Musoma Vijijini waguswa na ushauri wa Prof.Muhongo kwa Serikali

NA FRESHA KINASA

WANANCHI wa Jimbo la Musoma Vijiji mkoani Mara wamefurahishwa na ushauri alioutoa Mbunge wao, Prof.Sospeter Muhongo kwa serikali kuhusu mipango ya maendeleo kuwa na shabaha ya kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa pamoja na kushughulikia mahitaji muhimu ya kila siku ya Watanzania.

Ambapo mahitaji hayo ni pamoja na chakula, maji, umeme na matibabu ambayo Watanzania kila siku wanayahitaji kwa ajili ya maisha yao.

Prof. Muhongo alitoa ushauri huo Novemba 9, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia mapendekezo ya Mpango wa Taifa kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025.

Katika ushauri wake kwa Serikali Prof. Muhongo pia alisema kuwa uchumi wa nchi unapswa ukue kwa Kasi ya asilimia 8 -10, ili kupunguza umaskini kwa kasi kubwa.

Novemba 17, 2023 baadhi ya wananchi wa Musoma Vijijini wakizungumza na DIRAMAKINI wamesema, ushauri wake ni mzuri kwani unalenga kuhakikisha mahitaji ambayo watanzania wengi kwa kila siku wanayapata na ni vyema serikali ikajitahidi kuhakikisha mahitaji hayo yanakuwa thabiti ili kupunguza umaskini.

Juma Mafuru Mkazi wa Nyegina amesema kuwa, "Kwa mfano suala la matibabu likiimarishwa na Serikali hakuna mtanzania ambaye atapata shida, akiugua atajua kuna dawa katika vituo vya kutolea huduma na pia kuna madaktari na huduma zote muhimu zipo.

"Kwa hiyo, ni muhimu Serikali ikazidi kuimarisha eneo hilo hili katika mipango yake kama ambavyo alishauri Prof.Muhongo,"amesema Mafuru.

Jenepher Maira mkazi Bugwema amesema kuwa, "tunaona Serikali yetu inajitahidi kuboresha huduma ya maji safi na salama vijijini na mijini, hatua hii ni njema.

"Lakini pia juhudi ziongezewe kusudi kila mtanzania apate maji karibu na makazi yake tena kwa uteshelevu unaotakiwa kitaalamu.

"Huduma ya maji ikiwa imara Watanzania watatumia muda wao mwingi hasa kina mama kufanya uzalishaji na maendeleo nilifurahishwa sana na ushauri wa Mbunge wangu,"amesema Jenepher.

"Prof. Muhongo alishauri uchumi wetu ili ukue kati ya asilimia 8-10 ni vyema Serikali ikawekeza kwenye gesi asilia na madini mengine ambayo yana thamani kubwa duniani.

"Mimi binafsi nilifurahi. Serikali yetu ni vyema iuchukue na kuufanyia kazi kwa vitendo katika kupiga hatua kiuchumi kama mataifa mengine ambayo yamefanikiwa,"amesema Bwire Laurent Mkazi wa Nyakatende.

"Wapo baadhi ya Watanzania hasa maeneo ya vijijini, mahitaji muhimu kwao ni changamoto bado hawajafanikiwa kuyapata inavyopaswa.

"Ni muhimu serikali katika mipango yake sasa ikajielekeza kuimarisha huko na pia kwenye Kilimo, Uvuvi, Ufugaji ikaimarisha umaskini utapungua kama ambavyo ushauri alivyoutoa," amesema Jefta Masegesa mkazi wa Bukumi.

"Nilimsikiliza Prof. Muhongo katika ushauri wake aligusia mipango kuweka mkazo katika suala la utafiti, hapa aligusa penyewe kabisa, naomba Serikali katika mipango yake itazame eneo hili ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu na ukuzaji wa uchumi.

"Bila utafiti ni ngumu kupiga hatua na kupata ufumbuzi wa kitaalamu wa mambo mbalimbali iwe changamoto, suluhisho au mikakati ya kuchukua dhidi ya jambo fulani iwe madini wapi yalipo au maji yachimbwe eneo gani,"alisema Costanza Juma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news