NA GODFREY NNKO
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limerekodi mafanikio ya namna yake katika kipindi cha mwaka 2018/19 hadi 2021/22 ambapo limefanikiwa kutunisha Mfuko Mkuu wa Serikali kutoka shilingi bilioni 9.1 hadi shilingi bilioni 43.5.
"Mafanikio haya yamewezekana hasa kutokana na usikivu wa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kupokea ushauri mbalimbali wa kitaalam na kutoa maelekezo sahihi kupitia Wizara ya Uchukuzi;
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Nelson Mlali ameyabainisha hayo Oktoba 5,2023 wakati wa kikao kazi kati ya wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
"Tumefanikiwa kuongeza mchango katika Mfuko Mkuu wa Serikali, hii naomba muiangalie vizuri sana, ni taasisi changa imeanza kama miaka mitano iliyopita, lakini naomba muone huu mwendelezo wa uchamgiaji katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
"Nadhani Msajili wa Hazina ni shahidi katika hili, tumetoka bilioni tisa, lakini sasa tunazungumzia bilioni 43 ni ongezeko kubwa sana kuchangia mfuko wa serikali,"amesema Mlali.
Pia, amesema wamefanikiwa kufikia hatua hiyo kutokana na wao kuzingatia miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali pamoja na kamati za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sambamba na ushirikishwaji wa wadau wa sekta ya usafiri kwa njia ya maji katika masuala mbalimbali yanayoihusu sekta hiyo hapa nchini.
TASAC ambayo ipo chini ya Wizara ya Uchukuzi ilianzishwa chini ya Kifungu cha 4 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura ya 415 na kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake Februari 23, 2018 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 53 lilitolewa Februari 16, 2018.
Shirika hili lilianzishwa ili kuweza kutekeleza majukumu ya kusimamia usafiri kwa njia ya maji,usalama, ulinzi na udhibiti wa mazingira ya bahari dhidi ya uchafuzi utokanao na shughuli za meli, jukumu ambalo lilikuwa likitekelezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).
Mlali amesema, shirika hilo lina maono thabiti ambayo yanalenga kuhakikisha wanakuwa mdhibiti wa usafiri majini wa viwango vya ubora wa Kimataifa na kuwezesha Tanzania kuwa kitovu cha usafiri wa majini duniani.
Vile vile kudhibiti huduma za usafiri majini ili ziwe salama, shindani na rafiki kwa mazingira ili kuchangia katika ustawi wa jamii na Taifa.
Aidha, shirika hilo linatekeleza Mpango Mkakati wa Pili wa Miaka 5 (2021/22 hadi 2025/26) ikiwemo kutoa huduma zinazomjali mteja, ubunifu, uadilifu na uwajibikaji.
Wanavyowajibika
Mlali amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura ya 415, majukumu makuu ya TASAC yapo kwenye vifungu Na. 7, 11 na 12.
Amesema, miongoni mwa majukumu hayo ni kufanya kazi za Uwakala wa Forodha kwa bidhaa chache zenye maslahi mapana kwa Taifa.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo amefafanua kuwa, kazi hizo ni pamoja na ugomboaji na uondoshaji wa silaha za moto na vilipuzi ikiwemo makinikia.
"Nyingine ni kemikali zinazoagizwa na kutumika na kampuni za uchimbaji madini, nyara za Serikali na wanyama hai kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa wanyamapori nchini."
Mlali amesema, katika jukumu la uwakala wa forodha, shirika hilo huwa linahakiki nyaraka za wateja za uingizaji na uondoshaji shehena na kuratibu ufuatiliaji wa vibali kutoka mamlaka mbalimbali.
Pia, shirika huwa linaandaa kadhia kupitia mifumo ya forodha,kufuatilia malipo ya kodi na kufuatilia nyaraka za usafiri na usafirishaji kutoka kwa wakala wa meli.
"Na tunashiriki katika ukaguzi wa shehena kwenye maeneo ya kiforodha,kuratibu na kufuatilia ankara za malipo ya gharama za bandari, kuratibu usafirishaji wa shehena."
Aidha, amebainisha kuwa, TASAC inatoa ushauri kwa waagizaji na wasafirishaji wa shehena kuhusu taratibu za kiforodha kwa shehena zilizoainishwa hususani zinapoingia au kutoka nchini.
Wakati huo huo, TASAC inasimamia ulinzi na usalama wa usafiri majini na kuzuia uchafuzi wa mazingira utokanao na shughuli za usafiri majini.
"Katika kutekeleza majukumu haya, TASAC inasimamia utekelezaji wa Sheria ya Usalama wa Vyombo vya Majini, Sura ya 165 (The Merchant Shipping Act, Cap. 165) ikiwemo utekelezaji wa mikataba ya Kimataifa kuhusu Usafirishaji Majini inayoratibiwa na Shirika la Bahari Duniani (International Maritime Organization-IMO),
"Na tunafanya ukaguzi wa meli zilizosajiliwa nchini na meli za nje zinazoingia katika bandari za Tanzania Bara,kudhibiti vivuko (ferries) na kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji majini."
