MCHANGO WA MBUNGE WA JIMBO LA KISESA, MHE.LUHAGA JOELSON MPINA AKICHANGIA KUHUSU MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA MWONGOZO WA BAJETI KWA MWAKA 2024/2025 BUNGENI DODOMA TAREHE 8 NOVEMBA 2023
1: UTANGULIZI
Nimesoma mawasilisho yote yaliyowasilishwa na waheshimiwa Mawaziri, kabla ya kufikiria mpango mpya ni muhimu sana kufanya tathmini ya kina juu ya mafanikio na changamoto za mpango unaomalizika.
Vinginevyo tutaendelea kukutana kila mwaka kuweka mipango ambayo haina matokeo yaliyokusudiwa.Tusipokuwa na vyanzo vya mapato vya uhakika vya ugharamiaji wa utekelezaji wa mpango,mikataba mibovu na matumizi mabaya ya Serikali na kuwepo kwa ubadhirifu, wizi, rushwa na ufisadi, kukosekana weledi na bidii ya kazi kama ilivyothitishwa na taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022.
Kwa mwendo huu hatutaweza kufikia malengo na shabaha ya mpango. Ninachokiona hapa mikakati ya kutekeleza Mpango ni ile ile iliyokuwepo mwaka uliopita ambapo tumekutana na changamoto nyingi katika utekelezaji wa miradi lakini pia mikakati ya kukabiliana na vihatarishi vya mpango nayo ni ile ile hivyo kunipa mashaka makubwa kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Mwaka 2024/2025.
2. UCHAMBUZI WA MAPENDEKEZO YA MPANGO
Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Uwekezaji amesisitiza kuwa mipango ya sasa na itakayoandaliwa baadaye itajikita katika kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi wetu unakuwa jumuishi, unapunguza umasikini, unazalisha ajira nyingi, unatengeneza utajiri na unachochea mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi.
Hii kauli mbiu aliyokuja nayo Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Mhe. Profesa Kitila Mkumbo ni nzuri na ya
kupongezwa ingawa mashaka yangu makubwa ni utekelezaji wa kauli mbiu hiyo kwani mara nyingi tumekuwa tukifanya kinyume chake, nimesoma hotuba ya Waziri na Mapendekezo ya Mpango sijaona mkakati wa kutekeleza kauli mbiu ya mpango huu.
2.1 Ulinzi wa Viwanda na Ajira nchini
Suala la kukuza viwanda na kutengeneza ajira lipo kwenye vitabu vya mipango na hotuba za viongozi lakini kiuhalisia mambo mengi tunayofanya ni ya kuua viwanda na kuhamisha ajira nchini. Nitoe mifano machache kama ifuatavyo:-
(a) TANESCO na REA kwa sehemu kubwa inanunua vifaa vya umeme kutoka nje ya nchi hata kwa vifaa ambavyo vinatengenezwa na viwanda vya ndani nchini.
(b) Licha ya nchi yetu kubahatisha mwekezaji wa kiwanda kikubwa cha Chanjo za mifugo Kampuni ya Hester Bioscience African Limited kutoka India kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani lakini kwa sehemu kubwa chanjo za mifugo zinaagizwa kutoka nje ya nchi.
(c) Viuatilifu, mbegu, mbolea, dawa kwa sehemu kubwa zinaagizwa nje ya nchi wakati zinazalishwa nchini na uwezo wa kuongeza uzalishaji upo.
(d) Kazi na miradi mingi wanapewa makampuni ya kigeni hata kwa miradi ambayo ingeweza kufanywa na wazawa.
Kama miradi ya TANROADS, REA, RUWASA, TANESCO nk. mifumo ya TEHAMA kutoka nje ya nchi kama wa ETS.
Ukarabati wa Kivuko cha Mv Magogoni kufanyiwa na kampuni ya Kenya badala ya Kampuni ya Songoro Marine Transport LTD na hapa ulifanyika upendeleo wa wazi na wa kuvunja Sheria za nchi. Pia vibali vya bidhaa muhimu vinatolewa kiholela.
(e) Utoaji wa vibali na uagizaji holela wa bidhaa za mchele, ngano, maziwa, nyama, mbogamboga na matunda,mayai, kuku, samaki, vifaa vya ujenzi, samani, sabuni, viatu, nguo na mafuta kutoka nje ya nchi.
