Musoma Vijijini waanza kujenga maabara ya sayansi Mtiro Sekondari

NA FRESHA KINASA

SHULE ya Sekondari Mtiro ya Kata ya Bukumu yenye Vijiji vinne vya Bukumi, Buira, Buraga na Busekera iliyoko katika Jimbo la Musoma Vijijini Mkoani Mara ambayo ilifunguliwa Mwaka 2006, imeanza ujenzi wa maabara za masomo matatu ya Fizikia, Kemia na Baiolojia.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Novemba 6, 2023 imebainisha hayo, ambapo ujenzi huo ukilenga kuhakikisha wanafunzi wa shule hiyo wanasoma masomo ya Sayansi ili kuwaandaa kuja kutoa mchango wao katika Taifa katika maendeleo ya nyanja mbalimbali.

Ujenzi wa maabara za masomo ya Sayansi katika Jimbo la Musoma Vijijini zinachagizwa na jitihada za Mbunge wa Jimbo hilo Prof. Sospeter Muhongo ambaye amekuwa akiendesha harambee jimboni humo ili kuchangia ujenzi wa maabara katika shule mbalimbali za Sekondari jimboni mwake akishirikiana na Wananchi, Serikali pamoja na wadau.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa "Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo, anaendelea kushawishi na kuhimiza wananchi kushirikiana na serikali yetu kuharakisha ujenzi na uboreshaji wa maabara tatu za masomo ya sayansi kwenye kila sekondari iliyoko Musoma Vijijini ambayo ni Fizikia, Kemia na Baiolojia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo imeeleza kuwa "Mtiro Sekondari haina maabara hata moja, kwa hiyo wanafunzi wake hawavutiwi kuchagua kusoma masomo ya sayansi. Vilevile, ufaulu wa masomo ya sayansi ni mdogo sana,"

"Matatizo haya mawili (mvuto wa kusoma sayansi & ufaulu mbaya wa masomo haya) yanadhoofisha uwepo wa wanasayansi wengi na mahiri nchini mwetu.

HALI YA MASOMO YA SAYANSI MTIRO SEKONDARI.

"Hali ya Masomo ya Sayansi Mtiro Sekondari kwa Mwaka jana (2022) ni Wanafunzi 139 walimaliza Form IV. na Mwanafunzi mmoja (1) tu alienda Form V kusoma masomo ya sayansi. Kwa Mwaka huu (2023), Wanafunzi watakaomaliza Form IV ni 123,Wanafunzi wanaosoma Fizikia ni 21 na Wanafunzi wanaosoma Kemia ni 26,"

HATUA ILIYOCHUKULIWA.

"Tumeamua kujenga maabara tatu za masomo ya sayansi kuhakikisha wanafunzi wanapenda kusoma masomo hayo kwa ufanisi ambapo Michango ya ujenzi imeanza kutolewa kama ifuatavyo:

(i) Michango kutoka kwa wananchi:
Tsh 7,989,100
(ii) Michango kutoka kwa walimu na wanafunzi
Usombaji wa maji, moramu na mawe
vyenye thamani ya Tsh 3,640,000
(iii) Mbunge wa Jimbo amechangia:
Saruji Mifuko 125
(iv) Mfuko wa Jimbo umechangia:
Saruji Mifuko 200 & Nondo 29

Mtiro Sekondari inaomba mchango wako. Tafadhali changia moja kwa moja kupitia Akaunti ya Benki ya Shule:
MTIRO SECONDARY
NMB
A/C NO. 30301200299
Tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwa mchango wako utakaoipatia Mtiro Sekondari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news