NA GODFREY NNKO
OKTOBA 26, 2023 jijini Dar es Salaam Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imethibitisha kuwa, Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika bodi hiyo ili kuwanufaisha wanafunzi wengi zaidi nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema, katika kipindi cha miaka minne ambayo inajumuisha 2020/2021 hadi 2023/2024),Serikali imeongeza bajeti ya mikopo kwa asilimia 69 kutoka shilingi bilioni 464 hadi shilingi bilioni 786.
Badru ameyabainisha hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya HESLB katika kipindi cha miaka minne katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Hili ni ongezeko kubwa na limeongeza idadi ya wanufaika kwa mwaka kutoka 149,506 hadi 220,376 watakaonufaika mwaka huu wa masomo,”amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Amesema, kati ya fedha hizo shilingi bilioni 731 ni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu kwa ajili ya masomo ya shahada ya kwanza.
"Ni kwa ajili ya kusomesha wanafunzi 220,376 wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa kwanza 75,000 watakaojiunga na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu kwa ajili ya masomo ya shahada ya kwanza. Fedha hizo zitanufaisha wanafunzi 145,376 wanaoendelea."
Mkurugenzi Mtendaji huyo amefafanua kuwa, shilingi bilioni 6.7 ni kwa ajili ya Programu ya Samia Scholarship ambapo zinawafikia jumla ya wanufaika 1,276 wakiwemo wanafunzi 640 wapya.
Amesema,juhudi hizo zinafanyika ikiwa ni kwa kutambua umuhimu wa wataalamu wa Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba kwa maendeleo ya Taifa.
"Hivyo, Samia Scholarship imeingia katika msimu wa pili baada ya wanafunzi 636 wa fani kama hizo kunufaika mwaka jana 2022/2023."
Aidha, kati ya fedha hizo shilingi bilioni 48 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya Diploma ambapo itawafikia wanufaika 8,000 wa fani za kipaumbele.
Badru amezitaja fani hizo kuwa, ni Afya na Sayansi Shirikishi, Elimu,Usafiri na Usafirishaji, Uhandisi na Nishati,Madini na Sayansi ya Ardhi,Kilimo na Mifugo
Amefafanua kuwa, fedha zimekuwa zikitolewa kwa wakati na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ongezeko hilo na kuhakikisha zinapatikana kwa wakati hatua inayoimarisha utulivu vyuoni.
Kwa nini HESLB?
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilianzishwa mwaka 2004 kupitia Sheria ya HESLB (SURA 178) na kuanza kazi rasmi Julai, 2005.
HESLB inatekeleza majukumu makuu mawili ambayo ni upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wahitaji na kukusanya madeni kutoka kwa wanufaika ambao madeni yao yameiva.Lengo kuu ni kuwezesha uzalishaji wa nguvu kazi ili kuchochea maendeleo nchini.
Pia amesema, tangu kuanzishwa kwake ukwasi wake umefikia zaidi ya shilingi trilioni 7.2 ambazo zimekwenda kwa wanufaika 750,000 nchini.
“Kwa wale ambao mnatazama hesabu za kibenki, ukwasi wa Bodi ya Mikopo, kihasibu, kifedha umefikia shilingi trilioni 7.2 huu ni uwekezaji uliofanyika kwa miaka 20 iliyopita ambazo zimekwenda kwa wanufaika 750,000.
“Kama hii investment isingekuwepo kungekuwa na upungufu mkubwa wa watenda kazi wenye ujuzi katika taaluma mbalimbali.”
Amesema, hadi kufikia Septemba, mwaka huu kuna kiasi cha mkopo ambacho kimekusanywa ambacho kinakadiriwa kufikia shilingi trilioni 1.3 kutoka kwa wakopaji zaidi ya 230,000. Aidha, amesema kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 700 cha mikopo hiyo zimeiva, lakini hazijakusanywa.
“Tuna kazi ya kujenga utamaduni miongoni mwetu wa unapokopa basi unalipa, waajiri ni wakala wetu wakubwa,lakini bado waajiri fulani fulani hawawasilishi kwa wakati, na wengine wanawasilisha makato ambayo yana upungufu,”amefafanua Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kuwa, bodi imefanikiwa kukusanya shilingi trilioni 1.34, kati ya shilingi trilioni 2.1, kutoka kwa wanufaika wa mikopo sawa na asilimia 64.
"Jumla ya makusanyo tangu 2005/06 hadi sasa ni shilingi trilioni 1.34 kati ya shilingi trilioni 2.1 zilizoiva sawa na ufanisi wa asilimia 64,"amefafanua Badru.
Badru amesema kuwa, wanaendelea kuwafuatilia wanufaika wa mikopo hiyo ambao ni wanafunzi wa elimu ya juu ili waweze kulipa na kutumika kwa wahitaji wengine.
Amesema kuwa, kwa upande wa utoaji mikopo, bodi yake haina upendeleo wowote, wanafuata kanuni na taratibu zilizowekwa katika kuwapatia mikopo wanafunzi.
"Kwa sasa tunawaomba watanzania walionufaika na mikopo, warejeshe ili fedha hizo ziwasaidie wengine, pamoja na hayo tunawaomba watanzania kutoa ushirikiano ili kuwapata wanufaika waanze kurejesha fedha hizo,"amesema.