(f) Biashara za magendo,uingizaji wa bidhaa feki na bandia na mauzo ya mazao ghafi nje ya nchi ambayo hajaongezwa thamani.
Hapa kwa hii mifano michache niliyoitaja, fursa na raslimali zilizopo nchini zinanufaisha uchumi wa mataifa mengine huku watanzania wakibaki kuwa watazamaji.
Pia inathibitisha kuwa hakuna ulinzi wa ajira wala ulinzi wa viwanda na uwekezaji ndani ya nchi hivyo ni vigumu sana kufikia malengo ya mpango.
2.2 Usimamizi wa pembejeo na bei za mazao ya wakulima
Kwa sasa kuna Usimamizi usioridhisha wa viwango na bei za mbolea, viuatilifu na mbegu. Pia usimamizi dhaifu wa bei ya mazao ya wakulima (pamba).
(i) Kwa nini Serikali imeshindwa kuweka mfumo mzuri wa ufuatiliaji na uhakiki wa bei zinazotamkwa na wafanyabiashara za mbolea, viuatilifu na mbegu hali inayosababisha kupatikana kwa bei kubwa na
kukwamisha kilimo nchini.
Pembejeo hizi za kilimo zimekuwa zikichelewa na kuuzwa kwa bei kubwa isiyo na uhalisia mfano mfuko wa kilo 2 za mbegu ya mahindi kuuzwa shilingi 24,000 wakati mahindi ya kawaida kuuzwa kwa Tsh. 1,200 kwa kilo 2.
(ii) Je kwanini Serikali ilitumia mfumo wa mbolea ya ruzuku ambao ulikuwa na kasoro nyingi na haukuwa na kibali cha eGA na kupelekea Wakulima zaidi ya milioni 2.2 kukosa mbolea na kutumia zaidi ya Tsh Bilioni 64 ya kiwango kilichoruhusiwa na Bunge.
(iii) Mamlaka zinazosimamia zinatekeleza vipi wajibu wake hadi haya yatokee, mamlaka za TPRI, TFRA, ASA, TARI na TOSCI?
(iv) Kwa nini wananchi wanaendelea kuuziwa viuatilifu feki vinavyonenepesha wadudu badala ya kuua na kupata hasara kubwa kwenye kilimo. Tatizo la ukosefu wa viuatilifu limetatuliwaje na Serikali. TPRI wako wapi hadi mambo haya yanatokea.
(v) Bei ya Pamba, ni utafiti gani wa kimasoko wa ndani na katika soko la dunia uliofanywa kuthibitisha uhalali wa bei ya pamba iliyotumika kwa Wakulima mwaka huu?
Ninaamini kuwa endapo kutakuwepo na ufuatiliaji na usimamizi makini gharama za pembejeo zitashuka, Masoko na bei nzuri ya mazao ya Wakulima itapatikana, hivi sasa Wakulima wanapata
hasara na umasikini mkubwa kutokana na anguko la bei ya mazao na gharama kubwa za pembejeo na hivyo si rahisi kufikia malengo ya mpango ya kuwatajirisha wananchi.
2.3 Ukamataji na utozaji faini holela wa mifugo inapokamatwa ndani ya hifadhi,
Kwa nini Serikali kupitia TAWA, TFS, TANAPA inatoza faini ya Tsh.100,000 kwa kichwa cha ng’ombe jambo ambalo ni kinyume cha sheria? Licha ya Waziri Mkuu kupiga marufuku, Bunge kulalamikia maagizo ya Waziri Mkuu kudharauliwa, maafisa wa uhifadhi wanaendelea na ukamataji holela, upigaji faini holela, uuzaji wa mifugo holela na mbaya zaidi hapa Bungeni Waziri wa Maliasili ameliambia Bunge kuwa wanaofanyiwa hayo waende Mahakamani, Kauli hii imetolewa ndani ya Bunge akiwemo Waziri Mkuu.
Wananchi wamelalamika kupitia wabunge wao kuhusu uvunjaji wa sheria unaofanywa na Taasisi za Serikali alafu wanaambiwa waende Mahakamani na hata waliokwenda Mahakamani na kushinda kesi mpaka leo hawajarudishiwa mifugo yao.
