Dkt.Mwigulu amshukuru Rais Dkt.Samia,jimboni wasema mitano tena

SINGIDA-Waziri wa Fedha, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuridhia ombi na kuwapatia leseni 28 wachimbaji wadogo wanaofanya shughuli zao katika mgodi wa dhahabu wa Sekenke One uliopo Iramba mkoani Singida.

Leseni hizo 20 ni kwa ajili ya uchimbaji na zingine nane zinahusu shughuli za uchenjuaji madini ya dhahabu, katika eneo la mgodi wa Sekenke One.

Aidha, Dkt. Nchemba aliwaeleza wapiga kura wake kwamba, kwa kipindi cha utawala wa Rais Dkt Samia, jimbo la Iramba magharibi limepiga hatua kubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, huku sekta ya umeme nayo ikifanikiwa kupitia nishati ya umeme vijijini (REA).

"Leo hii hapa Barabara yenu inayotoka Mgela-Mtoa-Shelui mpaka kule Sibiti, inafanyiwa upembuzi yakinifu, Serikali inahitaji kuiboresha kwa kuiwekea lami, ili iungane na ile ya Sibiti," alisema Dk. Nchemba, huku akishangiliwa na umati wa watu kwa kusema 'Mitano tena.

Naye Waziri wa Madini, Mhe Anthony Mavunde, akikabidhi leseni za Wachimbaji hao wadogo, katika Mgodi wa dhahabu wa Sekenke One ulipo kijiji cha nkonkilangi, Kata ya Ntwike, Tarafa ya Shelui, aliwataka wafanye kazi kwa bidii na maarifa, waweze kuinua uchumi wao, Taifa na familia kwa ujumla.

Awali katika mkutano huo, Mkuu wa wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda, amemwambia Mhe Mavunde kuwa wilaya hiyo ina hazina kubwa ya madini ya aina mbalimbali, lakini maeneo husika yanahitaji kufanyiwa utafiti kabla ya kuanza kuchimbwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news