DAR ES SALAAM-Klabu ya TP Mazembe kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeinyuka Esperance Sportive de Tunis ya nchini Tunisia bao 1-0 katika michuano ya African Football League.
Ushindi huo wameupata Oktoba 22, 2023 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Kupitia mchuano huo wa robo fainali, bao hilo la pekee limefungwa na foward wao,Cheick Oumar Abdallah Fofana dakika ya 11.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt.Damas Ndumbaro ni miongoni mwa viongozi walioshuhudia mchezo huo.
Wengine ni Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Hamis Mwinjuma na Katibu Mkuu Bw. Gerson Msigwa, vongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Vilabu na Mashabiki ambao wamejitikoza kwa wingi ukiwa ni mchezo wa pili wa mashindano hayo katika uwanja huo.
Mashindano hayo yalifunguliwa hapo hapo Oktoba 20, 2023 kwa mchezo kati ya Simba na Al Alhy ya nchini Misri ambao walitoka suluhu ya mabao 2-2.
Miamba hao wa Afrika ya Kati wanatarajiwa kuelekea Tunis katika kile kinachotajwa kuwa ni vita kali zaidi huko Kaskazini wakati pande hizo mbili zitakapokutana tena Jumatano ya Oktoba 25,2023.