Ipo mifano ya siku za karibuni katika Wilaya ya Meatu na Wilaya ya Ngorongoro ambapo mifugo zaidi ya 4,000 imekamatwa kiholela, kupigwa faini ya Tsh 100,000 kwa kila ng’ombe na mifugo mingine kuuzwa kiholela porini kwa bei ya kutupwa kiasi cha Tsh 120,000 kwa kila ng’ombe badala ya bei ya soko ya wastani wa Tsh. 750,000 kwa kila ng’ombe kinyume na Kanuni Animal Welfare (Impounded Animal) Regulation 2020.
Badala ya taifa letu kutumia fursa ya uwepo wa mifugo mingi nchini tuliyojaliwa na Mungu, lakini Serikali iko bize kuwafilisi wafugaji kila uchao, nilitegemea tungejikita kutengeneza programu na mikakati ya kuongeza uzalishaji wa nyama, maziwa, ngozi, siagi, samadi, mayai, vifaranga, wanyama kazi na kuuza katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Hivyo kukuza uchumi, kuzalisha
ajira na kupunguza umasikini.
2.4 Kusuasua kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo
(i) Mradi wa SGR
Hatua iliyofikiwa Dar es Salaam- Morogoro (Km 300) asilimia 98.6, Morogoro- Makutupora (Km 412) asilimia 95.41, Mwanza- Isaka (Km 341) asilimia 41.95, Makutupora-Tabora (371) asilimia 12.32, Tabora- Isaka (Km 165) asilimia 5.02, Tabora-Kigoma (Km 506) asilimia 0.29.
(a) Nini kilichosababisha Mradi wa SGR Lot. 1 na Lot. 2 kutokukamilika hadi leo zaidi ya miaka 6.
(b) Nini kilichosababisha kusuasua kwa utekelezaji wa miradi ya SGR Lot. 3 (12.32%), Lot 4. (5.02%) na Lot. 6 (0.29%) tangu isainiwe Mikataba yake miaka 2 iliyopita.
(c) Nini kinachosababisha kuwepo kwa malalamiko na migomo ya wafanyakazi wanaojenga reli ya SGR?
Nionavyo mimi kuna changamoto kubwa ya usimamizi, uwezo mdogo wa wakandarasi na utoaji hafifu wa fedha katika miradi ya SGR hali inayopelekea miradi kusuasua.
Kuchelewa kukamilika kwa miradi kunaliingiza taifa kwenye hasara kubwa kwa kuwa gharama zinazidi kuongezeka, fedha zilizowekezwa hazizalishi mali na ajira, mikopo kuiva kulipwa kabla ya mradi haujaanza kuzalisha na wananchi kuchelewa kupata huduma ya usafiri na usafirishaji.
(ii) Miradi ya Barabara inayofadhiliwa kwa utaratibu wa EPC+F
Utekelezaji wa Mikataba hii haujaanza tangu usainiwe mwezi Juni 2023 miezi 6 iliyopita. Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa alipokuwa ziara Mkoa wa Simiyu (Daraja la Mto Sibiti)
alieleza kuwa ucheleweshaji huo unasababishwa na kuchelewa kulipwa 10% ya gharama ya mradi ambayo ni Tsh. Bilioni 377.5, vile vile Waziri wa Ujenzi ndani ya Bunge ameeleza kuwa katika kipindi cha miezi 6 wakandarasi wanafanya usanifu wa kina wa miradi hiyo (Preliminaries Design)
Awali aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa Mnyaa siku ya kusaini Mikataba wa wakandarasi Juni 2023 alisema Serikali imepata Makandarasi wa kujenga barabara
saba (7) kwa kiwango cha lami zenye jumla ya urefu wa kilometa 2,035 kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Trilioni 3.775 kwa kutumia utaratibu wa Engineering, Procurement, Construction and Financing (EPC + F) kwamba mkandarasi atajenga kwa gharama zake na kukabidhi mradi kwa Serikali.
Maswali na Uchambuzi\
(i) Kwa kuwa Waziri Prof. Mbarawa alitueleza kuwa wakandarasi hao watajenga barabara hizo kwa fedha zao hadi kukamilika, Je haya madai ya kutaka kulipwa malipo ya awali Tsh Bilioni 377.5 yametoka wapi? Na kama Serikali inalipa malipo ya awali nini maana ya EPC+F?
Hapa tuelezwe bayana namna Serikali itakavyowalipa wakandarasi wa miradi ya barabara ya EPC+F kiasi cha Tsh. Trilioni 3.775.
