DCEA yakamata kilo 423.54 za Skanka,ukiwa na taarifa dawa za kulevya piga simu 119 bure

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya kwa kupiga namba ya bure ya 119 ambapo taarifa zitapokelewa kwa usiri mkubwa na kufanyiwa kazi.

Ombi hilo limetolewa leo Novemba 8, 2023 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi ya mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.

Mbali na hayo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema,mamlaka hiyo imekamata kilo 423.54 za bangi iliyosindikwa maarufu kama skanka katika operesheni maalum zilizofanyika kwenye mipaka na fukwe za Bahari ya Hindi.

Amesema, kilogramu 158.54 zilikamatwa eneo la Kigamboni na Kawe jijini Dar es Salaam zikiwa zimehifadhiwa ndani ya mabegi ya nguo tayari kwa kusafirishwa.

Vile vile, amesema kilogramu 265.64 zilikamatwa katika matukio tofauti mikoa ya Nyanda za Juu Kusini zikiwa zimefichwa ndani ya magari kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine ikiwemo maboksi yenye matunda aina ya apples zikisafirishwa kuelekea jijini Dar es salaam.
Kamishna Jenerali huyo amesema, mamlaka imekamata watu wanaojihusisha na utengenezaji wa biskuti kwa kuchanganya na skanka katika eneo la Kawe jijini Dar es salaam.

Katika tukio hilo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, watuhumiwa walikutwa wakiendelea na uzalishaji wa biskuti hizo kwa kutumia mtambo mdogo wa kusaga skanka na vifaa vya kutengeneza biskuti za bangi.

“Vilevile, mamlaka imebaini maeneo yanayotumika kama masoko ya kusambazia na kuuza skanka kwenye fukwe za Bahari ya Hindi.

“Kutokana na operesheni hizo, watu 16 wamekamatwa ambapo kati yao sita (6) wamefikishwa mahakamani na 10 watafikishwa baada ya taratibu za kisheria kukamilika,”amebainisha Kamishna Jenerali Lyimo.

Amesema, Skanka (skunk) ni jina la mtaani linaloitambulisha aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu (TetraHydroCannabinol - THC) ikilinganishwa na bangi ya kawaida.

“Dawa hii ya kulevya hutokana na kilimo cha bangi mseto ambapo asilimia 75 ni bangi aina ya sativa na asilimia 25 ni bangi aina ya indica.

“Kiwango cha sumu kilichopo kwenye skanka ni zaidi ya asilimia 45 ukilinganisha na bangi ya kawaida ambayo kiwango chake cha sumu ni kati ya asilimia 3 mpaka 10.

“Hivyo, skanka ina madhara makubwa zaidi kwa mtumiaji ikiwemo kuamsha na kuzidisha magonjwa ya afya ya akili kwa haraka,”amesema Kamishna Jenerali.

Pia, imebainika kuwa, watu wasiowaaminifu huchanganya skanka kwenye vyakula kama vile biskuti, keki, jamu, sharubati, tomato sauce pia kwenye sigara na shisha.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema, lengo la kufanya hivyo ni kurahisisha uuzwaji wa dawa hizo kwa kificho na kuongeza idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya vyakula hivyo hupendwa na watoto.

“Wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo wanapaswa kuwa makini na vyakula wanavyovitumia na kuacha kufuata mikumbo isiyofaa ikiwemo kutumia vilevi na vitu wasivyovijua hali ambayo inaweza kuwaingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya,”amesisitiza Kamishna Jenerali Lyimo.

Wakati huo huo,Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imesema, inaendelea kufanya operesheni dhidi ya wasafirishaji na wazalishaji wa dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha dawa za kulevya haziendelei kuwepo nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news