Nafuu inakuja kwa mashirika ya umma nchini

NA GODFREY NNKO

OFISI ya Msajili wa Hazina imesema kuwa,Muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Mwaka 2023 unapendekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma nchini.

Muswada huo ambao ulisomwa kwa mara ya kwanza Novemba 10,2023 bungeni jijini Dodoma pia unalenga kuweka masharti ya uwekezaji wa umma, mfumo wa kitaasisi kwa ajili ya uratibu wa usimamizi wa uwekezaji wa umma na usimamizi wa mashirika ya umma pamoja na kufuta Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina nchini (TR).
Hayo yamesemwa leo Novemba 28, 2023 na Msajili wa Hazina, Nehemiah Kyando Mchechu katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya ofisi hiyo jijini Dar es Salaam.

Amesema,mfuko huo utakuwa unagharamia uwekezaji unaofanywa na Serikali ikiwemo kuwezesha mashirika ya umma yenye ukosefu wa mitaji katika fursa za uwekezaji zenye tija pamoja na kugharamia uendeshaji wa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma.

“Lengo la kutaka kuanzisha Mfuko wa Uwekezaji wa Umma ni ili sisi tuwe na uwezo wa kuyapa mitaji mashirika na taasisi tunazozisimamia.”

Amesema, miongoni mwa faida ambazo wanatarajia kuzipata kwa kuanzishwa mfuko huo ni kuiwezesha Serikali kufanya uwekezaji wa kimkakati kwa wakati.

Vile vile, kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa mashirika na taasisi za umma ambazo zipo chini ya ofisi hiyo.

Mchechu amesema, faida nyingine ni kuyaokoa mashirika ambayo bila mfuko yanaweza kuanguka kutokana na hali mbaya ya kiuchumi hususani kwa kukosa mitaji.

Sambamba na kuyawezesha mashirika ya umma kuweza kustahimili ushindani ndani na nje ya nchi.

Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa ofisi inayojitegemea kimuundo.

Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC), ofisi ilikabidhiwa majukumu ya shirika hilo ambapo kwa sasa wanaendelea na maboresho makubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news