HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA 13 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 10 NOVEMBA, 2023 JIJINI DODOMA.
UTANGULIZI
Shukurani
1. Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na afya njema na kutuwezesha kuhitimisha shughuli zote za Mkutano wa 13 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama zilivyopangwa.
Hivyo basi, tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atupe hekima na nguvu ya kuweza kutekeleza maazimio yote yaliyopitishwa na Bunge lako tukufu.
2. Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suhulu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada za kutekeleza dhamira yake ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.
Sina shaka nyote mtakubaliana nami kuwa uongozi wake makini na busara zake zimeendelea kuchagiza maendeleo ya haraka ya uchumi wa nchi yetu pamoja na ustawi wa Mtanzania mmoja mmoja.
Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya, ninawasihi Watanzania wote tuendelee kumuunga mkono ili aweze kutimiza dhamira yake.
3. Mheshimiwa Spika, naomba pia nitumie fursa hii kumshukuru sana Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais kutelekeza majukumu yake ya kuwatumikia Watanzania.
Ninampongeza sana Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa jitihada anazozifanya, ama kwa hakika busara zake zimekuwa chachu katika kuleta maendeleo ya haraka ya Taifa letu.
4. Mheshimiwa Spika, awali ya yote nitumie fursa hii kukupongeza sana kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani, IPU, katika kikao cha Baraza la Uongozi kilichofanyika tarehe 23 hadi 27 Oktoba huko Luanda, nchini Angola.
Vilevile, ninakupongeza sana kwa kuwa Rais wa Tatu mwanamke kushika nafasi hiyo ambayo imeshawahi kushikwa na Mheshimiwa Najma Heptulla kutoka India (1999–2002) na Mheshimiwa Gabriela Cuevas kutoka Mexico (2017–2020).
Kipekee ninakupongeza sana kwa kuwa Rais wa kwanza Mwanamke kutoka Afrika kuchaguliwa kushika nafasi hiyo kubwa ya Rais wa Mabunge Duniani.
5. Mheshimiwa Spika, nirudie kukupongeza sana kwa ushindi huo ambao kwa hakika umetuletea heshima kubwa sana Watanzania kwani umeithibitishia Dunia nzima kuwa Watanzania tunao uwezo mkubwa wa uongozi na tunaaminika sana.
Nitumie fursa hii kukutakia kila la heri Mheshimiwa Spika katika kutekeleza majukumu yako na niwasihi waheshimiwa wabunge wenzangu na Watanzania wote tuendelee kumwombea heri Mheshimiwa Spika.
6. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kukushukuru na kukupongeza sana kuendelea kuliongoza vema Bunge hili tukufu na kusimamia vema mijadala yote iliyoendeshwa katika Mkutano huu wa 13 tutakaouhitimisha hivi leo.
Mwenye macho haambiwi tazama, hekima, ukomavu na weledi wako umeendelea kuongezeka siku hata siku. Hongera sana Mheshimiwa Spika!
7. Mheshimiwa Spika, nimshukuru pia Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb.), Naibu Spika kwa kazi nzuri anayoifanya ya kukusaidia wewe Mheshimiwa Spika kutekeleza majukumu ya kuliongoza Bunge. Vilevile, niwashukuru Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge ambao ni Mheshimiwa Najma Murtaza Giga (Mb.) na Mheshimiwa Daniel Baran Sillo (Mb.).
8. Mheshimiwa Spika, nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Bahati Ndingo, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo kufuatia uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni.
Ushindi huo wa kishindo ni kielelezo tosha kuwa wananchi wa Jimbo la Mbarali bado wana imani kubwa kwa Serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi.
Vilevile, ninampongeza sana Mheshimiwa Aziza Sleyum Ally kwa kuteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Mapinduzi.
Nitumie fursa hii kukukaribisha sana, na kwa upande wetu, sisi Wabunge tunakuhakikishia kuwa tutakupa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yako ya kuwatumikia wananchi.
9. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitowashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kazi kubwa mliyoifanya.
Mmeshiriki kikamilifu kutoka kamati, mijadala ambako hoja mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa Mkutano huu.
Michango yenu ni muhimu sana katika kuimarisha ustawi na huduma kwa Watanzania. Hivyo basi, niwahikishie kuwa Serikali imepokea michango yote, maoni pamoja na ushauri wenu ambao kimsingi umekuwa ukisaidia sana katika kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya Serikali.
Salamu za Pole
10. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Septemba hadi Novemba 2023, wapo Watanzania wenzetu waliopatwa na majanga mbalimbali yakiwemo ajali za barabarani, moto na mengine yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali.
Kwa masikitiko makubwa ninatoa salamu nyingi za pole kwa wahanga wote wa majanga hayo. Aidha, ninatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao kutokana na masahibu hayo.
Kwa wale majeruhi tuzidi kuwaombea uponyaji wa haraka na kwa marehemu tuwaombee kwa Mwenyezi Mungu ili azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina!
SHUGHULI ZA BUNGE
11. Mheshimiwa Spika, Mkutano huu wa 13 wa Bunge lako tukufu, ulipokea na kujadili taarifa mbalimbali kutoka kwa kamati za Kudumu za Bunge, maswali kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na majibu ya Serikali sambamba na kujadili na kupitisha miswada ya sheria.
Maswali na Majibu
12. Mheshimiwa Spika, kupitia mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliuliza maswali 154 ya msingi na mengine 454 ya nyongeza ambayo yalijibiwa na Serikali.
Halikadhalika, maswali manne ya papo kwa papo yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Waziri Mkuu baada ya kuwa nimetoa taarifa kuhusu Kuidhinishwa kwa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Tolea la 2023 na Mitaala ya Elimu ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu mbele ya Bunge lako tukufu.
Miswada ya Sheria
13. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako tukufu limepokea Miswada nane ya sheria kama ifuatavyo:
Moja: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbakmbali (Na.4) wa Mwaka 2023 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.4) Bill, 2023].
