NA GODFREY NNKO
SERIKALI imewataka wananchi kuhakikisha kabla ya kufanya maamuzi ya kukopa au kuweka akiba katika kikundi chochote ndani ya jamii wajiridhishe kwanza na usajili wake.
Vile vile kujiridhisha na mifumo ya fedha ili kuepuka changamoto mbalimbali ambazo wanaweza kukumbana nazo huko mbeleni.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 23, 2023 mkoani Morogoro na Kamishna Msaidizi, Idara ya Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bi.Dionicia Mdeme katika kongamano la siku mbili kwa wamiliki wa mitandao ya kijamii lililoandaliwa na wizara hiyo.
Bi. Mdeme alikuwa akiwasilisha taarifa kuhusu Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha nchini. “Inabidi uifahamu kwa kina hii mifumo ya fedha ili ujue kama inakufaidisha au inakunyonya.”
Amesema, vikundi vyote iwe kazini au mitaani vinapaswa kusajiliwa kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha usalama wa fedha za wanachama hao.
Bi.Mdeme amesema, hilo linatakiwa kuzingatiwa kwa kuwa ni kwa mujibu wa Kanuni na Sheria Ndogo za Fedha (Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo) za Mwaka 2019.
Pia, kanuni na Sheria Ndogo za Fedha (Vikundi vya Kijamii vya Huduma Ndogo za Fedha) za Mwaka 2019 ambavyo vinajumuisha vikundi vya VISLA,Mary Go Round, Kijumbe, VIKOBA na vinginevyo.
Sambamba na Kanuni za Kuwalinda Watumiaji wa Huduma za Fedha za Mwaka 2019. “Watu wote wanaofanya VIKOBA, wanapaswa kusajiliwa kwa mujibu wa sheria. Kwa sababu sheria imeweka adhabu, na imeweka masharti. Vikundi vyote visajiliwe, visiposajiliwa mtu akitapeliwa inakuwa ni cheusi na chekundu.
“Kwa hiyo, hakikisheni vikundi vyenu vya kuhifadhi fedha vimesajiliwa kwa kuwa kutofanya hivyo ni kujiweka hatarini kupoteza fedha katika mazingira ya kutapeliwa,”amesema Bi.Mdeme.
Mbali na hayo,Bi.Mdeme amesema, upatikanaji na utumiaji wa bidhaa na huduma rasmi za fedha mwaka 2023 uliongezeka hadi kufikia asilimia 89 na 76 mtawalia.
Amesema, hii ni kulinganisha na upatikanaji wa bidhaa na huduma za fedha kwa asilimia 86 na 65 mtawalia kwa mwaka 2017.
Bi.Mdeme amesema, ongezeko la upatikanaji wa vituo vya utoaji wa huduma za fedha na watumiaji wa huduma rasmi za fedha umechangiwa na mambo mbalimbali ikiwemo sera na sheria wezeshi katika Sekta ya Fedha.
Vile vile, matumizi ya mifumo ya kidigitali katika utoaji wa huduma za fedha, kuongezeka kwa uelewa wa masuala ya elimu fedha kwa watumiaji wa huduma za fedha.
Sambamba na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi katika kutatua changamoto za sekta ya fedha nchini.
Amesisitiza kuwa, Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha ndani ya Wizara ya Fedha ni muhimili muhimu ambao unaangalia kuhusu mzunguko wa fedha kuanzia kwa wananchi hadi katika uchumi wa nchi.
“Idara ya Sekta ya Fedha, ndiyo inayoangalia namna ambavyo fedha zinatoka katika uchumi wa nchi, hii ni kama damu katika mwili wa binadamu. Hii ndiyo inafanya uchumi wa nchi kuendelea na kukuwa.
“Maendeleio ya nchi yoyote ile duniani yanategemea mfumo imara wa fedha.Tunaangalia riba, mfumuko wa bei na hela ilivyo katika ukwasi.”
Bi.Mdeme amesema, sheria imegawa sekta hiyo katika maeneo makuu manne ikiwemo watoa huduma za fedha wanaopokea amana, watoa huduma za fedha wasiopokea amana.
Wengine ni vyama vya ushirika vya akiba na mikopo, na vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha nchini.
Muundo
Afisa Tawala wa Idara ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Brighton Ngowo amesema, wizara hiyo inasimamia taasisi 29 na mabaraza mawili.
Ameyabainisha hayo wakati akiwasilisha wasilisho kuhusu muundo wa wizara hiyo. “Ili iitwe taasisi lazima kwanza iwe imeundwa kisheria, na lazima iwe na muundo.”
“Hayo mabaraza mawili maana yake yameundwa kisheria, lakini hayana muundo. Taasisi lazima iwe na muundo,lakini baraza halina muundo, linapotokea jambo ndipo wanapokutana.”
Amesema, taasisi ambazo zinasimamiwa na wizara hiyo zimegawanyika katika makundi mbalimbali.
Miongoni mwa taasisi hizo ni zile za fedha na dhamana ambazo zinajumuisha benki ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mifuko ya uwekezaji kama UTT Amis na nyinginezo.
Pia,amesema kuna taasisi za kikodi ambazo zinajumuisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) na Baraza la Rufani za Kikodi (TRAT).
