NA BROWN JONAS
MAWAZIRI wa Michezo wa Tanzania, Kenya na Uganda wamekutana na timu ya wataalamu kutoka nchi hizo kuweka mikakati ya pamoja kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2027, leo Novemba 7, 2023 mjini Mombasa nchini Kenya.
Kwa upande wa Tanzania kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Tabia Maulid Mwita, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Wallace Karia Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo Ally Mayai, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Bi. Neema Msitha na wataalamu wengine.
Kenya imewakilishwa na Waziri wa Michezo Mhe. Ababu Namwamba na Katibu Mkuu, Mhandisi Peter Tum huku Uganda ikiwakilishwa na Bw. Rodgers Byamukama ambaye ni Mjumbe wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini humo.
Kikao hicho ni cha kwanza tangu Tanzania, Kenya na Uganda ziliposhinda ombi la kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.