ARUSHA-Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa usimamizi thabiti wa sekta ya fedha nchini pamoja na jitihada inazofanya katika kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma za fedha.
Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo alipotembea banda la BoT kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ambapo alipokelewa na Naibu Gavana, Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Kassim Msemo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (kulia) akikabidhiwa zawadi na Naibu Gavana, Bi. Sauda Kassim Msemo, alipotembelea banda la BoT kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Katikati ni Waziri wa Fedha, Dkt, Mwigulu Nchemba.
Bi. Msemo alisema kuwa katika maadhimisho hayo BoT inatoa elimu kwa umma kuhusu haki zao kutoka kwa taasisi za fedha pamoja na wajibu wa wananchi katika kutumia huduma za fedha.
Katika banda la Benki Kuu wananchi wanapata fursa yakujifunza kuhusu sera za uchumi na fedha; uwekezaji katika dhamana za serikali; usimamizi wa fedha binafsi, akiba, mkopo;namna BoT inawalinda watumiaji wa huduma za fedha; utunzaji sahihi wa noti na utambuzi wa alama za usalama; mifumo ya malipo ya taifa na namna Bodi ya Bima ya Amana inavyokinga amana za wateja wa benki na taasisi za fedha.