Wananchi Dar mtapata makazi bora-TBA

DAR ES SALAAM-Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umewahikishia wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kupata makazi bora yanayokidhi mahitaji ya teknolojia ya kisasa.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya nyumba za makazi katika Maeneo ya Temeke Kota, Magomeni Kota na Masaki Mkurugenzi wa Idara ya Miliki FRV. Said Mndeme amesema TBA imeazimia kutekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi ili kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba bora za makazi nchini.

Aidha, amesema anaishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kutenga fedha zaidi bilioni 60 ndani ya miaka miwili kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mpya za makazi.

"Katika eneo la Temeke Kota unaendelea ujenzi wa jengo moja la sakafu tisa (9) lenye uwezo wa kuchukua familia 144 ambapo mpango wetu kama Wakala ni kuhakikisha eneo hilo limakuwa na majengo saba yenye uwezo wa kuchukua familia 1008," amesema Mndeme.

Pia ametoa ufafanuzi juu ya miradi inayoendelea kutekelezwa katika maeneo ya Magomeni Kota awamu ya Pili na Msasani Peninsular Masaki kuwa katika maeneo hayo TBA inaendelea kuhakikisha inakamilisha majengo ya kisasa yatakayokuwa na huduma zote za msingi.

"Katika Maeneo ya Magomeni Kota na Canadian Masaki tumekamilisha majengo mawili ambayo yalizinduliwa na sasa tunaendelea na ujenzi wa ghorofa ambalo limefikia 83% na matarajio yetu mwezi Januari 2024 litaanza kutumika.

"Pia katika eneo la Masaki tunaendelea na ujenzi wa majengo mawili yenye uwezo wa kubeba familia 24 ambayo yamefikia 53%, ambayo tunatarajia kuwa na wakaazi 472 pamoja na uwepo wa maduka ya kisasa,”amesema Mndeme.

Awali akizungumza Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Dar es Salaam, Arch. Benard Mayemba amesema miradi yote itakamilika kwa wakati kwa kuzingatia viwango vya ubora pamoja kuhakikisha mahitaji yote ya msingi yanazingatiwa ili nyumba hizo ziweze kwenda kutatua changamoto ya makazi kwa jamii iliyokusudiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news