Nyingine ni taasisi za ununuzi wa umma ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na nyinginezo.
Aidha, kuna taasisi za takwimu na bidhaa ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).
Vile vile, wizara inasimamia vyuo ikiwemo Bodi ya Wataalamu wa Ugavi na Ununuzi Tanzania (PSPTB), Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),
Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Taasisi ya Uhasibu Arusha (AII) na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) na taasisi nyinginezo ikiwemo FIU.
Wito
Awali wanahabari wa mitandao ya kijamii nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu kutoa elimu kwa Watanzania ili kuwa wazalendo katika kulipa kodi.
Sambamba na kila anayefanya manunuzi ya bidhaa kuhakikisha kuwa, anadai risiti halali ili kuiwezesha Serikali kupata mapato yatakayoiwezesha kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.
“Lakini pia watu wajue umuhimu kwamba kuna masuala mengi ambayo yanatakiwa yafanyike, ninazungumzia suala la kodi kwa mfano,mitandao ya kijamii ina nafasi kubwa sana ya kuhamasisha watu kulipa kodi.
“Lakini, kuongeza ile base ya walipa kodi, sasa hivi tunawalipa kodi wachache, kupitia misukumo yenu, mitazamo yenu, makala zenu, maoni yenu kwenda kuwauliza wadau kwamba kodi zina umuhimu gani, tunaamini kwamba ile base ya walipa kodi itaongezeka;
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Wizara ya Fedha, Benny Mwaipaja ameyasema hayo wakati akifungua kongamano hilo la siku mbili kati ya Wizara ya Fedha na baadhi ya wamiliki wa mitandao ya kijamii nchini.
“Si hivyo tu, lakini pia tunataka watu zama hizi watu wawe wanadai risiti wanapofanya manunuzi yoyote na risiti zenyewe ziwe ni zile zenye thamani halisi ya hela uliotoa.
“Kwa mfano siku hizi watu wanaenda madukani, wanaulizwa unataka na risiti au hautaki na risiti, ikiwa risiti unambiwa Bwana nitakuuzia shilingi laki mbili, lakini bila risiti nitakuuzia laki moja na nusu.
“Kumbe ile simu bei yake ni laki na ishirini, au laki na nusu na hela nyingine ambayo ingesaidia maendeleo ya kwako wewe, kununulia dawa hospitalini, unamwachia mwenye duka.
“Kwa sababu mtu kakwambia ikiwa na VAT kiasi hiki, isipokuwa na VAT ni kiasi hiki, kwa hiyo maana yake tunaikosesha Serikali mapato yake ambayo yangetumika kuhudumia jamii, kutuhudumia sisi sote, kwa hiyo ninawasihi mtusaidie katika kampeni ya kuhamasisha wananchi kwanza walipe kodi, lakini pia wanapokwenda kununua kitu wadai risiti halali ya hela waliyotoa na wasikubali kwamba kuna risiti kiasi hiki, bila risiti kiasi hiki,”amefafanua Mwaipaja.
Amesema, mitandao ya kijamii imekuwa na mchango mkubwa katika kuharabarisha umma kuhusu miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na Serikali, hivyo wanapaswa kutoa taarifa sahihi ili umma ufahamu yanayofanyika.
“Na sisi (Wizara ya Fedha) tumeazimia kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuwafikia watu wengi zaidi.”
Amesema kuwa, kupitia vyombo hivyo vya habari vya mitandaoni vimekuwa vinatoa taarifa kwa haraka na kwa kasi.
Mwaipaja amefafanua kuwa, Serikali imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na inaendelea ikiwemo ya kimkakati mijini na vijijini ambayo inapaswa kufahamika kwa jamii.
“Yapo mambo mengi ambayo Serikali inayafanya ambayo yanahitaji ninyi myaeleze, vivyo hivyo kuna mambo ambayo Serikali bado haijayafanya ambayo yanahitaji msukumo wenu kwa ajili ya kuyaeleza ili na sisi tuendelee kutafuta rasimali fedha kwa ajili ya kuyatekeleza.”
Aidha, amesema wanatarajia kukutana na wadau wengine wa mitandao ya kijamii kadri muda na rasilimali fedha zitakavyokaa vizuri.
Mbali na hayo,Mwaipaja amewatoa hofu watanzania kuhusu deni la Taifa, na kuwataka kutambua kuwa ni himilivu, linalipika na ndio maana Serikali inaendelea kuaminika na inakopesheka kwa manufaa ya Taifa.
"Ukiona mtu anakopeshwa ujue ameaminika na ndio maana mpaka kuna baadhi ya tasisi za nje ya nchi zinaomba zitukopeshe ama zifadhili miradi yetu, kwa hilo tu jamii iamini kuwa nchi ipo salama na deni la taifa bado ni himilivu linalipika.
"Na wananchi wanapaswa kutambua kuwa mikopo ni njia moja wapo ya maendeleo na mikopo mingi tunayoichukua kwa wadau wa maendeleo mingine inakua na muda wa msamaha kabla ya kuanza kurejesha mpaka muda wa miaka 30.Hivyo, inasaidia kuongeza ufanisi kwenye shughuli za kimaendeleo na kijamii,"amefafanua Mwaipaja.