Mbili: Muswada we Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Sekta ya Sheria wa Mwaka 2023 [The Legal Sector Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2023]
Tatu: Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote wa Mwaka 2023.
Nne: Muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma wa Mwaka 2023.
Tano: Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023.
Sita: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (5) wa Mwaka 2023(The Written Laws Miscellaneous Amendments) (No.5) Bill, 2023.
Saba: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023 (The Political Affairs Laws (Ammendment) Bill, 2023.
Nane: Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Mwaka 2023.
Maazimio ya Bunge
14. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 61 na 107 hadi 112 za Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Februari 2023, na kwa kuzingatia wajibu wa Bunge katika kuisimamia na kuishauri Serikali, Bunge lako tukufu lilipokea, kujadili na kupitisha Maazimio mawili kama ifuatavyo:
Moja: Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Taasisi ya Dawa ya Afrika la Mwaka 2023 (Treaty for Establishment of the African Medicines Agency - AMA).
Mbili: Azimio ta Bunge kuhusu Mapendekezo ya Tanzania Kundhia Kusunga na Mkataba we Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu la Mwaka 2009 (Statute of the Intemational Renewable Energy Agency - IRENA).
15. Mheshimiwa Spika, Maazimio haya yalipokelewa na kujadiliwa na Waheshimiwa Wabunge kwa ustadi wa hali ya juu huku wakionesha nia njema ya kujenga mustakabali mwema wa taifa letu. Kwa dhati niwapongeze Waheshimiwa Wabunge kwa kukubali kuridhia kupitisha maazimio haya.
Taarifa za Serikali Bungeni
16. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 56 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Februari 2023, Bunge lako tukufu katika Mkutano wa 13 lilipokea Taarifa ya Serikali kuhusu Kuidhinishwa kwa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Tolea la 2023 na Mitaala ya Elimu ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu niliyoitoa mbele ya Bunge lako Tukufu siku ya tarehe 3 Novemba 2023.
Taarifa ya Kamati za PAC na LAAC kuhusu hesabu zilizokaguliwa na CAG kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na Taarifa ya Kamati ya PIC kuhusu Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022
17. Mheshimiwa Spika, Mkutano huu wa 13 wa Bunge lako ulipata nafasi pia ya kupokea na kujadili kwa kina Taarifa za Kamati za Bunge ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 ulioishia tarehe 30 Juni, 2022. Taarifa hizi za Kamati zinazotokana na Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
18. Mheshimiwa Spika, taarifa za Kamati hizi tatu zimechambua kwa kina hoja mbalimbali za ukaguzi zinazohusu matumizi ya fedha za umma kwa hesabu za Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma pamoja na mwenendo wa uwekezaji wa mitaji ya umma uliofanywa na taasisi za umma kwa mwaka wa fedha ulioiishia tarehe 30 Juni, 2022.
Jumla ya maazimio 117 yaliyotokana na hoja 14 yameweza kutolewa na Bunge, ambayo kimsingi ni maelekezo mahsusi kwa Serikali.
19. Mheshimiwa Spika, niruhusu nitoe pongezi za dhati kwa ndugu Charles E. Kichere, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa kuendelea kuwa taasisi yenye kuaminika inayotoa Huduma za Ukaguzi kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Nyote ni mashahidi kwamba, ofisi hii imendelea kujipambanua kwa namna inavyojenga, inavyokuza na kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji katika kusimamia na kudhibiti ipasavyo ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali kama inavyoidhinishwa na Bunge katika Wizara na Taasisi za Serikali, Mikoa na Halmashauri.
Vilevile, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imeweza kuwahikikishia Watanzania na jamii yote namna ambavyo nchi yetu inavyoweza kupata faida au tija kutokana na matumizi bora ya fedha za Umma, na namna ambavyo mali za Umma zinahifadhiwa, kutunzwa na kulindwa ipasavyo.
20. Mheshimiwa Spika, niwashukuru Maafisa Masuuli pamoja na Watendaji wote wa Serikali kwa namna ambavyo wameweza siyo tu kujibu hoja za Ukaguzi ambazo zilibainishwa katika Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, lakini pia kuweza kutekeleza takwa la Kikatiba la kufika mbele ya Kamati husika za Bunge kwa ajili ya ufafanuzi wa kina.
Aidha, nitoe shukrani zangu kwa Waheshimiwa Mawaziri kwa michango yao katika kutoa majibu ya Serikali kwa baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge.
Ni ukweli ulio bayana kwamba hoja zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge ni nyingi, muhimu na zote zinahitaji majibu na utekelezaji wa haraka. Niseme tu kuwa Serikali yenu ni sikivu na itatekeleza mapendekezo hayo kwa kutoa majibu sahihi na utekelezaji wa haraka.
21. Mheshimiwa Spika, hivyo basi, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge pamoja na majibu yaliyotolewa na Serikali, mturuhusu tufanyie kazi masuala yote yanayohitaji mabadiliko ya kisera na kisheria.
Na mabadiliko haya yote tutalishirikisha kikamilifu Bunge hili ili kutimiza ndoto na malengo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu.
22. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Serikali baada ya kupokea hoja na maazimio yote, tayari imeandaa Bangokitita ambalo linaainisha jukumu la kila Wizara kwa ajili ya kufanyia kazi maelekezo ya Bunge ili kurahisisha uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji kwa waheshimiwa wabunge rejea yao.
Hivyo basi, ninaziagiza Wizara husika ziandae kwa wakati taarifa za utekelezaji wa Maazimio yote kulingana na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati. Ofisi ya Waziri Mkuu kwa upande wake, itaandaa taarifa ya Serikali ambayo itawasilishwa kwa Mheshimiwa Spika.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
23. Mheshimiwa Spika, pamoja na hoja za Kamati za Bunge zilizopokelewa na kujadiliwa na Waheshimiwa Wabunge, Serikali iliwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 ambapo Waheshimiwa Wabunge wameweza kuchangia hoja hii moja kwa moja na kwa maandishi.
Ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao katika Mpango huu pamoja na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2024/2025.
24. Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba Mipango ya Maendeleo ya kila mwaka ni nyenzo muhimu ya matumizi bora ya rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Mipango hii huhakikisha malengo ya Dira 2025 yanafuatiliwa na kusimamiwa kila mwaka ili kuweza kukuza uchumi na kuondoa umaskini nchini.
Mapendekezo ya Mpango yameainisha maeneo mahsusi ya kipaumbele yatakayozingatiwa katika maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa kuzingatia rasilimali zilizopo.
25. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla katika mwaka 2024/2025 msisitizo utawekwa katika kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi; kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na maendeleo.
Vilevile, msisitizo utawekwa katika kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika maandalizi na utekelezaji wa mipango, uwekezaji na uzalishaji nchini.
26. Mheshimiwa Spika, Serikali pia imewasilisha Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2024/2025.
Mwongozo huu kimsingi ni maelekezo ya jumla na maelekezo mahsusi yanayopaswa kuzingatiwa na Maafisa Masuuli katika hatua zote za uandaaji, uwasilishaji, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini pamoja na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/2025.
27. Mheshimiwa Spika, Mwongozo huu umejikita katika kuhakikisha Serikali inatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambavyo ni pamoja na: kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.
28. Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao kwenye hoja hizi mbili ambazo kwa pamoja zinatoa mwelekeo wa wapi nchi yetu inataka kufika kwa kuangalia kule tulipotoka.
Hivyo, nitoe rai kwa Maafisa Masuuli na watendaji wote wa Serikali kutafsiri kwa vitendo na kwa umakini mkubwa maelekezo yote yaliyotolewa na Bunge hili ikiwa ni sehemu ya kutimiza ndoto za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MASUALA YA UTABIRI WA HALI YA HEWA
29. Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kuwa, mvua zimeanza kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Na tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeshatoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2023.
Utabiri huo, umebainisha uwepo wa hali ya El Nino ambayo itaambatana na mvua kubwa na kusababisha mafuriko ambayo yanaweza kuleta athari mbalimbali zikiwemo; madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii, upotevu wa mali na uharibifu wa miundombinu.
30. Mheshimiwa Spika, taarifa ya utabiri wa hali ya hewa inaonesha mvua hizo zitakuwa juu ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Shinyanga, kusini mwa Mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia) na kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro.
31. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kuzuia na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na uwepo wa El Nino sambamba na kujiandaa kukabiliana na mvua hizo kubwa.
Kwa msingi huo, nitumie fursa hii kuzielekeza Wizara, Mikoa na Taasisi za Serikali kuzingatia masuala yafuatayo:
Moja: Kuainisha na kuandaa rasilimali za kujiandaa, kuzuia na kukabiliana na maafa endapo yatatokea;
Mbili: Kuelimisha na kuhimiza wananchi kuhama kwenye maeneo hatarishi na kuchukua tahadhari ili kuokoa maisha na mali;
Tatu: Idara na Taasisi zinazohusika na mazingira na miundombinu zihakikishe barabara zinapitika wakati wote, mitaro na makalvati yanaimarishwa na kusafishwa ili kuruhu maji yapite;
Nne: Sekta za maji, umeme na mawasiliano ziweke mipango ya kuzuia madhara na kuhakikisha uharibifu katika huduma hizo unapewa ufumbuzi mapema;
Tano: Kushirikisha wadau wa maafa ikiwemo wananchi, taasisi za umma na sekta binafsi katika mipango yote ya usimamizi wa maafa;
Sita: Kutoa taarifa haraka kwa mamlaka husika inapotokea maafa katika sekta husika;
Saba: Kamati za Maafa katika ngazi ya Kijiji, Wilaya, Mkoa na Taifa zijipange kikamilifu kukabiliana na changamoto za El Nino endapo zitajitokeza;
Nane: Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na Halmashauri ziandae mipango ya utekelezaji katika maeneo yao kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El Nino.
32. Mheshimiwa Spika, niwasihi wananchi wote kujenga utamaduni wa kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kutekeleza maelekezo yanayotolewa na Viongozi na Mamlaka ya Hali ya Hewa ikiwemo kuhama kwenye maeneo hatarishi na kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo salama.
Kwa upande mwingine, wananchi waendelee kuweka akiba ya chakula na kutumia mvua hizo nyingi kulima mazao yanayostawi katika mazingira ya maji mengi.
HALI YA UKUSANYAJI WA MAPATO
33. Mheshimiwa Spika, uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita ikiwemo kuwezesha uwekezaji wa kimkakati katika sekta za uzalishaji, huduma za jamii na miundombinu.
Ukuaji huo wa uchumi umechangia kuongezeka kwa uzalishaji katika sekta rasmi na isiyo rasmi na hivyo, kuiwezesha Serikali kukusanya mapato zaidi.
34. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2023/2024, mapato kutoka vyanzo vyote vya ndani na nje yalifikia shilingi trilioni 9.06, sawa na asilimia 89.6 ya lengo la kipindi hicho.
Kati ya kiasi hicho, mapato ya ndani yalikuwa shilingi trilioni 6.94 sawa na asilimia 96.2 ya lengo la kipindi hicho. Mapato ya ndani yanajumuisha shilingi trilioni 6.15 zilizokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania; shilingi bilioni 491 za mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Wizara, Idara zinazojitegemea na Taasisi; na shilingi bilioni 299 kutoka vyanzo vya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
35. Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa mapato kunatokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, ikiwemo kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kurahisisha ulipaji wa kodi.
Katika hatua nyingine, kuimarika kwa mapato kumewezesha Serikali kuendelea kuwahudumia wananchi kupitia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa hospitali na vituo vya afya.
