Waziri Mkuu ashuhudia ng'ombe wenye uwezo wa kuzalisha lita 35 hadi 70 za maziwa kwa siku

MILAN-WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea shamba la ufugaji wa ng'ombe wa maziwa la Alesandra lilipo Milan nchini Italia, ambalo linaendeshwa kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kielektoniki ikiwemo ukamuaji wa maziwa kwa kutumia roboti.

Akiwa katika shamba lenye takribani ngombe 500 Mheshimiwa Majaliwa ameshuhudia mifumo bora ya ufugaji, ulishaji , unyonyeshaji na ukamuaji wa maziwa, ambapo ng'ombe mmoja anauwezo wa kutoa lita kuanzia 35 hadi 70 kwa siku na kumuwezesha mfugaji kupata tija zaidi.

Waziri Mkuu alitembelea shamba hilo Oktoba 19, 2023 na alionesha kufurahishwa na teknolojia inayotumika katika ufugaji huo. Waziri Mkuu yuko nchini Italia akimuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023, Rome nchini Italia.

Viongozi wengine walioambatana na Mheshiwa waziri Mkuu kutembelea shmba hilo shamba hilo ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamata Shaame Hamisi ambaye alisema amefurahishwa na misingi bora ya ufugaji na kwamba utaratibu huo ukitumika nchini utaongeza tija katika sekta ya mifugo.

Alisema aina ya ufugaji inayotumika kwenye shamba hilo kuanzia hatua uandaaji wa malisho, ukamuaji wa maziwa, usafirishaji na utunzaji wa mifugo aliojifunza shambani hapo atakwenda kuufanyia kazi kwa lengo la kuimarisha sekta ya mifugo ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato kwa wafugaji na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema amefurahishwa na namna ya uendeshaji katika shamba hilo ambalo pia wanafanya kilimo mseto kwa kufuga, kulima malisho ya mifugo na kutumia kinyesi cha ng'ombe kuzalisha nishati ambayo wanaitumia kwa shughuli za shambani na ziada kuuza kwenye gridi ya Taifa.

Alisema jambo jingine lililomfurahisha katika shamba hilo ni namna ambavyo mifugo yao imewekewa hereni za kielektroniki kwa ajili ya utambuzi ambazo zinaiwezesha nchini kujua idadi ya ng'ombe pamoja na maendeleo yake ikiwemo kutambua magonjwa, hivyo atakutana viongozi wa sekta husika ili kuangalia namna bora ya kuboresha ufugaji nchini.


Naye, mfugali wa ng'ombe kutoka Wami Sokoine, Morogoro, Mainga Ole Kalaita ambaye alitembelea shamba hilo kwa ajili ya kujifunza ufugaji bora alisema amepata elimu ya ufugaji bora na atakwenda kuwashauri wafugaji wenzake nchini wabadilike ili waendane na mahitaji ya sasa ya soko ikiwa ni pamoja na kubadili njia za ufugaji. “Hakuna haja ya kuwa na mifugo mingi isiyokuwa na tija, tubadilike tufuge kisasa.”

Ole Kalaita alisema kuwa kuna haja ya wafugaji nchini kukubali mifugo iwekewe hereni kwa ajili ya utambuzi wa aina ya uzao wa ngombe kwani katika masoko ya kimataifa lazima wahoji historia ya mfugo, aliiomba Serikali iendelee kuwaelimisha wafugaji umuhimu wa kuwa na taarifa za mifugo.

Awali, mmiliki wa shamba hilo, Bibi Alessandra Soresina alisema katika shamba hilo wanatumia teknolojia ya uhimilishaji wa mifugo kwa lengo la kuwa na kosafu za mifugo yao. 

"Teknolojia hiyo inawasaidia kuwa na uhakika wa kuwa na muendelezo mzuri wa ng'ombe wanaotoa maziwa kwa wingi. “Wakati mwingine hutumia akili bandia ili kuweza kubaini mbegu za ngombe jike pekee kwa ajili ya uhimilishaji ila njia hii hugharimu fedha nyingi zaidi.”

Alisema ng'ombe wote wanapewa chakula kinachozalishwa shambani hapo kwa kuchanganya mahindi na nyasi zilizohifadhiwa vizuri kwa kutumia teknolojia ya kisasa na mifugo hiyo inapewa chakula mara tatu kwa siku ambapo ratiba hiyo inaweza kubadilika kulingana na msimu. Kwenye shamba hilo hakuna madume na iwapo ikitokea ng'ombe amezaa ndama dume, ndama hao huuzwa.

Aliongeza kuwa ng'ombe wao wamevalishwa hereni ikiwa ni utambulisho rasmi unaohusisha aina, uzao, asili, utambuzi wa mmiliki na kuwezesha ufuatiliaji wa maendeleo yake ikiwemo kutambua magonjwa, uwezo wa kutoa maziwa pamoja na kujua kama anakula vizuri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news