Waziri Kairuki aanika maboresho ya utalii, awakaribisha wawekezaji

NA JOHN MAPEPELE

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amesema Serikali ya Tanzania inafanya maboresho makubwa kwenye miundombinu sekta ya utalii na amewakaribisha wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja kuwekeza nchini kwa kuwa Tanzania imejaaliwa kuwa na maliasili za kipekee, vivutio vya kitamaduni na maeneo marefu ya fukwe za Tanzania Bara na Zanzibar.

Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo katika siku ya pili ya Maonesho ya Saba ya Swahili International Tourism Expo - S!TE, 2023 leo Oktoba 7,2023 wakati akifungua Jukwaa la Uwekezaji jijini Dar es Salaam linalojulikana kama "Uwekezaji Endelevu kwa Maendeleo Jumuishi ya Kijamii na Kiuchumi".

Mhe. Kairuki amesema pamoja na kazi kubwa ya kuboresha miundombinu iliyofanywa na kusaidia kuleta watalii pia amefafanua kuwa ongezeko kubwa la watalii limetokana na kazi nzuri iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya “The Royal Tour”. Filamu hii ilionyeshwa katika vituo vingi vya televisheni vinavyotambulika nchini Marekani na kwingineko duniani ili kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania.

Amesema The Royal Tour na juhudi nyingine za masoko umesababisha kuongezeka kwa idadi ya watalii waliofika kutoka nje ya nchi imeongezeka kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi watalii 1,454,920 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 57.7. Aidha, idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi 2,363,260 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 199.5.

Aidha amesema utalii umeendelea kuwa msingi wa ukuaji wa uchumi wa nchi ambapo amefafanua kuwa sekta, inachangia hadi 17.2% ya jumla ya Pato la Taifa na 25% ya mapato yote ya mauzo ya nje ambapo amesema kuna sekta inaweza kuchangia zaidi kwenye uchumi zaidi pia baada ya kupatikana kwa bidhaa mpya za utalii kama utalii wa mikutano na utalii wa meli ambazo kwa sasa Serikali inafanya kazi.

Akitoa mada kwenye Jukwaa la Uwekezaji Naibu Kamishna wa Uhifadhi kutoka Hifadhi ya Ngorongoro Imani Richard Nkuwi amefafanua kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii na Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imepokea andiko la mradi (project proposal) unaotambulika kama “Development of Water Front and Cruising Ship Terminal” kutoka kwa Mkandarasi tarajiwa. Mradi husika unatarajiwa kugharimu takribani kiasi cha USD 300 milioni na utahusisha ujenzi wa gati la mizigo ya mwambao na ujenzi wa gati la meli za kitalii pamoja na uendelezaji wa ufukwe wa Bahari ya Hindi jirani na gati la meli za kitalii. Ujenzi wa miundombinu husika unategemewa kuanza kabla ya mwaka wa fedha 2023/24.

Mhe. Waziri amezitaja baadhi ya juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha miundombinu kuwa ni pamoja na Reli ya Standard Gauge (SGR) ambayo iko katika hatua za mwisho kukamilika inalenga kuunganisha Jiji la Dar es Salaam kama lango kuu la watalii wanaofika njia ya kati na Kusini, kuimarisha Shirika la Ndege la Taifa kwa kuongeza idadi ya safari za ndege ili kuimarisha utalii kuunganishwa kwa kanda mbalimbali za kitalii za Tanzania.

Pia ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal 3 na ukarabati wa Viwanja vya Ndege vya Mikoani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news