Waziri Mkuu: FAO imeahidi kuunga mkono jitihada za Serikali katika kilimo

ROME-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) limeahidi kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo.

Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zina mipango ya kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula ndani ya nchi na ziada kuuza nje ifikapo 2030.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jioni ya Oktoba 16, 2023 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023, ambapo kauli hiyo ametoa wakati akihutubia mkutano huo kwa niaba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Kabla ya ufunguzi wa mkutano huo uliowahusisha Wakuu wa nchi na Serikali, Waziri Mkuu alishiriki katika Maadhimisho ya miaka 78 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).

“Pamoja na jitihada ambazo tumeziweka ndani za kushirikisha vijana na wanawake kuhakikisha kwamba tunaongeza teknolojia, kutumia mbolea kwenye kilimo, pamoja na ushirikishaji wa sekta binafsi, tumeamua kuungana na FAO kupitia Mkurugenzi Mkuu na wameahidi kutuunga mkono kwenye Sekta ya kilimo,” amesema

Amesema Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara na nishati vijijini ili kurahisisha shughuli za kilimo.

“Maboresho mengine ni ujenzi wa viwanda vya kuzalisha pembejeo za kilimo na kuhamasisha wakulima kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji,” amesema Waziri Mkuu

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dk. Qu Dongyu amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kuendeleza sekta ya kilimo na uchumi wa buluu, hivyo Shirika lao liko tayari kushirikiana na Tanzania katika kutoa msaada wa kitaalam pamoja na kukuza mifumo ya uzalishaji wa chakula.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news