36. Mheshimiwa Spika, vilevile, mapato hayo yamewezesha ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa; Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere; uboreshaji wa miundombinu ya barabara na reli; mpango wa Elimumsingi na Sekondari bila ada; kuboresha Shirika la Ndege la Tanzania; usambazaji umeme vijijini na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
37. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha kuwa malengo ya makusanyo na utekelezaji wa bajeti kwa ujumla yanafikiwa.
Mikakati hiyo ni pamoja na: kuimarisha mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa mapato; kuimarisha doria maeneo ya mipakani; kutoa elimu kwa walipa kodi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari; kuhimiza matumizi ya stakabadhi za kielektroniki za EFD na kuendelea kuboresha mazingira ya kuvutia uwekezaji na biashara.
38. Mheshimiwa Spika, vilevile, mikakati hiyo inalenga kuhakikisha taasisi zenye sura za utoaji wa huduma kwa pamoja zinaboresha mifumo ya ukusanyaji kwa kuwezesha kutoa namba ya malipo jumuishi ili kurahisisha ulipaji kodi, ada na tozo mbalimbali kwa wateja na hivyo kuongeza uhiari wa ulipaji kodi; na kuendelea kusimamia na kutekeleza kikamilifu sera za bajeti na fedha.
39. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuzielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani ili kuondoa mianya ya uvujaji wa mapato.
Aidha, Mamlaka hizo ziimarishe ushirikiano na Taasisi nyingine za umma kwenye ukusanyaji wa mapato ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania.
40. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee niwashukuru wananchi kwa kushirikiana na Serikali katika ukusanyaji wa mapato ambayo ndiyo msingi wa maendeleo yetu.
Vilevile, niwapongeze kwa dhati watumishi wa taasisi zenye dhamana na ukusanyaji wa mapato zikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kufanikisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Aidha, niwasihi watumishi wote waliopewa dhamana hiyo kutekeleza jukumu hilo kwa uadilifu na kuendelea kutoa elimu ya mlipakodi ili kufanikisha ulipaji wa kodi kwa hiyari
USIMAMIZI WA ELIMUMSINGI
41. Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kuwa mojawapo ya malengo ya elimu nchini Tanzania ni kutoa elimu bora itakayowajengea uwezo wahitimu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. Hatua hiyo itawezesha Taifa letu kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
42. Mheshimiwa Spika, Serikali katika kutekeleza azma hiyo, imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kuboresha miundombinu; kutekeleza mpango wa elimumsingi na kidato cha tano na sita bila ada; kuongeza ajira za walimu na wakufunzi wenye sifa; kutoa ufadhili na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na maboresho ya sera na mitaala.
43. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia uandikishaji wa wanafunzi kuanzia ngazi ya elimu ya awali bila kusahau watoto wenye mahitaji maalum ambapo zoezi ambalo huanza mwezi Oktoba kila mwaka.
Kwa mwaka 2024, Serikali inatarajia kuandikisha Watoto wa Elimu ya Awali 1,877,484 wenye rika lengwa wakiwemo wavulana 934,560 na wasichana 942,924 na Darasa la Kwanza 1,729,180 wakiwemo wavulana 860,870 na wasichana 868,310.
44. Mheshimiwa Spika, hadi sasa jumla ya watoto wa elimu ya awali 407,138 sawa na asilimia 21.7 wakiwemo wavulana 201,244 na wasichana 206,253 wameandikishwa.
Kati ya watoto wa elimu ya awali walioandikishwa watoto wenye mahitaji maalum ni 960 kati yao wavulana ni 488 na wasichana ni 472.
45. Mheshimiwa Spika, watoto wanaotarajia kujiunga darasa la kwanza walioandikishwa ni 593,452 sawa na asilimia 34.3 wakiwemo wavulana 293,728 na wasichana 299,724.
Kati ya wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa wenye mahitaji maalum ni 1,365 wakiwemo wavulana ni 733 na wasichana 632.
46. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwaelekeza Wakuu wa Mikoa yote nchini kusimamia zoezi la uandikishaji katika maeneo yao ambalo itakuwa vema likihitimishwa tarehe 31 Desemba 2023.
Nitumie fursa hii pia kuwakumbusha wazazi/walezi wote wenye Watoto wenye rika lengwa kuwaandikisha Watoto hao ili waweze kuanza masomo ifikapo Januari, 2024.
47. Mheshimiwa Spika, ninatoa wito kwa wadau wote wa maendeleo zikiwemo Taasisi za Kidini na Taasisi za Kiraia kushiriki katika kutoa hamasa kwa Watanzania nchi nzima ili watoto wote wenye rika lengwa waweze kuanza masomo mwezi Januari.
48. Mheshimiwa Spika, jitihada hizo zinaenda sambamba na kukamilisha maandalizi yote muhimu ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2024 ikiwemo ujenzi wa miundombinu.
Jumla ya wanafunzi 1,206,995 sawa na asilimia 86.4 ya wanafunzi 1,397,370 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kuhitimu Elimu ya Msingi mwaka 2023 wanatarajiwa kujiunga na Elimu ya Sekondari Januari, 2024.
49. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwakumbusha Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wote nchini wahakikishe kuwa ujenzi wa miundombinu yote katika Shule za Sekondari unakamilika kabla ya tarehe 30 Novemba 2023.
Serikali itachukua hatua kali kwa wote watakaoshindwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika Shule za Sekondari.
Wakuu wa Mikoa fanyeni ufuatiliaji, Serikali imeshapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi katika Halmashauri zote nchini hivyo hakuna sababu wala visingizio vya kutokamilisha ujenzi kwa wakati.
MIKOPO YA ELIMU YA JUU
50. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya kati na ya juu kwa kuwezesha vijana wa Kitanzania kupata mikopo ya wanafunzi. \
Katika mwaka wa masomo 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni 786 kwa ajili ya mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati.