(ii) Wakandarasi waliwezaje kuomba na kusaini Mikataba kabla ya kufanya usanifu wa kina wa miradi hiyo (Preliminaries Design) ili kujua mahitaji na gharama?
(iii) Nini faida ya kutumia utaratibu wa EPC+F ikilinganishwa na utaratibu wa zabuni wa kawaida? Gharama ya kujenga kilomita moja ya lami ni kiasi gani kwa njia ya EPC+F? na wastani wa ujenzi wa kilomita 1 ya lami kwa njia ya zabuni ya kawaida ni kiasi gani?
(iv) Je usimamizi wa miradi ya EPC+F utakuwaje kwa kuwa fedha hazipiti Hazina na CAG hawezi kukagua miradi hiyo?
Nionavyo mimi Mikataba hii ya ujenzi wa barabara inayojengwa kwa utaratibu wa EPC+F yenye thamani ya Tsh. Trilioni 3.775 ambayo itakamilika kwa kipindi cha miaka 5, ni Mikataba Mibovu
itakayoliingiza Taifa kwenye hasara kubwa. Gharama za mradi ni kubwa, inaua viwanda na uwekezaji nchini, inaua na kuhamisha ajira nchini.
Hakuna uchumi jumuishi na unawafanya watanzania kuwa watazamaji wa makampuni ya kigeni. Ushauri wangu, Mikataba ya Makampuni 4 ya Kichina ya China Civil Engineering Construction Company (CCECC), Sino hydro Corporation LTD, China Overseas Engineering Group Co. LTD
(COVEC) na China Railway Company 15th Bureau Group (CR15G) na TANROADs ivunjwe kabla haijawaingiza hasara kubwa watanzania.
2.5 MIKATABA INAYOINGIWA NA SERIKALI
2.5.1 Mikataba iliyofanyiwa upekuzi
Katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Aprili, 2023, Serikali iliingia Mikataba ya kitaifa na kimataifa 1,304 ambapo ilifanyiwa upekuzi na kuthaminishwa kwa thamani ya Tsh Trilioni 91 na kati ya Mikataba hiyo Mikataba 43 ni ya raslimali na maliasili za nchi.
Maswali ya kujiuliza
(i) Kwa nini Serikali inaendelea kuingia mikataba kwa siri na kwanini imekaidi agizo la Bunge la
kuwasilisha orodha ya Mikataba hiyo Bungeni yenye thamani ya Tsh. Trilioni 91?
(ii) Kwa nini Serikali imeingia mikataba 43 ya raslimali na maliasili za nchi kinyume cha sheria? Kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Sheria ya Ulinzi wa Raslimali (The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act No.5 of 2017) ambacho kinataka Mikataba hiyo kuletwa Bungeni,
lakini Serikali haijaleta mikataba hiyo Bungeni hadi sasa.
Pia kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya The Tanzania Extractive Industries (Transparency and Accountability) Act 2015 ambacho kinataka miradi, leseni, vipengele na mikataba kuwekwa wazi kwenye tovuti na kutangazwa kwenye vyombo vya habari. Mikataba hii imeingiwa kwa siri, vigezo na masharti ya Mikataba hiyo haijulikani.
2.5.2 Mkataba wa Mradi wa usindikaji na Uchakataji Gesi Asilia (LNG)
Mapendekezo ya Mpango yanaeleza kuwa hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa majadiliano ya mkataba baina ya nchi hodhi (Host Government Agreement-HGA) na Mkataba wa uzalishaji na ugawanaji mapato (Amended Production Sharing Agreement- PSA) kati ya Serikali na Kampuni za kimataifa za Nishati (International Energy Companies –IECs). Hizi hatua zimefikiwajebila Bunge.
Awali Juni 2023 tulielezwa kuwa wataalam wapo katika kazi ya kuandika mikataba ya mradi huo. Mkataba mmoja ni wa Nchi Hodhi (HGA) na mwingine ni mkataba uliounganishwa wa vitalu
vya Gesi Asilia Namba I, II na IV ambavyo gesi yake itatumika kwenye mradi wa Mradi wa Liquefied Natural Gas (LNG Project) ili kuliwezesha taifa letu kuanza kunufaika na raslimali ya gesi asilia tuliyobarikiwa na Mwenyezi Mungu ambapo akiba ya gesi asili iliyopo nchini mwetu ni futi za ujazo (cubic feet) Trilioni 57.
