Waziri Mkuu awataka Watanzania watumie vizuri fursa za uwekezaji

*Awataka watoe ushirikiano kwa wawekezaji wanaoonesha nia ya kuwekeza nchini

ROME-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania walioshiriki katika Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia wahakikishe wanatumia vizuri fursa walizozipata kutoka kwenye jukwaa hilo, ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na wafanyabiashara walioonesha nia ya kuja kuwekeza nchini.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Watanzania walioshiriki katika Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia, Milan Oktoba 20,2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeondoa tozo na urasimu uliokuwepo awali kwa lengo la kurahisisha shughuli za biashara na uwekezaji nchini.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi wahakikishe Taifa linanufaika kwa kuwa mabalozi wazuri wa kutangaza vivutio vya uwekezaji pamoja na kuwashawishi wawekezaji kutoka katika nchi wanazoishi waje kuwekeza Tanzania.

Ameyasema hayo Oktoba 20, 2023 katika hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa kushirikiana na Benki ya NMB kwa lengo la kuwatambua wafadhili na washiriki wa Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia.

Waziri Mkuu ambaye yuko Italia akimuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023, Rome nchini Italia, aliwasisitiza Watanzania waheshimu sheria za nchi husika.

Mheshimiwa Majaliwa alisema kupitia jukwaa hilo wafanyabiashara na wawekezaji wengi kutoka nchini Italia wameonesha nia ya kuja Tanzania kwa ajili ya kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo, hivyo amewataka viongozi na watendaji wa wizara zinazohusika na masuala ya uwekezaji kuchangamkia fursa hiyo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wafugaji nchini wakubali kubadilika na wafuge kwa kutumia teknolijia ya kisasa ili waweze kujinufaisha zaidi na shughuli hiyo. “Tubadilike tupate manufaa zaidi, ufugaji ni uchumi, ufugaji ni maisha na ufugaji ni kazi, hivyo tubadili mfumo wa ufugaji wetu kwa ajili ya kujiongezea kipato zaidi.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa alisema mamlaka yao imefaidika sana kwa kushiriki katika jukwaa hilo kwa sababu sekta zote walizozitangaza zikiwemo za ujenzi, viwanda zimeonesha kufurahiwa na wadau wa uwekezaji, hivyo wamejipanga kupokea wafanyabiashara.

Awali, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo amemshukuru Mheshimiwa Majaliwa kwa kushiriki katika jukwaa hilo na kwamba ofisi hizo za Ubalozi wa Tanzania nchini Italia zitatoa ushirikiano kwa wafanyabiashara na wawekezaji wote waliokuwa tayari kuja kuwekeza na kufanya biashara nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news