DAR ES SALAAM-Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) amemuaga Balozi wa Australia nchini mwenye makazi yake nchini Kenya, Mhe. Luke Williams baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi.

Waziri Mbarouk ameongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Australia ni jambo lililochochewa na kazi nzuri iliyofanywa na Balozi Williams wakati akitekeleza majukumu yake ya kibalozi.

"Kazi yako imechochea uboreshaji wa sekta za elimu, utalii, madini, nishati, uchumi wa buluu na kuchangia ukuaji wa sekta ya biashara uwekezaji katika nchi zetu, ni matumaini yangu kuwa utaendelea kuwa Balozi mwema kwa Tanzania nchini Australia na kokote uendako Duniani,” amesema Balozi Mbarouk.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mbarouk amemueleza Balozi Williams kuwa kwa sasa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kiasi kikubwa na kuwaalika wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Australia kuja kuwekeza kwa wingi nchini.

“Kwa kweli ni ngumu sana kuaga lakini haya ndiyo Maisha ya wanadiplomasia hakuna budi, siku zote nitakumbuka utu na ukarimu wa Watanzania,” amesema Mhe. Williams