51. Mheshimiwa Spika, kati ya fedha hizo shilingi bilioni 731.3 zitatolewa kama mikopo kwa wanafunzi 220,376 wa shahada mbalimbali; shilingi bilioni 6.7 kwa wanafunzi 1,200 wanaofadhiliwa kwa mpango wa Samia Scholarship; na shilingi bilioni 48 kwa wanafunzi wa stashahada zenye uhitaji mkubwa wa rasilimaliwatu nchini.
52. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuongeza wigo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi ambapo katika mwaka wa masomo 2023/2024 utoaji wa mikopo umehusisha wanafunzi wa stashahada. Dirisha la kupokea maombi ya mkopo kwa wanafunzi wa stashahada lilifunguliwa tarehe 7 Oktoba 2023 na kufungwa tarehe 29 Oktoba 2023. Hadi dirisha linafungwa jumla ya waombaji 12,910 walikuwa wamewasilisha maombi.
53. Mheshimiwa Spika, kwa upande shahada hadi tarehe 5 Novemba 2023 jumla ya wanafunzi 169,180 sawa na asilimia 77 ya lengo walikuwa wamepangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 555.8.
Kati yao, wanafunzi 73,078 ni wapya wa shahada za kwanza na wengine 96,102 ni wanufaika wanaoendelea na masomo ambao matokeo yao ya ufaulu wa mitihani na kuendelea na masomo yamepokelewa na Bodi ya Mikopo.
54. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi ya Teknolojia kusimamia kikamilifu zoezi la utoaji wa mikopo na kuhakikisha kuwa zoezi hilo linakamilika kwa wakati sambamba na kushughulikia kwa wakati changamoto za utoaji wa mikopo kwa wanafunzi pale zinapojitokeza.
55. Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kutoa fedha nyingi kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupata elimu ya juu, bado kuna baadhi ya waajiri na wanufaika wa mikopo ambao hawatimizi wajibu wao wa kurejesha fedha waliokopeshwa ili mfuko uweze kusomesha vijana wengi zaidi.
Hivyo basi, nitoe wito kwa waajiri na wanufaika wadaiwa wote kutimiza wajibu wao wa kisheria wa kurejesha mikopo hiyo kwa hiyari.
KUIMARISHA MAZINGIRA YA BIASHARA
56. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuimarisha na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Sote tumeshuhudia mabadiliko ndani ya Serikali yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais, kwa kuanzisha Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ili kuimarisha uratibu na kuongeza imani zaidi kwa wawekezaji.
57. Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuimarisha uwekezaji nchini ninaomba nitumie fursa hii kusisitiza masuala yafuatayo:
Moja: Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kupitia Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, NIDA, BRELA, TRA, Idara ya Kazi, Idara ya Uhamiaji, NEMC, TANESCO, TBS, OSHA na TMDA, iboreshe mwongozo wa uwekezaji ili kubainisha fursa kulingana na mazingira ya sasa na kuzingatia taratibu za kuwatambua na kuwasajili wanaotaka kuwekeza nchini;
Mbili: Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) kiimarishe matumizi ya TEHAMA ili kutangaza fursa nyingi za uwekezaji zilizopo nchini na kuwawezesha wawekezaji kutumia TIC kama kiungo cha kupata taarifa muhimu kutoka kwenye taasisi za Serikali nchini; na
Tatu: TIC ihakikishe kuwa mwongozo wa uwekezaji unapatikana kwa urahisi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
MASUALA YA MAENDELEO YA VIJANA
58. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuratibu shughuli za Maendeleo ya vijana sambamba na kuandaa mfumo wa kitaifa wa uratibu wa afua zinazotekelezwa na Wadau mbalimbali.
Mfumo huo utasaidia upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati na kuwawezesha vijana kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi.
59. Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kupitia Programu ya Ukuzaji Ujuzi imetoa mafunzo kwa vijana 121,898.
Katika kipindi cha 2017 hadi 2023 vijana 91,106 wamepata ujuzi kwa njia ya uanagenzi. Vilevile, vijana 22,296 wamerasimishiwa ujuzi uliopatikana katika mfumo usio rasmi.
Licha ya hayo, vijana 6,300 wamepata mafunzo ya uzoefu kazini na vijana 2,196 waliokuwa kazini wameongezewa ujuzi. Pia, kupitia Mpango wa Jenga Kesho iliyobora vijana 812 wamedahiliwa na wanashiriki mafunzo ya Kilimo Biashara.
60. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana imetoa mikopo ya shilingi bilioni 1.88 kwa miradi 85 yenye vijana 595.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imeendelea kutoa mikopo ambapo hadi kufikia Oktoba 2023 shilingi bilioni 1.27 zimetolewa kwa miradi 56 yenye vijana 392.
BARAZA LA TAIFA LA BIASHARA
61. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa Sekta Binafsi, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi na kutengeneza fursa ya majadiliano kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma kupitia Baraza la Taifa la Biashara.
Baraza hilo huandaa vikao vya majadiliano rasmi kufikia muafaka kati ya sekta hizo kuhusu maboresho ya mazingira ya biashara, uwekezaji na uchumi kwa ujumla.
62. Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada hizo baraza limeongeza ushiriki wa Sekta Binafsi kupitia mfumo rasmi na jumuishi wa majadiliano katika ngazi zote za utawala. Vilevile, Baraza limewezesha Mikoa 11 kuratibu na kufanya mikutano ya Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya.
63. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa maazimio ya Baraza umewezesha kufanya mapitio sera, sheria, kanuni, taratibu na mifumo mbalimbali; kuunganisha majukumu ya taasisi yanayoingiliana; kuimarisha vituo vya huduma za mahali pamoja; kuanzisha na kuunganisha mifumo ya TEHAMA na kuimarisha na kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za kiuchumi hususan miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali.
