Wazee Zanzibar wapendekeza umri wao uanzie miaka 60 badala ya 70

ZANZIBAR-Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeida Rashid Abdallah amesema, wizara hiyo imepokea maoni yaliyotolewa na wazee kuhusu kuifanyia marekebisho Sheria ya Masuala ya Wazee, Sheria Na.2 ya mwaka 2020 katika kifungu kinachozungumzia umri wa mzee.
Akizungumza baada ya kikao cha pamoja baina ya watendaji wa wizara hiyo,Kamati ya Kanuni na Sheria ndogo ndogo ya Baraza la Wawakilishi, wazee kutoka Jumuiya ya Wazee (JUWAZA) pamoja na wazee wanaoishi katika makao ya wazee, kilichofanyika katika Ukumbi wa Makao ya Wazee Sebleni, Unguja.

Alisema, wazee wametaka kifungu cha sheria hiyo kifanyiwe marekebisho umri wa mzee uwe miaka 60 badala ya miaka 70. Hivyo watendaji wa wizara hiyo watakaa chini na kutafakari.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Sheria ndogo ndogo za Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Mihayo Juma N'hunga (kulia) akiongea na wazee wanaolelewa katika Makao ya Wazee Welezo, Unguja,Oktoba 27,2023.

“Kamati imekuja kututembelea katika makao ya wazee, pamoja kupata maoni ya kanuni, ya masuala ya wazee iliyotungwa hivi karibuni lakini majadala mkubwa umejitokeza, baada ya kanuni hiyo kuonesha umri wa mzee ni miaka 70, na umri huo umewekwa kwa mujibu wa sheria ya masuala ya Wazee, hivyo wazee wametaka turudi kwenye sheria tuifanyie marekebisho,”alisema Katibu Mkuu huyo.

Aidha, alisema kwamba Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi amewaagiza watendaji wake kwamba endapo sheria ikionekana inaleta changamoto basi ifanyiwe marekebisho ili iendane na wakati uliopo.

Alisema zaidi wajumbe wa kamati hiyo katika kikao cha majumuisho watatoa maelekezo kuhusiana na hilo, pamoja na wadau wengine ambao wanafanya kazi katika jumuiya za wazee katika kusimami masuala ya wazee.

Alieleza muda sio mrefu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto itatoa elimu dhidi ya kanuni ya Masuala ya Wazee (Utowaji Huduma za Makaazi ) kupitia makundi mbali mbali ndani ya jamii ili kila mtu aifahamu kanuni hiyo. kwani kanuni hiyo imetoa fursa mtu yeyote anaweza kuanzisha Makao ya Wazee.


Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mwera Mhe. Mihayo Juma N’Hunga amesema wako katika utaratibu wa kuchua maoni kwa wadau na kuangalia kama Kanuni hiyo inafanya kazi na kama kuna mapungufu basi ifanyiwe marekebisho.

Alisema, kanuni hiyo imetungwa mwezi Aprili, mwaka huu, hivyo kamati inafuatilia utekelezaji wake na ndio maana walianza na ziara ya kuwatembelewa wazee katika makao ya Wazee, Limbani Pemba, na kwa upande wa Unguja Welezo na Sebleni na kuwauliza masuala mbali mbali kuhusiana na kanuni.
Kwa upande wa Wazee akizungumza Bi Salama Kombo Ahmed kwa niaba ya wazee wa Jumuiya wa Wazee Zanzibar (JUWAZA) alisema Serikali ya Zanzibar inamuachisha mtu kazi anapofikia umri wa miaka 60 na sio 70, hivyo sheria ifanyiwe marekebisho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news