SINGIDA-Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameutaka Mgodi wa Singida Gold Mine unaomilikiwa na Kampuni ya Shanta Mine kuharakisha ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopo ndani ya eneo la leseni ambao walikuwa bado hawajalipwa.
Amesema hayo leo Oktoba 14, 2023 alipotembelea Mgodi huo wilayani Ikungi mkoani Singida kujionea maendeleo ya mradi huo.
Waziri Mavunde amesema kuwa mgodi huo umefanya kazi kubwa ya kuhakikisha wanatimiza masharti ya leseni ya uchimbaji hivyo ni muhimu kuharakisha ulipaji wa fidia kwa wananchi waliokuwa bado hawajalipwa.
“Niwapongeze kwa hatua mliyopiga ndani ya kipindi kifupi, niwahimize kuharakisha suala la fidia kwa wananchi ambao bado, hii itawasaidia nyie kufanya shughuli zenu bila malalamiko ya wananchi wa maeneo yanayowazunguka, na kwa kuwa wamebaki wachache naamini halitachukua muda mrefu sana" amesema Mavunde.
Pia, Mhe. Mavunde ameuhimiza Mgodi wa Singida kuendelea kuboresha mahusiano mazuri na wananchi wanaozunguka mgodi huo kwa kuendelea kuwaboreshea miundombinu yao kupitia Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) pamoja na kuwapa kipaombele wazawa katika utoaji wa huduma katika mgodini kama sheria inavyotaka.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Singida Gold Mine, George Kondela amesema kuwa tayari Mgodi umewalipa fidia ya ardhi wananchi 236 na kuwajengea nyumba wananchi 12, na kwamba wanashughulikia fidia ya ardhi kwa wananchi 53 waliosalia na nyumba za wananchi 10.
Aidha, ameongoza kuwa mgodi huo unaendeshwa na wazawa kwa asilimia 100 kwa hatua zote kuanzia kwenye usanifu, ujenzi na uendeshaji.