MKAKATI WA KUENDELEZA WANANCHI KIUCHUMI
64. Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada zilizochukuliwa na Serikali katika kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, ikiwa ni sehemu ya uwezeshaji kwa wananchi wetu, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuwaendeleza wananchi kiuchumi.
65. Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ambalo limeanzishwa chini ya Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Na. 16 ya mwaka 2004. Sambamba na kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004, limepewa dhamana ya kuratibu, kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi ambazo ni mtambuka na zenye kuhusisha wadau wa sekta mbalimbali za kiuchumi.
66. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Septemba, 2023, mifuko na programu za uwezeshaji ilifanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 743.7 kwa wanufaika wapatao 6,064,957 ambapo wanawake ni asilimia 54.
Aidha, kwa mwaka 2022/2023, mifuko na programu za uwezeshaji ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 743.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni 713.8 zilizotolewa mwaka 2021/2022. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 4.02.
UHUSIANO WA KIDIPLOMASIA
67. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha na kuchochea shughuli za maendeleo nchini, Serikali imeendelea kuimarisha uhusiano wa kikanda na kimataifa kwa lengo kufungua fursa mbalimbali ikiwemo uwekezaji na mitaji katika sekta za utalii na uchukuzi.
Katika hili, nimpongeze kwa dhati Mwanadiplomasia namba moja, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele kuimarisha diplomasia ya uchumi.
68. Mheshimiwa Spika, masuala yanayozingatiwa kwenye diplomasia ya uchumi ni pamoja na kutafuta masoko ya bidhaa zetu, kutafuta fursa za kiuchumi katika sekta mbalimbali, fursa za elimu, mafunzo, utaalamu na ujuzi pamoja na ajira nje ya nchi na kubidhaisha lugha ya Kiswahili.
69. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2022/2023, Serikali iliratibu na kufanikisha kusainiwa kwa mikataba 13 na Hati za Makubaliano 37.
Mikataba na hati hizo zinagusa sekta za kiuchumi na kijamii ikiwemo ulinzi na usalama, kilimo na uvuvi, viwanda, biashara, uwekezaji, TEHAMA na utalii. Nyingine ni afya, elimu, uchukuzi, mawasiliano, utamaduni, sanaa na michezo, sayansi na teknolojia, mazingira na uchumi wa buluu.
70. Mheshimiwa Spika, ziara zinazofanywa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine zimekuwa chachu ya kuimarisha uhusiano wa kimataifa.
Vilevile, ziara hizo zimeibua fursa zenye manufaa ya kiuchumi nchini. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni ongezeko la watalii, ongezeko la wafanyabishara na wawekezaji, miradi mikubwa na ya kati, uwekezaji na kufungua masoko ya bidhaa mbalimbali.
Kipekee, nimpongeze tena Mheshimiwa Rais wetu ambaye kupitia ziara zake na nchi jirani, aliweza kutatua changamoto za kibiashara kwenye mipaka ya Kenya na Zambia.
71. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu na kufanikisha ziara za kikazi na kitaifa za Viongozi Wakuu kutoka mataifa mengine kuja hapa nchini. Baadhi ya viongozi hao walitoka Ujerumani, Indonesia, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Afrika Kusini, Falme za Kiarabu, Uswisi na Marekani.
72. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuratibu ziara za Viongozi Wakuu wa nchi nyingine wanaozuru Tanzania ili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi nyingine. Ziara hizo zitaimarishwa ili nchi yetu iendelee kunufaika na fursa za kiuchumi na kijamii lakini pia iweze kung’ara kikanda na kimataifa.
MAELEKEZO MAHSUSI
73. Mheshimiwa Spika, wakati nikielekea kuhitimisha hotuba yangu naomba sasa niweke msisitizo katika masuala muhimu yafuatayo ambayo ni uratibu wa upatikanaji wa pembejeo; udhibiti na utatuzi wa migogoro ya ardhi; uhifadhi wa mazingira na kuimarisha mazingira ya biashara.
Kuimarisha Uratibu wa Upatikanaji wa Pembejeo
74. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa pembejeo muhimu kwa wakulima zikiwemo mbolea. Hadi kufikia tarehe 31 Oktoba, 2023, wakulima zaidi ya milioni 3.6 walikuwa wamesajiliwa na kupata namba za utambulisho za kununua mbolea ya ruzuku.
75. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kupitia Bunge lako tukufu kuwaelekeza Wakuu wa Wilaya ambao pia ni Wenyeviti wa Kamati za Pembejeo za Wilaya wawahamasishe wakulima kujisajili na kutoa taarifa sahihi kuhusu mazao wanayolima na ukubwa wa mashamba yao kwenye madaftari ya wakulima ambayo yamesambazwa kwa watendaji wa vijiji na mitaa ili taarifa zao ziweze kuingizwa kwenye mfumo na wapatiwe namba za kununulia mbolea ya ruzuku.
76. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuielekeza Wizara ya Kilimo ihakikishe mbolea inapatikana kwa wakati na ishirikiane na Wakuu wa Wilaya kusimamia kwa karibu usambazaji wa mbolea kwa wakulima. Hatua hii iende sambamba na kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa usambazaji wa pembejeo hiyo muhimu.
77. Mheshimiwa Spika, vilevile, kampuni na taasisi zinazozalisha mbegu bora ziongeze kiwango cha uzalishaji na kuweka utaratibu mahsusi wa kufikisha mbegu hizo kwa wakulima katika maeneo yao ya uzalishaji.
Udhibiti na Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi
78. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kushughulikia migogoro ya ardhi kwa kushirikisha Wizara za kisekta.
Mikakati hiyo ni pamoja na kuunda kamati maalum za kushughulikia migogoro, kuendesha kliniki maalum za ardhi ambapo wananchi wamekuwa wakisikilizwa malalamiko yao na kupatiwa ufumbuzi.