Akizungumzia kuhusu shughuli za utafutaji na uokoaji majini, Mlali amesema, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) linaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa boti za uokozi katika Ziwa Victoria, Tanganyika na Ziwa Nyasa.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, wanaendelea na utekelezaji wa ujezi wa boti hizo tano za uokozi ambapo mbili zitakuwa Ziwa Victoria, mbili Ziwa Tanganyika na moja Ziwa Nyasa.
"Tunatekeleza ujenzi wa boti tano za uokozi ambapo tunataka tuweke pale Ziwa Victoria boti mbili, Ziwa Tanganyika mbili na pale Ziwa Nyasa boti moja.
"Taratibu zimeshaanza kuangalia uwezekano wa kufanya vitu hivyo ili baadae tufike mahala tuweze kuwa na boti hizo za uokozi ambazo zitakuwa tayari kukimbia katika maeneo ya matukio kwenye maeneo ya karibu,"amefafanua Mlali.
Mbali na hayo amesema, wanaendelea kudhibiti utunzaji wa mazingira dhidi ya uchafuzi utokanao na shughuli za meli na kutoa taarifa na uelewa kwa umma kuhusu masuala ya ulinzi, usalama na mazingira majini.
"TASAC, pia tunatoa leseni, kuzihuisha na kufuta kwa wale ambao wanakuwa wameshindwa kutekeleza matakwa na taratibu za viwango vinavyodhibitiwa.
"Lengo ni kuzifanya bandari zetu ziweze kupata sifa nzuri duniani, lakini pia tunaweka masharti yanayodhibiti tozo miongoni mwa watoa huduma kuweka usawa wa ushindani ili kutoharibiana biashara.
"Vile vile tunasimamia mienendo ya watoa huduma katika sekta na kutoa taarifa kuhusu nafasi na masuala mbalambali yanayohusu majukumu ya shirika."
Amesema, pia wana jukumu la kudhibiti watoa huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji nchini ambalo linawahusu watoa huduma baharini,maziwani na bandari kavu.
Mafanikio
Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo amebainisha kuwa, TASAC tangu kuanzishwa kwake hapa nchini inajivunia mafanikio mbalimbali ikiwemo utatuzi wa kero mbalimbali.
""Naomba nieleze mafanikio yaliyopatikana na yanayoendelea kupatikana kama ifuatavyo, kwanza tukefanikiwa kuongeza idadi ya kadhia kutoka 6000 mwaka 2020 hadi zaidi ya kadhia 10,000 mwaka 2021/22.
"Hapa ninaomba tu muone kwamba ndani ya kipindi kifupi, lakini uhuduumiaji kadhia umekuwa na mafanikio kwa idadi inavyojieleza."
Kwa mujibu wa Mlali idadi ya nyenzo za udhibiti imeongezeka mwaka 2018 kutoka nyenzo tano hadi zaidi ya 20 mwaka 2022.
"Lakini pia tuemefanikiwa kuunda nyenzo ambazo zinadhibiti, nyenzo hizi ni pamoja na kanuni na miongozo mbalambali ili ziweze kuongoza na kuleta nidhamu katika sekta yetu ya usafiri wa maji.Lengo ni sekta yetu ya usafiri majini iweze kuwa salama."
Aidha, amesema TASAC imefanikiwa kuongeza idadi ya watoa huduma wanaodhibitiwa na shirika hilo kwa maana ya idadi ya leseni na vyeti vya usajili vilivyotolewa.
Mlali amesema, shirika hilo limetoa vyeti vya usajili 1,038 mwaka 2021/22 kutoka 796 mwaka 2018/19 na limetoa leseni 240 mwaka 2021/22 kutoka 145 mwaka 2018/19.
“Pia shirika limeongeza idadi ya vyeti vinavyotolewa kwa mabaharia waliokidhi masharti na kufikia vyeti 17,689 mwaka 2021/22 kutoka 5,699 mwaka 2018/19 na imeongeza idadi ya leseni za vyombo vidogo kutoka 2,006 mwaka 2018/ hadi 6,366 mwaka 2022,” alieleza Mlali.
MLVMCT
Katika hatua nyingine Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, TASAC inatekeleza Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria (Multi-National Lake Victoria Maritime Communication and
Transport- MLVMCT) unaotarajiwa kukamilika Desemba, 2024.
“Shirika pia linatekeleza mradi wa Kimataifa wa mawasiliano na uchukuzi katika Ziwa Victoria, ambao ni mpana sana, lengo lake ni kuboresha mawasiliano na kusaidia katika shughuli za uokoaji zinapotokea ajali ili watu waweze kuwasiliana, na msaada wa karibu uweze kufika.
“Ziwa letu ni kubwa katika eneo tunalolimiliki, mradi huu umelenga kuwasaida watu wa kawaida kabisa, kwa hiyo Serikali imefanya jitihada kubwa ili kuwafikiria watu wa chini,"amesema.