Maswali na uchambuzi
(i) Kwa nini Serikali imefanya mapitio ya PSA kwa siri na bila kuwashirikisha wananchi? Upande wangu sijaona taarifa ya kufanyiwa mapitio Mkataba wa uzalishaji na ugawanaji mapato (Amended Production Sharing Agreement- PSA) wala GN ya PSA katika vitalu na 1, 2 na 4 vinavyokwenda kutumika katika mradi wa LNG. Na hii ni kinyume cha Sheria ya TEIT na Natural Resources.
(ii) Je Government Negotiation Team (GNT) imefika hitimisho ya vipengele vya mikataba wa HGA na vitalu na 1, 2 na 4 kwa ajili ya mradi wa LNG kwa kutumia nyaraka gani au PSA zipi wakati marekebisho ya PSA yalikuwa hayajakamilika.
(iii) Je ni kwa nini Serikali imeendesha majadiliano katika vipengele vya mikataba kwa usiri kinyume na sheria za nchi kuhusu raslimali za nchi? Tangu mazungumzo yaanze baina ya GNT na wawekezaji hapakuwa na ushirikishwaji mpana wa wananchi, GNT ilitakiwa kufanya public hearing kwa kushirikisha watu wenye taaluma mbalimbali na Bunge kabla ya kufika hitimisho la majadiliano ya vipengele vya mkataba.
Kilichofanyika ni kinyume na kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya The Tanzania Extractive Industries
(Transparency and Accountability) Act 2015 na Kifungu cha 12 cha Sheria ya Ulinzi wa Raslimali (The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act No.5 of 2017).
(iv) Kwa nini Serikali imeingia mkataba na Kampuni ya Baker Botts LLP ya Uingereza kama mshauri elekezi wakati huo Kampuni ya Shell nayo inatoka Uingereza hapa tunawezaje kuzuia mgongano wa maslahi (Conflict of Interest).
2.5.3 Mikataba ya uwekezaji wa Bandari (HGAs) Ibara ya 35 ya Hotuba ya Waziri ukurasa wa 16, Baada ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mamlaka ya Falme ya Dubai kuingia katika mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi (IGA) Mwezi Oktoba 2022, hivi sasa mikataba mitatu ya utekelezaji wa miradi katika kuwekeza na kuendesha gati 0-3 na gati 4-7 zilisainiwa kati ya TPA na DP World Tarehe 22 Oktoba 2023.Nimepitia hotuba ya Waziri ametaja kuingiwa kwa Mikataba pekee bila kueleza kwa kina.
(i) Kwa nini Serikali inafanya siri kwa raslimali muhimu kama Bandari hadi imeshindwa kuweka bayana Kampuni ya DP World inakwenda kuwekeza maeneo gani na kwa gharama gani? Kwa minajili ya kuboresha na kuongeza ufanisi wa bandari. Je ni tathmini gani iliyofanyika kubainisha mahitaji ya uwekezaji huo?
(ii) Kwanini Mikataba hiyo ya Bandari tangu kusainiwa kwake hadi sasa haijaletwa Bungeni kama lilivyo takwa la kisheria ili kujua kwa uwazi nini kilichosainiwa na maslahi ya taifa yamezingatiwaje kama Sheria ya TEIT na Natural Wealth inavyotaka.
Sheria ya Natural Wealth na TEIT zinataka michakato na Mikataba ya raslimali na maliasili kuwa wazi na kuridhiwa na Bunge, lakini Serikali imeenda kuingia Mikataba 43 kwa siri na bila kulishirikisha
Bunge. Hii ina inaleta mashaka makubwa juu ya uhalali wa Mikataba hiyo. Lakini pia usiri unaondelea katika maandalizi ya Mikataba ya LNG mradi wenye thamani ya zaidi ya Tsh. Trilioni 80 na Mikataba ya uwekezaji wa DP World inatia mashaka makubwa juu ya uhalali wake.
2.6 Huduma za Mawasiliano ya Simu na Intaneti Nchi yetu imepiga hatua kubwa katika kufikisha mawasiliano sehemu mbalimbali nchini ambapo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ( Seacom International undersea fibre optic network) umesambazawa nchini kwa Jumla ya Kilomita 8,319 na laini
zilizosajiliwa zimefikia Milioni 62.3, wanaotumia Intaneti kufikia Milioni 33.1 huku Matumizi ya kusafirisha pesa kwa njia ya simu yakiwa yameongeza na kuwa njia ya kutegemewa na wananchi.
Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA kwa kushika nafasi ya 26 kidunia na ya pili barani Afrika baada ya Mauritius kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia (WB) mwaka 2022 kuhusu ukomavu wa matumizi ya Teknolojia duniani katika utoaji wa huduma za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi (GovTech Maturity Index).
Maswali na uchambuzi
(i) Nini kinachosababisha mabando, vifurushi vya mitandao ya simu kuongezeka kwa ongezeko la zaidi
ya 300% kutoka Septemba 2021 hadi sasa 2023.
Gharama hizi zimekuwa kubwa wananchi wameshindwa kunufaika kwa kiwango kinachostahili
na maendeleo ya TEHAMA nchini mwao mfano matumizi ya Intaneti kwa wanafunzi, madaktari,
wafanyabiashara nk.
(ii) Ni mifumo mingapi tunayotumia ya kutoka nje ya nchi na nini kinachotufanya tununue na kutumia
mifumo ya TEHAMA kutoka nje ya nchi wakati tumeshapiga hatua kubwa hapa nchini ikiwemo
uwepo wa wataalamu wabobezi wa kujenga na kuendesha mifumo ya TEHAMA.
Mfano wa mifumo kutoka nje ni ule wa TANESCO (unaojengwa na Tech Mahindra) na Mfumo wa TRA (ETS- unaoendeshwa na SICPA) ambapo mifumo hii inalalamikiwa nchini.
Mimi naamini hizi gharama za mabando na vifurushi vya simu zinaweza kushuka kama Mamlaka husika za TCRA na eGA zitafanya ukaguzi na utafiti wa kisayansi kubaini uhalali
wa bei zinazotumika hivi sasa na kuweka bei elekezi. Ni lazima uongozi wetu uwape raha wananchi na sio kuwaumiza.
2.7 Huduma ya Nishati ya Umeme na Mafuta
Ni vigumu sana kufikia malengo ya Mpango kama uhaba wa nishati ya umeme utaendelea na bei za nishati ya mafuta zikaendelea zilivyo sasa.
Sababu za migao na katakata ya umeme zimekuwa hazieleweki tangu Septemba 2021 kila siku mara ukame, mvua zikinyesha mnaambiwa ukarabati wa mitambo na njia za kusafirisha umeme, mara Matumizi ya umeme yameongezeka viwandani na majumbani.
Lakini takwimu tulizonazo ni kwamba umeme tulionao ni mwingi kuliko mahitaji tuliyonayo. Upande wa Nishati ya Mafuta hadi sasa bei ya nishati ya mafuta bado ziko juu na zinazidi kupanda kila uchao na kuchangia kwa kiwango kikubwa kupanda kwa bei za bidhaa na kusababisha ugumu wa maisha kwa watanzania.
Awali tuliambiwa sababu ni vita vya Ukraine na Urusi. Kwa mujibu wa Sheria, EWURA inayo jukumu la kupokea taarifa ya utendaji (Performance Report) ya kila mwezi na kufanya ukaguzi wa uzingatiaji (Compliance Audit) kila mwaka ili kujiridhisha na utendaji pamoja na uzingatiaji wa shughuli za utoaji wa huduma za nishati ya umeme (TANESCO) na mafuta (TPDC) nchini.
Maswali na Uchambuzi
(i) Kwa nini Serikali imeshindwa kutoa majibu ya kisayansi kuhusu katakata ya umeme
inayoendelea na upandaji wa bei ya nishati ya mafuta kuanzia Septemba 2021.
Na kwanini Serikali imeshindwa kutoa taarifa ya ufuatiliaji na uhakiki wa bei za nishati ya mafuta
katika soko la dunia (Due Diligence).
(ii) Ni kwa mujibu wa taarifa na ukaguzi gani uliofanywa na EWURA kwa TANESCO na TPDC unaothibitisha usahihi na uhalali wa sababu zinazotolewa za:-
(a) Migao na katakata za umeme isiyoisha iliyoanza Septemba 2021 hadi sasa Novemba
2023
(b) Bei za nishati ya mafuta kupanda kutoka wastani wa Tsh 2,400 kwa lita 2021 hadi Tsh 3,500 mwaka 2023 ongezeko la 45%.
