Mara wanolewa kuhusu dawa za kulevya

MARA-Wapelelezi na waendesha Mashtaka wa Serikali wa Mkoa wa Mara wamekumbushwa kutumia weledi na kuzingatia taratibu za kisheria ili kuhakikisha mashauri ya dawa za kulevya yanamalizika katika hali ya kufanikiwa.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 4,2023 katika Ukumbi wa Bwalo la Polisi mjini Musoma Mkoa wa Mara na Kamishna wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Bi. Veronica Matikila wakati akiwasilisha mada juu ya upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya dawa za kulevya kwa kundi hilo. Kupitia kikao kazi hicho, zaidi ya washiriki 101 wamepatiwa mafunzo.
Mada zilizojadiliwa ni pamoja na aina za ushahidi, namna kuthibitisha makosa ya dawa za kulevya na maeneo muhimu ya kuzingatia kwa waendesha mashtaka katika kuongoza upelelezi wa kesi za dawa za kulevya.
Aidha, akizugumzia mafunzo hayo, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Mtwara,Joseph Mauggo amesema, mafunzo haya yanafanyika kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya,
Sambamba na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai kuhakikisha wanafanya mafunzo endelevu kwa maafisa wanaopeleleza na wanaoendesha mashauri ya dawa za kulevya ili kukabiliana na changamoto za kiutendaji pamoja na kubadilishana uzoefu juu ya upelelezi na uendeshaji mashauri hayo.
"Mnamo mwezi Juni mwaka 2023 Mheshimwa Waziri Mkuu ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya aliekeza kuundwa kwa Tume ili kufanya tathmini ya mwenendo wa kesi za dawa za kulevya."
Miongoni mwa mambo yaliyobainika na Tume hiyo ni kwamba Serikali inapoteza kesi nyingi na moja ya sababu ya kupoteza kesi hizo ni kutokuwa na uelewa wa pamoja wa watendaji muhimu kwenye masuala ya dawa za kulevya" amesema Maugo.
Ameongeza kuwa nia ya mafunzo ni kujengeana uelewa wa pamoja na kutatua changamoto na malalamiko ya wananchi ili hata jamii ione na kutambua jitihada zinazofanyika kwenye suala la dawa za kulevya.
Mafunzo kwa Waendesha Mashtaka na Wapelelezi ni muendelezo wa mafunzo yaliyotangulia katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, na Iringa yanayotolewa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news