MUHIMBILI KUONDOA MTOTO WA JICHO KWA NJIA YA MATUNDU MADOGO

DAR ES SALAAM-Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa wa Macho kutoka Korea inatarajia kuweka kambi maalumu ya upasuaji wa macho kwa njia ya matundu madogo kwa wagonjwa wenye matatizo ya mtoto wa jicho.

Kambi hiyo ambayo inaratibiwa na MNH kwa kushirikiana na Taasisi ya Vision Care, itafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 27 Novemba hadi tarehe 2 Desemba 2023, ikiwa ni muendelezo wa Muhimbili kupanua wigo wake wa kutoa huduma za upasuaji kwa njia ya matundu madogo.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Macho MNH Upanga, Dkt. Joachim Kilemile amesema upasuaji huu ni tofauti na uliokuwa unatumika awali ambapo mgonjwa alikuwa anapasuliwa sehemu kubwa ili kuweza kutoa mtoto wa jicho.

“Upasuaji huu ni wa kisasa zaidi mgonjwa atapasuliwa sehemu ndogo tofauti na ilivyokuwa ikifanyika awali na kwamba katika Hospitali za Umma Muhimbili ni hospitali pekee ambayo inatoa huduma hii,”amesema Dkt. Kilemile.

Akizungumzia faida za upasuaji huu Dkt. Kilemile amesema unafaida nyingi kwakuwa mgonjwa atapona kwa muda mfupi na kuendelea na shughuli zake kama kawaida.

“Mgonjwa atahudumiwa na kuruhusiwa siku hiyo hiyo kurejea nyumbani, atapona kwa muda mfupi na kuweza kuendelea na ratiba zake za kila siku ambapo awali mgonjwa alikuwa akifanyiwa upasuaji inamchukua zaidi ya wiki moja kupona na kurudi katika hali yake,”amefafanua Dkt. Kilemile.

Hivyo Dkt. Kilemile ametoa wito kwa wagonjwa wote wenye changamoto ya mtoto wa jicho kufika Muhimbili Upanga kwa ajili ya kupata matibabu hayo. Kwa maelezo zaidi na kuweka miadi (appointment) unaweza kuwasiliana kupitia namba za simu: 0713-209056/ 0758 261 493 / 0713 091 664.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news