79. Mheshimiwa Spika, mikakati mingine inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na kufanya vikao na wadau mbalimbali kuhusu usimamizi bora wa ardhi; kufanya kaguzi za milki; kutoa elimu kwa umma kuhusu utatuzi wa migogoro kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa na kuwajengea uwezo watumishi ili kuimarisha huduma zitolewazo kwa jamii.
80. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwachukulia hatua watumishi wanaochochea migogoro kwa kutozingatia sheria na kanuni na taratibu ikiwemo kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Vitendo hivyo havikubaliki kwani ni kinyume na maadili ya utendaji wa watumishi wa umma. Hivyo basi, nitumie fursa hii kumwagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuwachukulia hatua kali watumishi wa idara za ardhi wanaokiuka sheria. Hivyo basi, kila mmoja akafanye kazi kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia taaluma yake.
81. Mheshimiwa Spika, nilitoa maelekezo kwamba kampuni zote zilizopewa kazi za upimaji wa viwanja kwenye Majiji, Manispaa na Mikoa na zimeshindwa kukamilisha kazi hiyo, ziwe zilikuwa na mikataba ama hazikuwa na mikataba zichukuliwe hatua kali za kisheria.
Ikumbukwe kuwa, kampuni nyingi zilizopewa kazi za kupima maeneo ya wananchi kwa lengo la kutoa hati miliki kote nchini hazifanyi kazi hizo kikamilifu licha ya wananchi kulipa fedha kwa muda mrefu, nasisitiza kuwa kampuni hizo zikuchukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kuziachisha hizo.
82. Mheshimiwa Spika, nilielekeza pia kwamba, Halmashauri zote kama mamlaka za upangaji ziongeze udhibiti na usimamizi wa maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa ajili ya matumizi ya umma na yale ya hifadhi ya mazingira, yakiwepo maeneo ya ukanda wa kijani, maeneo ya wazi, viwanja vya michezo, makaburi na mengineyo ili kuzuia uvamizi na mabadiliko ya matumizi ya maeneo hayo. Mfano halisi ni Jiji la Dodoma na Manispaa ya Kigoma.
Maeneo yote yaliyotengwa na kuhifadhiwa yasiruhusiwe kufanyiwa mabadiliko ni vema mabadiliko hayo yawe yamerishiwa na Kamati za Usalama za Mikoa na Wilaya kabla ya kuwasilishwa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
MICHEZO
83. Mheshimiwa Spika, kipekee nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono mapana aliyonayo katika kuinua Sekta ya Michezo hapa nchini.
Mheshimiwa Rais, katika vipindi mbalimbali amekuwa akitoa miongozo ambayo imekuwa na tija na hatimaye kuleta mapinduzi makubwa katika ya sekta ya michezo.
Sina shaka mtakubaliana nami kuwa kupitia maono yake, tasnia ya Michezo nchini inaendelea kuthaminiwa na tumeendelea kushuhudia matunda mazuri kwa timu zetu zikiwemo zile za Taifa.
84. Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kuwa ili timu zetu za taifa ziweze kushiriki katika michuano ya kimataifa, maandalizi ya kutosha yanahitajika ambayo yanagharimu fedha nyingi.
Ninatoa pongezi kubwa sana kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya maamuzi sahihi ya kuiwezesha timu ya Taifa ya Tanzania kufuzu katika Fainali za AFCON.
85. Mheshimiwa Spika, aidha, Mheshimiwa Rais amekuwa akiridhia ujumbe maalumu wa Serikali kuambatana na Taifa Stars katika michezo yao ya ugenini ili kuongeza hamasa kwa wachezaji na matokeo kweli tumeyaona.
Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kutoa motisha kwa wanamichezo wetu ambazo zimekuwa zikiongeza ari na hamasa kwa wanamichezo wetu.
Licha ya kuendeleza mpango wa Goli la Mama, mtakumbuka Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo tarehe 4 Oktoba 2023 alinituma nikatekeleze ahadi yake ya kuwatunuku Timu ya Taifa Stars fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kwa kufuzu kushiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika nchini Ivory Coast Januari, 2024.
86. Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, mafanikio katika sekta ya michezo hapa nchini yamechagizwa pia michango ya Waheshimiwa Wabunge ambayo imekuwa ikitolewa ili kuboresha sekta ya michezo nchini.
Sote tu mashuhuda jamii sasa imehamasika na ushiriki katika michezo na umeongezeka. Michezo imekuwa zaidi ya burudani kwani sasa ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi kusaidia kutatua changamoto mbalimbali katika Jamii ikiwemo ile ya ajira kwa vijana.
87. Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) katika kutekeleza mikakati ya maendeleo ya michezo hapa nchini Tanzania.
Ushirikiano unaotolewa kwa taasisi za michezo umekuwa chachu ya kufanikiwa kutimiza malengo yetu ya kuendeleza michezo.
Mfano mzuri ni ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya Michezo kwa sekata ya umma na binafsi. Kwa mfano Azam Complex, taasisi za ulinzi, taasisi za elimu kwa mfano shule, vyuo na taasisi nyinginezo.
88. Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kutoa pongezi nyingi kwa TFF kwa uzinduzi wa Mashindano ya Ligi ya Soka ya Afrika uliofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Oktoba katika Uwanja wa Benjamin William Mkapa ambao haujawahi kutokea. Katika mechi hiyo ya uzinduzi Klabu ya Simba ilichuana na klabu ya Al Ahly ya Misri na kutoka sare.
89. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuipongeza sana Timu ya Taifa ya soka ya Wanawake chini ya umri wa miaka 20 almaarufu Tanzanite Queens kwa ushindi wa mabao 7 kwa 0 dhidi ya Djibouti katika mchezo wa kufuzu kombe la Dunia uliochezwa Uwanja wa Azam Complex tarehe 11 Oktoba, 2023.
Kwa ushindi huo, Tanzanite Queens watachuana na Nigeria katika pambano litakalofanyika nchini Colombia mwaka 2024.
