Vitendo vya ubakaji, mimba kwa watoto Zanzibar havikubaliki

ZANZIBAR-Mbali na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar za kuongeza umakini katika upatikanaji wa haki za watoto wa kike, lakini bado watoto hao wanaendelea kukabiliwa na changamoto za kubakwa na mimba za mapema.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Riziki Pembe Juma alisema hayo katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo,Mhe.Anna Athnas Paul katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike, yaliofanyika jana katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil, Kikwajuni, Unguja.

Alisema,Serikali imekuwa ikifanya jitihada kuongeza umakini katika upatikanaji wa haki za watoto wa kike, lakini bado watoto wanaendelea kukabiliwa na changamoto zinazohusu usalama wao ikiwemo kubakwa na mimba za mapema.

Aliezea, kwamba jumla ya matukio 1,081 ya ukatili na udhalilishaji yameripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Agosti 2023 kwa mujibu wa takwimu za Mtakwim Mkuu wa Serikali. Alisema,kati ya matukio hayo matukio 838 yanahusu watoto wa kike.

“Vitendo hivyo hupunguza nguvu kazi ya jamii katika ukuzaji wa shughuli za maendeleo, kukatiza ndoto zao za maisha na kudumaza ukuaji wao na maendeleo kwa ujumla,”alisema Waziri huyo.

Alisema, katika kukabiliana na changamoto hiyo Serikali imeendelea kuboresha huduma za malezi ya watoto wakiwemo wasichana kwa kutoa mafunzo ya malezi mazuri kwa wazazi na walezi kwa nia ya kuwezesha makuzi bora ya watoto katika Shehia, Wilaya na Taifa.

Alifafanua kwamba,familia 530 na watendaji wapatao 60 wamejengewa uwezo wa elimu ya malezi ili waweze kuzifikia jamii kwa ujumla. Hivyo, hatua hiyo imetoa mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

Naye Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Siti Abass Ali amewataka watoto wa kike kufanya bidii katika masomo yao ili waje kuwa viogozi katika nyanja mbali mbali.

Alisema, Sheria ya Mtoto Namba 6 ya mwaka 2011 imekusanya haki za mtoto ikiwemo haki ya kupata matibabu, kupatiwa amani na ulinzi, kupata elimu hivyo mtoto wa kike anawajibu wa kusoma, hivyo amewataka watoto hao kuwa na msimamo wa kutokujiingiza katika vitendo viovu na kujiamini kwamba wanaweza kuwa viongozi katika bunge, kampuni, jamii, nk.

Naye mtoto wa kike jina limehifadhiwa ambaye ni mwanafunzi wa skuli ya msingi Kiswandui ameishauri Serikali kwamba mtu yeyote anayefanya kitendo kibaya kwa mtoto afungwe jela maisha kwa sababu akitolewa ataanzisha makundi maovu katika jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news