Pamoja na sababu nyingine ambazo ziko nje ya uwezo wetu, ninaamini kuwa hadi sasa nchi yetu ina migao na katakata ya umeme ya kutengenezwa na genge la watu kwa manufaa yao binafsi.
Pia upande wa bei za nishati ya mafuta, bei zilizopo hazina uhalisia zimepandishwa kiholela kwa maslahi binafsi.
Hakuna uhakiki na ufuatiliaji wa bei katika soko la dunia na soko la ndani (Due Diligence) ili kujiridhisha na uhalali wa bei unaotamkwa na wafanyabiashara wanaoagiza na kusambaza mafuta nchini, PBPA na EWURA huwaoni wapi wamedhibiti hali hiyo matokeo yake kuna udhibiti hafifu wa bei za mafuta na kusababisha bei ya mafuta kuendelea kuwa juu kwa visingizio vya soko la dunia na gharama na faida (Premium).
Leo watanzania wanateseka kutoka na kupanda kwa nishati ya mafuta na uhaba wa umeme ambao umesababisha mfumko mkubwa wa bei na ugumu wa maisha, uzalishaji viwandani umeshuka, mali na bidhaa za wananchi kuharibika.
Pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali za ujenzi na ukarabati wa mitambo na miundombinu ya kusafirisha umeme, naamini kuwa katakata ya umeme na upandishaji wa bei za nishati ya mafuta zinaweza kutatuliwa kwa kuziba mianya ya upigaji, kuimarisha menejimenti na bodi za TANESCO, TPDC na PBPA pia EWURA na PPRA kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa uzingatiaji (Compliance Audit) katika taasisi husika.
Haya Maelezo yangu yanathibitishwa na usimamizi makini uliokuwepo ambapo kwa miaka 6 iliyopita kulikuwa na utulivu wa bei za mafuta na katakata na migao ya umeme ilipungua kwa kiasi
kikubwa lakini matatizo makubwa yalikuja kuanza Septemba 2021 hadi sasa.
2.8 Kuhuisha Sera, Mitaala, Sheria na miongozo ya utoaji wa elimu na mafunzo nchini Serikali imekamilisha kuandaa sera na mtaala mpya wa elimu, jambo ambalo tulisubiri kwa muda mrefu kuona maboresho yakifanyika na kwa ujumla Sera na Mtaala mpya umesheheni mambo mazuri.
Binafsi ninaona kuna changamoto kubwa katika maeneo mawili kwa Sera, sasa elimu ya msingi na ya sekondari (kidato cha 4) kuwa ya lazima hivyo mwanafunzi atasoma kutoka shule ya awali hadi kidato cha 4 bila kuzingatia ufaulu au kufeli mitihani ya darasa la 4, Darasa la 6 na Kidato cha 2, kwani badala ya mitihani kutakuwepo na assessment.lakini pia ili kukidhi mahitaji itatulazimu kuwa na sekondari kila
kijiji na kuongeza miundombinu iliyopo katika sekondari.
Pia mahitaji ya madawati, vitabu na walimu yataongezeka. Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda ametangaza sera hiyo itaanza kutekelezwa mwaka wa masomo 2024.
(i) Kwa kuwa tumekubali kuwa na sera ya namna hiyo na inaanza kutumika mwaka wa masomo 2024 Je kupitia mpango huu tumejiandaaje kama taifa kugharamia ujenzi wa sekondari mpya kila kijiji na ongezeko la miundombinu kama madarasa, vyoo, nyumba za walimu, hosteli na pia ongezeko la vitabu, madawati na walimu.
Wastani wa 25% ya wanafunzi wanaofanya mtihani wa Darasa la 7 kila mwaka huwa wanafeli mtihani wa kuingia kidato cha 1, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2023
Wanafunzi wa Darasa la 7 waliofanya mtihani ni 1,397,370, hivyo inakadiriwa wanafunzi 349,343 hawataenda kidato cha 1 mwakani kutokana na kufeli mtihani.
