TANGA-Wananchi wanaomiliki silaha kinyume na sheria mkoani Tanga wametakiwa kutii sheria bila shuruti na kuzisalimisha kwa Jeshi la Polisi kwani zoezi hilo litafikia mwisho ifikapo Oktoba 31, mwaka huu ambapo badala ya siku hiyo sheria kali itachukuliwa dhidi ya atakayekutwa anamiliki.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi ametoa wito huo wakati matembezi maalumu ya kulinda amani ya jeshi hilo na kusema kuwa, muda ambao umetolewa ili kila aliyenayo aisalimishe ili hatua isichukuliwe dhidi yake.
"Niwatake wananchi katika Mkoa wa Tanga, wilaya zote, hata kama ndugu yako alikuwa anamiliki na amefariki inapaswa kuletwa polisi na kusalimishwa, lakini pia mtu kama anayo silaha na anajua kuwa anaimiliki isivyo halali aisalimishe kituo cha polisi au katika ofisi za watendaji hawatashtakiwa.
"Katika kipindi hiki ambacho Waziri wetu wa Mambo ya Ndani ya Nchi ametoa msamaha wa kuwasamehe wanaosalimisha silaha kwa hiari, lakini kwa watakaokaidi, niwatangazie kabisa kuwa kutakuwa na msako mkali usiokoma kwa maana wapo watu wanatengeneza silaha kama magobore halafu wanayatumia kufanyia uhalifu,"amesema.