Meli
Amesema, TASAC imejidhatiti kuhakikisha huduma za usafirishaji kwa njia ya maji zinatolewa kwa ubora, ufanisi na kwa wakati.
Huduma za udhibiti zimegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni udhibiti huduma za bandari na udhibiti huduma za usafirishaji kwa njia ya meli.
"Tumefanikiwa kuongeza kaguzi za meli za kigeni, kaguzi hizi kazi kubwa sana ni kuhakikisha usalama kwa sababu kama vyombo vinakuja lazima tuvikague vizuri,kisha tunatoa taarifa ambazo zinaheshimiwa katika bandari zile meli zinaenda."
Mhandisi Said Kaneko akizungumzia meli za kigeni zinazoingia nchini amesema, pamoja na changamoto za wataalamu wa ukaguzi wa meli za kigeni uliopo nchini hadi sasa kuna wataalamu 16 pekee ambao wamefanikiwa kukagua meli 39 kutoka meli 7.
Amesema, takwimu zinaonesha ongezeko la kaguzi za meli za kigeni kutoka meli saba mwaka 2018. meeli nne mwaka 2019, meli tatau mwaka 2020, meli 13 mwaka 2021 na meli 39 mwaka 2022.
Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC amesema kuwa, wamefanikiwa kufanya sensa ya kwanza ya vyombo vidogo vya usafiri majini vinavyotumika katika usafirishaji wa abiria, mizigo na uvuvi katika maeneo yote yenye maji ikiwemo bahari, maziwa, mito na mabwawa kwa Tanzania Bara.
Amesema, sensa ilibaini kuwa idadi ya vyombo vidogo vya majini ni 52,189. Kati ya vyombo hivyo, vyombo vidogo vya majini vyenye urefu wa mita nne na zaidi ni 45,976 sawa na asilimia 88.
Fursa
Mlali amewashauri Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya biashara na usafiri majini kwa kushiriki kuanzisha usajili wa meli kwa masharti rafiki,uanzishwaji wa maeneo ya ukarabati na ujenzi wa meli katika Ukanda wa Pwani.
Fursa zingine amesema, ni uanzishwaji wa maegesho ya boti ndogo katika Ukanda wa Pwani,uanzishwaji wa viwanda vya utengenezaji malighafi za ujenzi wa boti za plastiki,ujenzi wa bandari rasmi za uvuvi na kukidhi mahitaji ya soko la Comoro.
“Zipo fursa nyingi katika sekta ya usafirishaji wa majini.Ipo fursa ya kusajili meli kwa njia rafiki na fursa ya kuwekeza katika vituo vya kufanya matengenezo ya vyombo vya majini.”
Mlali amesema,miongoni mwa sababu zinazowafanya kuzidi kuwa kinara katika sekta ya usafiri majini ni kutokana na ushirikiano mkubwa walio nao na wadau.
“Pia tunawakaribisha katika kuanzisha maegesho kwa ajili ya vyombo vya majini hususani boti, uanzishaji wa viwanda vya malighafi za utengenezaji wa boti za plastiki, fursa za uanzishwaji wa bandari za uvuvi, fursa ya kukidhi mahitaji ya visiwa vya Comoro.
“Kumekuwa na changamoto kadhaa wakati mwingine wa kushindwa kukidhi mahitaji ya watu wa Comoro, hivyo kuna fursa katika eneo hili.”
Amesema, Comoro wanategemea huduma nyingi kutoka nje ya nchi ambapo Tanzania ina bahati kubwa ya kuwa karibu na visiwa hivyo hususani kupitia Bandari ya Mtwara.
Mlali amesema, mahitaji kama mifugo hususani mbuzi, ng’ombe na samani mbalimbali kutoka nchini zina mahitaji makubwa nchini Comoro.
“Hivyo, kuna umuhimu wa kuwekeza katika eneo hili na hata umiliki wa vyombo vya usafirishaji majini, kwani tukiwa tayari kuwekeza kuhudumia watu wa Comoro ninadhani na hata wao watafarijika kuliko kuendelea kuagiza bidhaa kutoka mbali huko.”
Pia, amesema wamedhamiria kuweka msukumo wa kuhamasisha vijana wa Kitanzania ambao watasomea fani mbalimbali zinazohusiana na sekta ya biashara na usafirishaji majini.
TEF
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatius Balile ameendelea kumpongeza Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu kwa kuja na wazo jema ambalo linawezesha taasisi na mashirika yaliyopo chini ya ofisi yake kuweza kuyaeleza yale ambayo wanayafanya kwa kina huku wahariri wakipata nafasi ya kujadiliana na kuuliza maswali mbalimbali.
Amesema, utaratibu huo ni wa kipekee kutokana na umuhimu wa taasisi hizo ambazo wamiliki wakuu ni Watanzania wenyewe, hivyo kupitia vyombo vya habari wanapata nafasi ya kujua mikakati na mwelekeo wao.
Vile vile, Balile ameipongeza TASAC kwa utendaji wake na kuwashauri kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya fursa mbalimbali zinazopatikana katika biashara na usafirishaji majini.