Nionavyo mimi bado nchi yetu ina changamoto nyingi za Kiuchumi na Kijamii hivyo si rahisi kubeba mfumo wa elimu wenye gharama kubwa kiasi hiki. Tangu tuanze ujenzi wa Sekondari kila kata hatujafanikiwa kiasi kinachostahili kuboresha shule hizo kwani bado zina mapungufu makubwa
ya miundombinu na upungufu mkubwa wa walimu, vitabu, madawati. Badala ya kukimbilia kuanzisha mfumo mpya wa elimu ni bora tungeboresha shule zetu tulizonazo sasa.
(ii) Je utaratibu wa mwanafunzi kusoma kuanzia shule ya awali hadi Kidato cha 4 bila kipimo cha mitihani wa Taifa unalenga kuboresha elimu au kuua elimu nchini?
Awali tuliwahi kufanya makosa kwa kuondoa mtihani wa Taifa wa Darasa la 4 na Mtihani wa Taifa wa Kidato cha 2 jambo lilileta Malalamiko makubwa kwa wadau wa elimu, wananchi na wanafunzi. Je hili wazo la kuondoa mitihani na kuleta assessment limetokana na nini?
Nionavyo mimi hizi ni njama za kuua elimu hasa kwa watoto wa masikini ambao hawana fursa ya kusoma shule za kulipia au nje nchi. Kuna maslahi gani ya kulazimisha kijana ambaye hakufaulu mitihani ya shule ya msingi kwenda sekondari?
Pengine hata hajui kusoma na kuandika naye aende sekondari tu? Lakini pia maamuzi haya hayajazingatia mfumo wa maisha na mgawanyo wa kazi katika jamii zetu na taifa.
Kwani kusoma kwa miaka 11 bila cheti ni muda mrefu sana. Nashauri Mapungufu niliyobaisha yafanyiwe maboresho kabla ya kuanza utekelezaji wa sera mpya ya elimu mwaka 2024.
3. Ushauri
Ushauri kwa Prof. Kitila Mkumbo (Mb) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ambaye kwa moyo wa dhati nampongeza kwa dhamana kubwa aliyopewa na Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kulitumikia taifa letu katika nafasi hiyo nyeti.
Ninamshauri yafuatayo:-
(i) Kuandaa na kutekeleza mkakati utakaowezesha ukuaji wa uchumi wetu unakuwa jumuishi, unapunguza umasikini, unazalisha ajira nyingi, unatengeneza utajiri na unachochea mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi.
(ii) Aunde timu ya wataalamu (Mult Task Team) kupitia Mikataba na utekelezaji wa miradi yote ya kimkakati ya SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere, Bandari ya Uvuvi, DP World, Miradi ya EPC+F, LNG, Miradi ya REA, PPP, Daraja la Kigongo Busisi, Meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu ili kubaini kasoro zote na kuchukua hatua stahiki.
(iii) Kufanya mapitio na kusimamia kikamilifu mikataba na vibali vinavyotolewa na Wizara na taasisi zote nunuzi kuhakikisha kuwa kila taasisi ya Serikali inazingatia ushiriki wa wazawa (Local Content) na Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2023 inayoweka ulazima wa wazawa kupewa kipaumbele katika zabuni zote na kulinda viwanda na wawekezaji wa ndani.
Mikataba na vibali vinavyotolewa vya Manunuzi holela ya nje ya nchi vifutwe lakini pia kukomesha magendo na dhuluma za kila aina nchini.
(iv) Kufanya uchunguzi kwa baadhi ya Makampuni ambayo yanapewa zabuni nyingi kila mradi wanapewa wao hali inayopelekea miradi mingi kusuasua utekelezaji wake.
Mfano Kampuni ya China Civil Engineering Construction Company (CCECC) ambayo imepewa zabuni ya miradi ya SGR, EPC+F, Barabara za mzunguko Dodoma, Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria-Simiyu, Mradi wa Maji wa Miji 28 nk.
(v) Kufanya uhakiki na ufuatiliaji wa bei (Due Diligence) kupitia Mamlaka za PPRA, EWURA, TCRA, TOSCI,TFRA, TMDA, TPRI, CPB, FCC ili kujua sababu za kisayansi zilizopelekea migao na katakata ya umeme isiyoisha, kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta,kupanda bei ya mabando na vifurushi vya simu, bei za mbolea, mbegu, viuatilifu, chanjo na dawa, ngano,mafuta ya kula na bidhaa zingine muhimu.
Nawasilisha,
……………………………………
Luhaga Joelson Mpina (Mb)
Mbunge wa Jimbo la Kisesa