DODOMA-Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Stanlaus Nyongo ameishauri Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu (TB) na Ukoma kuongeza juhudi za utolewaji wa elimu kwa jamii na upimaji wa TB.
Mhe. Nyongo amesema hayo Oktoba 23, 2023 baada ya kupokea taarifa ya mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu pamoja na taarifa ya huduma za mama na mtoto kutoka Wizara ya Afya iliyowasilishwa kwenye Kamati hiyo katika kumbi za Bunge Jijini Dodoma.
“Kwanza niwapongeze sana Wizara ya Afya mnafanya kazi nzuri ya kuwatumikia Watanzania lakini pia niwaombe kupitia mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma izidi kutoa elimu kwa jamii na upimaji hasa katika kampeni kubwa kubwa ili kuwagundua wagonjwa mapema na kuwaanzishia matibabu kwa lengo la kupunguza zaidi maambukizi,"amesema Mhe. Nyongo
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema elimu ikiendelea kutolewa na jamii ikaelewa vizuri itasaidia kupunguza maambukizi pamoja na vifo vitokanavyo na Kifua Kikuu nchini.
Amesema, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2022 Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuwaibua wagonjwa wa TB na kuwapatia matibabu kutoka asilimia 37 hadi asilimia 65.
Aidha, Waziri Ummy amesema lengo la Shirika la Afya Duniani ni kuibua wagonjwa wa Kifua Kikuu ambapo Tanzania imefanikiwa kwa 65% lakini pia kupunguza vifo vitikanavyo na ugonjwa huo, Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Ili kuzidi kufanikiwa hilo kwa Tanzania Waziri Ummy ameitaka jamii iache tabia ya kuwaficha wagonjwa wa TB bali ichukue hatua za kuwapeleka katika vituo vya kutolea huduma za Afya mapema ikiwa watagundua dalili za ugonjwa huo.
“Familia ikiwa na mgonjwa wa Kifua Kikuu inatakiwa kutoa taarifa mapema ili isaidiwe haraka na Serikali itimize matakwa ya WHO ya kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo pamoja na vifo,” amesema Waziri Ummy.
Pia, Waziri Ummy amesema watu 70 hufariki kila siku kutokana na ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini Tanzania hali ambayo imekuwa ikishusha nguvu kazi katika jamii pamoja na uchumi wa nchi kwa ujumla.
“Ikitokea ajali ikaua watu 70, Watanzania watashtuka sana na kila sehemu tutaona pole zikitolewa lakini tufahamu kuwa watu 70 hufariki kila siku kutokana na ugonjwa wa TB lakini kwa sababu hatuwaoni kutokana wanakufa sehemu mbalimbali nchini nzima ndio maana hatuchukulii maanani,”amesema Waziri Ummy.