Amesema, kwa upande wa wanufaika kutoka sekta isiyo rasmi, wengi wameshindwa kujitokeza kwa hiari kurejesha mikopo waliyochukuwa, huku baadhi ya waajiri wakishindwa kuwasilisha makato sahihi na kwa wakati.
"Tunawashukuru waajiri na wanufaika kwa urejeshaji, kuna baadhi ya wanufaika ambao wameendelea kulipa kwa mkupuo salio baada ya kuondolewa kwa tozo ya kulinda thamani ya fedha m(VRF) na tozo ya adhabu (penalty).
"Pia, kuna mambo yaliyojitokeza ikiwemo athari za ugonjwa wa UVIKO-19 na changamoto nyingine ni wanufaika walio katika sekta binafsi na zisizo rasmi kutokuwa na utayari wa kujitokeza na kulipa madeni yao."
Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa, wanakamilisha ushirikiano wa kimkakati na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mfuko wa HIfadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na wakala wa Biashara na Leseni (BRELA).
Ameongeza kuwa, mbali na taasisi hizo, pia atawashirikisha viongozi wa serikali za Mtaa na vijiji ili kuwabaini wanufaika.
Mkurugenzi Mtendaji pia ameeleza, kuna mpango wa HESLB kuzindua kampeni ya #Fichua inayolenga kuwahamasisha wananchi wazalendo mitandaoni kuwafichua wanufaika wenye vipato, lakini hawajaanza kurejesha
"Tunaanzisha kampeni ya #Fichua ili wananchi watoe taarifa za wanufaika wasiojitokeza kwa hiari kwa ajili ya kurejesha mikopo yao Bodi ya Mikopo,"amesisitiza Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Ameongeza kwamba, kwa sasa huduma zao zote zinapatikana kupitia mifumo ya TEHAMA (online), huku akiwataka wateja kutumia mfumo huo kupata huduma na kwamba, mifumo yao imeunganishwa na GovESB (e-GA).
"Tunahimiza kuunganisha mifumo ili kuongeza ufanisi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), imeendelea kutubeba katika utoaji huduma na taarifa kwa jamii.
"Huduma zetu zote zinapatikana kupitia mifumo ya TEHAMA (online). Wateja watumie mifumo hiyo kupata huduma,"amesema Badru.
TEF
Neville Meena ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Jukwaa la Wahariri Tannzania (TEF) akizungumza kwa niaba ya wahariri hao ameipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazini na HESLB kwa kuwa na mtazamo chanya katika utoaji huduma nchini.
Pia, Meena ameishauri bodi hiyo kuangalia namna ambavyo itaongeza fani ya uandishi wa habari kama kipaumbele katika utoaji mikopo.
"Sisi tunaandika kila kitu, hapa tumepewa mahesabu ili tukaripoti, ili uandike vizuri lazima elimu ifanye kazi, tufikirieni na sisi kwa sababu tunahitaji ujuzi wa hali ya juu katika kufanya kazi hii.
“Pia, ninawapongeza kwa mtazamo wenu chanya katika utoaji wa huduma hivi sasa tofauti na zamani, tuna wanahabari walionufaika na mikopo, wanaweza kutumika kama mabalozi wa urejeshaji,” amesema Meena.
Vile vile, amewakumbusha wanahabari kutumia taaluma yao kuhamasisha urejeshaji wa mikopo iliyoiva kwa kuwa fedha zikirejeshwa zitawanufaisha watanzania wengine wahitaji nchini.
Hazina
Akizungumzia kuhusu vikao kazi hivyo, Afisa Uhusiano na Mawasiiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri amesema kuwa, “Ofisi ya Msajini wa Hazina tunasimamia maslahi ya Serikali kwenye taasisi za umma, tunaamini kwamba mali ya Serikali ni mali ya umma.
"Kwa mashirika haya au hizi taasisi wadau wake wakubwa ni umma, umma unatarajia malengo ya kuanzishwa kwa taasisi na mashirika haya yaweze kutimia, kama wanatoa huduma iwe bora, kama wanafanya biashara basi iwe na faida kwa maslahi ya Taifa.”
Amesema, Ofisi ya Msajili wa Hazina kupitia kwa maono ya Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu aliona kuna changamoto kwa haya mashirika na taasisi kwamba yanafanya mambo mazuri, lakini hayafahamiki.
“Kwa hiyo fursa ya mikutano hii ni kuzikutanisha taasisi na mashirika ya umma yaweze kusema, malengo yao, mafanikio yao, changamoto zinazowakabali, walipotoka, walipo na wanapolekea.”
Vyeti
Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo wa HESLB, George Mziray amesema kuwa, wanaomaliza mikopo kwa sasa wanapewa vyeti ya kumaliza deni lao bila usumbufu.
Amesema, kwa sasa mfumo umeboresha hivyo ambao wamehitimu, wanafanya kazi zao na kupata kipato wajitokeze kwa wingi kuirejesha ili iweze kunufaisha wengine.
Hata hivyo, sheria na kanuni za Bodi ya Mikopo zimeainisha sifa na vigezo vya jumla kwa wanafunzi wahitaji wa mikopo.
Kwa mujibu wa bodi hiyo,mwombaji stahiki na mhitaji anaweza kuomba mkopo ili kugharamia sehemu au gharama zote za masomo ya elimu ya juu.
Tags
Bodi ya Mikopo
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
Elimu
Elimu ya Juu nchini Tanzania
Habari
Makala
Ofisi ya Msajili wa Hazina