DAR ES SALAAM-Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), leo Novemba 23,2023 limetangaza rasmi matokeo ya mtihani wa darasa la saba huku ufaulu wa jumla ukiwa umeongezeka kwa asilimia 0.96.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es salaam na Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matokeo ya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE).
Ni mtihani uliofanyika Septemba 2023, ambapo amesema kuwa, jumla ya watahiniwa 1,092,960 sawa na asilimia 80.58 ya watahiniwa 1,356,296 wamefaulu ambapo wamepata Daraja A, B na C huku wavulana wakiwa ni asilimia 80.59 na wasichana asilimia 80.59.
“Ubora wa ufaulu kwa wasichana umeongezeka ksa kiasi kikubwa hadi asilimia 80.58 ikilinganishwa na asilimia 79.91 kwa mwaka 2022 huku ufaulu wa wavulana ukiwa umeongezeka kwa asilimia 80.59 ikilinganishwa na asilimia 80.41 kwa mwaka 2022, kiujumla niseme tu ufaulu wa wavulana na wasichana kwa mwaka huu 2023 unafanana,” amesema Dkt. Mohamed.
Wakati huo huo, NECTA imezuia matokeo ya watahiniwa 360 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mitihani kwa masomo yote ambapo watahiniwa hao wamepewa fursa ya kurudia mitihani hiyo mwaka 2024 kwa mujibu wa kifungu cha 32(1) cha Kanuni za Mitihani.
Ameongeza kuwa pia Baraza limefuta matokeo yote ya watahiniwa 31 kutoka shule 12 nchi nzima kwa tuhuma za kufanya udanganyifu katika mtihani.
Aidha, baraza limezifungia shule mbili kuwa vituo cha kufanya mtihani kwa kupanga kufanya udanganyifu katika mtihani, vituo hivyo ni Twiboki yenye namba ya usajili (PS0904095) na Graiyaki yenye namba (PS0904122) zote za Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani wa Mara.
Pia, Baraza la Mitihani lieziandikia barua za onyo vituo vya mitihani vinne ambavyo vilijaribu kujihusisha na vitendo vya udanganyifu katika mtihani.
“Tumeviandikia barua za onyo vituo vinne ambavyo ni Mother of Mercy (PS0203133), ST Mary’s Mbezi Beach (PS0203088) ambapo zipo Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam, Charm Modern (PS0103111) Halmashauri ya Karatu Mkoa wa Arusha pamoja na Morotonga (PS0904042) cha Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara.
“Vituo hivi vitakuwa chini ya uangalizi wa Baraza la Mitihani mpaka litakapojiridhisha kuwa ni vituo salama kwa uendeshaji wa mitihani ya Taifa,” amesema Dkt.Mohamed.
Katibu Mtendaji huyo wa NECTA, amesema kuwa jumla ya watahiniwa 1,397,293 walisajiliwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kati yao wasichana ni 742,690 na wavulana 654,603 huku wenye mahitaji maalumu walikua 4,599 sawa na asilimia 0.33.
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza Matokeo ya Darasa la Saba 2023