90. Mheshimiwa Spika, ninawapongeza pia timu ya Twiga Stars kwa kusonga mbele katika hatua ya kufuzu mashindano ya WAFCON 2024.
Ushindi huo umepatikana baada ya kupata ushindi wa penati 4 kwa 2 baada ya kuifunga timu ya Ivory Coast kwenye shindano lililofanyika pia katika Uwanja wa Azam Complex pale Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Aidha, ninawapongeza pia timu ya Twiga Stars kwa kufuzu mashindano ya Olimpiki-2024 baada ya kuibwaga Botswana kwa bao moja bila katika mchezo uliofanyika nchini Botswana.
91. Mheshimiwa Spika, ninatoa pongezi nyingi kwa Timu ya wanawake ya JKT Queens kwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Wanawake Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA). Ubingwa huo umewawezesha kushiriki Ligi ya Mabingwa ya Wanawake Afrika inayoendelea nchini Ivory Coast.
92. Mheshimiwa Spika, licha ya mchezo wa mpira wa miguu, ninawapongeza pia, vijana wetu Ramadhan Brothers wanasarakasi mahiri walioshiriki katika mashindano maarufu ya American Got Talent.
Vijana wetu hawa wameonesha vipawa na uwezo wa hali ya juu katika mchezo huo na kukonga mioyo ya watazamaji wengi.
93. Mheshimiwa Spika, washiriki wetu katika mchezo wa ngumi wameendelea kung’ara sana katika mashindano ya ndani na nje ya nchi yetu.
Ninampongeza sana Mwanamasumbwi wetu Ibrahim Class kwa kushinda mkanda wa TPBRC baada ya kumshinda mpinzani wake Xiao Tau Su kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
94. Mheshimiwa Spika, ninampongeza pia mwanasumbwi Pius Mpenda kwa kushinda ubingwa wa WBC Peace Champion baada ya kumshinda Mrusi Dauren Yeleussinov.
Vilevile, ninampongeza sana Nahodha wa Timu ya Taifa ya Ngumi Ngorongoro Black Rhinos Yusuf Lucas Changalawe kwa kufanikiwa kuingia katika fainali ya mashindano ya Olimpiki ya Paris 2024.
95. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mchezo wa mashindano ya mbio, ninampongeza sana mwanariadha wetu Magdalena Shauri kwa kushinda medali ya shaba katika mbio za BMW Berlin Marathon baada kushika nafasi ya tatu katika mbio hizo.
Vilevile, ninampa pongezi nyingi Mwanariadha Alphonce Felix Simbu kwa kushika nafasi ya pili kwenye mashindano ya majeshi yanayojulikana kama The World CISM Half Marathon yaliyofanyika huko Uswisi. Ninawapongeza sana wanariadha wetu kwa ushindi huo mkubwa.
96. Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro (Mb.) Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kuendelea kusimamia vema utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais.
Jitihada zenu zinaonekana kwani Tanzania inazidi kung’ara katika medani za kimataifa. Sote tunaendelea kushuhudia maendeleo makubwa ya sekta hii muhimu katika kuchangia Pato la Taifa na kukuza uchumi kwa ujumla.
HITIMISHO
97. Mheshimiwa Spika, ninapoelekea kuhitimisha hotuba yangu, nitumie fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kufanya mjadala wa Bunge hili kwa kuzingatia manufaa makubwa ya ustawi wa taifa letu.
Kama mnavyofahamu uwepo wa Bunge hili ulikuwa ni muhimu ili kuweza kupata maoni na ushauri kutokana na hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Aidha ninawashukuru watumishi wa Serikali kwa kuendelea kufanyia kazi masuala mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwezesha uwasilishaji wa hoja mbalimbali zilizotokana na mijadala ya Bunge hili.
98. Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Katibu wa Bunge na Watumishi wote wa Bunge kwa huduma nzuri mliyotupatia katika kipindi chote cha Bunge hili. Kipekee, nivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi yanu nzuri, kwa maana tumeishi kwa amani na utulivu katika kipindi chote cha Mkutano huu wa 13 wa Bunge la 12.
Ninawashukuru sana wanahabari kwa kuendelea kuuhabarisha umma juu ya shughuli zote za Bunge letu Tukufu toka siku ya kwanza mpaka siku hii ya leo tunapoelekea kuhitimisha mkutano wetu.
Pia natambua mchango mkubwa wa huduma unaotolewa na madereva wetu waliotuhudumia wakati wote. Pia ninatoa shukurani kwa watoa huduma wengine mlioshiriki kutuhudumia muda wote tukiwa hapa Dodoma.
99. Mheshimiwa Spika, nirudie kukushukuru sana, wewe na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, niwaahidi kuwa tutaendelea kutekeleza yale mliyoyashauri na kuyatolea maoni katika kipindi chote cha mkutano wa Bunge hili, kwani ushauri na maponi yenu ndio msingi wa kuiwezesha Serikali kutimiza majukumu yake ipasavyo.
Nami niwatakie Waheshimiwa Wabunge wenzangu safari njema na mnaporejea majimboni kwenu na mkaendelee kuwahakikishia wananchi dhamira njema ya Rais wetu Dkt. Samia suluhu Hassan katika kuwaletea maendeleo Watanzania.
100. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tunaelekea mwishoni mwa mwaka, na hatutakuwa na Mkutano wa Bunge tena ndani ya mwaka 2023, nitumie fursa hii kuwatakia Watanzania na waumini wote wa Kikristo, sherehe njema ya sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya wa 2024.
101. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa ninapenda kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu liahirishwe hadi siku ya Jumanne, tarehe 30 Januari, 2024 saa tatu kamili asubuhi litakapokutana tena katika ukumbi huu hapa Jijini Dodoma.
102. Mheshimiwa Spika, sasa, ninaomba kutoa hoja.

Tags
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Habari
Hotuba ya Waziri Mkuu
Makala
Ofisi ya Waziri Mkuu