikisha upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.

TIB ilianzishwa Novemba 1970 hapo awali na Sheria ya Bunge, Sheria ya Benki ya Uwekezaji ya Tanzania ya 1970 kwa kusudi kuu la kufadhili maendeleo kwa msisitizo juu ya ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Kutoa mikopo ya muda mrefu na ya kati, na tunafanya hivyo kwa mujibu wa sheria, tukiangalia zaidi katika kuchochea maendeleo, tunaangalia zaidi impact yetu katika maendeleo.”

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema, jukumu lingine ni kutoa ushauri wa kiufundi katika miradi mbalimbali.

Pia,wanawajibika kusimamia mifuko maalumu kwa niaba ya wadau wa maendeleo au Serikali.

“Tunakabidhiwa hiyo progamu au hiyo funds halafu tunasimamia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ambayo wameainisha kwa niaba ya Serikali.”

Amesema, mtaji wao wanategemea Serikali kwa kiwango kikubwa, lakini pia huwa wanakopa katika taasisi za Kimataifa ili kupata mtaji wa kujiendesha ambapo wanatarajia baadae kupunguza mzigo wa utegemezi serikalini.

Akizungumzia jukumu lingine la TIB, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema wanasimamia shughuli zozote ambazo zinaendana na maendeleo hapa nchini, kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji wa TIB.

Katika sekta ya kilimo, amesema TIB imefanya uwekezaji mkubwa. Amesema, katika hii sekta kuna uwekezaji wa aina mbili kwa maana ya fedha za TIB pekee na jambo la pili ni kupitia dirisha la kilimo.

Mbasse amesema, dirisha la kilimo wanalisimamia kwa niaba ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha ambapo riba ni asilimia tano kwa yale makampuni ambayo yanakwenda kukopa kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo.

Amesema, kupitia Sekta ya Kilimo TIB imewekeza katika miradi 253 ndani ya mikoa 23 ya Tanzania na katika wilaya 76 nchini.

Kupitia miradi inayotekelezwa ya kilimo, amesema zaidi ya ajira 10,000 zimepatikana.Mbali na hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema, TIB katika miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya maji.

Amesema, kupitia sekta hiyo wanawezesha miradi mbalimbali ya maji kupitia fedha za benki yenyewe.

Aina ya pili ya uwekezaji ni kupitia fedha za wahisani hususani Benki ya Dunia, wamekuwa wakienda kubadilisha zile pampu ambazo zinatumia dizel vijijini na kuweka umeme jua.

Zaidi ya jumuiya 60 zinanufaika na mradi huo, ambapo kupitia pre-paid wanapata fedha katika mfumo sahihi.

Uwekezaji wa tatu, wanasimamia Mfuko wa Maji wa Taifa, hivyo wana dirisha lao la mikopo ambayo wanatoa kwa mamlaka za maji ambazo zinakidhi vigezo.

“Fedha zimetengwa na Mfuko wa Maji wa Taifa, sisi tunasimamia.”Hadi kufikia Septemba, mwaka huu amesema, tayari wana mamlaka zaidi ya sita za maji ambapo zaidi ya shilingi bilioni 14 zimewekezwa.

Aidha, wananchi 750,000 wamenufaika kupitia miradi ya maji na kuwapunguzia changamoto ya kutembea umbali mrefu wa kwenda kutafuta maji.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo akizungumzia Sekta ya Nishati amesema, kuna uwekezaji wa aina mbili.

Uwekezaji huo unajumuisha fedha zao kama benki na aina ya pili ni uwekezaji kupitia fedha za Benki ya Dunia.

“Kwa fedha yetu ya TIB tumewekeza kwa taasisi kubwa kama TANESCO, shilingi bilioni 12.3 zimetolewa katika nishati. Megawati 8.84 zimezalishwa na kuingizwa katika Gridi ya Taifa.”

Mbali na sekta hizo tatu, TIB inatoa mitaji kwenye sekta zote nchini ili kuhakikisha ile miradi ambayo inatekelezwa inaleta matokeo chanya kwa ustawi bora wa jamii na uchumi wa Taifa.

Pia, amesema TIB imekuwa ikishiriki kikamilifu katika kufanikisha miradi ya kimkakati nchini.“Utalii ni miongoni mwa sekta ambazo tunazipa kipaumbele kikubwa.”

Amesema, kuna ajira zaidi ya 30,000 ambazo zinapatikana kulingana na miradi ambayo inafanikishwa na TIB.

Mbali na kutoa mitaji, TIB pia inatoa huduma ya usimamizi wa mifuko kwa niaba ya wadau wa maendeleo ikiwemo Serikali na wadau wengine.

Hadi kufikia Septemba 30,2023 wanasimamia mifuko nane. “Sisi kama benki ya kisera, tunatekeleza majukumu yetukwa kuzingatia sera za serikali.”

Akizungumzia huduma maalum za ushauri wa Kitaalamu, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema, benki yao imetoa ushauri wa kitaalamu katika miradi ya kimkakati ikiwemo ATCL na TTCL. Sambamba na utengenezaji wa mpango wa biashara wa muda wa kati.

Amesema, mradi wa TPDC ni wa utafutaji wa gesi (gas exploration), katika Bahari ya Hindi kupitia Kampuni ya M&P, ambapo waliweza kuwahudumia kupitia mpango huo, wakati kwa TANESCO ni kupitia mradi wa utanuzi wa huduma za umeme mijini.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo ameongeza kwamba, kupitia mpango wa kibiashara na fedha, walitoa ushauri wa kitaalamu wa mradi wa DART. Pia, kwa TPA waliangazia katika mpango wa kibiashara na fedha kwa ajili ya mradi wa Bandari ya Bagamoyo na ushauri wa kitaalamu katika uendeshaji miradi ya Bandari ya Bagamoyo.

Vile vile, TRL ni kupitia mpango wa kibiashara na fedha, ushauri wa kitaalamu wa mradi wa TRL, Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP)- Hoima (Uganda)-Tanga (Tanzania) na Mfuko wa Msaada wa Kiufundi, huku benki hiyo ikitenga fungu maalum kwa ajili ya kusaidia taasisi na mashirika kuandaa miradi inayokidhi vigezo vya uwekezaji na mikopo.

Miradi mingine iliyofaidika na mfuko huu ni Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha Mbezi Louis (Magufuli Bus Terminal), kupitia Jiji la Dar es Salaam (DDC), Mradi wa Soko la Kisasa la Kisutu kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, mradi wa Kiwanda cha Kuchakata zabibu kilichopo Chinangali katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Leo TIB, ni taasisi ya 19 ambayo ipo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kukutana na wahariri wa vyombo vya habari ikiwa ni kutekeleza maono ya Msajili Nehemiah Mchechu.

Mchechu anasisitiza kuwa, suala la utawala bora katika mashirika haya ni jambo muhimu na ambalo halikwepeki, kwani lazima kila aliyeaminiwa awajibike kikamilifu ili mashirika hayo yaweze kuleta matokeo chanya.

Hivyo, kupitia vikao kazi hivi wanapata nafasi ya kuelezea wanafanya mambo gani, wanaelekea wapi na yapi matarajio ya mashirika hayo.

Aidha,mikutano hii imekuwa kiunganishi muhimu kati ya wahariri ambao kupitia vyombo vyao wanaueleza umma kile ambacho taasisi au mashirika yao wanakifanya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news