Ofisi ya Msajili wa Hazina yadhamiria kupaisha zaidi mapato ya Serikali,Mchechu aweka bayana yajayo

NA GODFREY NNKO

MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Kyando Mchechu amesema, maboresho makubwa yanayoendelea kupitia ofisi hiyo kwa taasisi na mashirika ya umma inayoyasimamia yanalenga kuongeza ufanisi na mapato ya Serikali ili yaweze kuendesha shughuli za maendeleo.

Ameyasema hayo leo Novemba 28, 2023 katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya ofisi hiyo jijini Dar es Salaam.

Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia jumla ya taasisi 298 huku kati ya hizo yakiwemo mashirika ya umma na wakala wa Serikali 248 na kampuni zilizopo ndani na nje ya nchi 50.

Aidha, kati ya hizo 213 zinajihusisha na utoaji huduma, wakati kampuni 50 Serikali ina hisa chache kati ya hizo 40 zipo ndani ya nchi na 10 nje ya nchi.

Katika hatua nyingine,taasisi, mashirika ya umma na wakala wa Serikali 35 zinafanya biashara huku kampuni 50 nazo zikiwa zinafanya biashara.

“Hizi taasisi zikiwa dhaifu hata TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) haipati mapato, kwa hiyo tunaendelea na maboresho makubwa ili ziweze kuwa na tija zaidi.”

Amesema, mabadiliko ya sheria ya ofisi hiyo ambayo yanatarajiwa hivi karibuni yakikamilika, kuna mageuzi makubwa ambayo yanatarajiwa katika ofisi hiyo kuanzia muundo mpya, jina na ujio wa mfuko wa uwekezaji.

Muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Mwaka 2023 unapendekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma nchini.

Muswada huo ambao ulisomwa kwa mara ya kwanza Novemba 10,2023 bungeni jijini Dodoma pia unalenga kuweka masharti ya uwekezaji wa umma, mfumo wa kitaasisi kwa ajili ya uratibu wa usimamizi wa uwekezaji wa umma.

Sambamba na usimamizi wa mashirika ya umma pamoja kufuta Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina nchini (TR).

Safari inaendelea

"Safari yetu ya mabadiliko bado tunaendelea kuifanya, tumewaandaa wakuu wa taasisi mbalimbali na wenyeviti. Mimi nimeingia TR nimekuta hizo reforms Mheshimiwa Rais ameanza kuwasukuma, kwa hiyo tunaendelea nazo na tunahakikisha zinafanyika.

"Tumeshaongea na wakuu wa taasisi tukawaambia hizo reforms ni real ndio interests ya nchi kuona kwamba zinafanyika, katika historia shirika lilianza mwaka 1959 na wakati huo lilikuwa chini ya ukoloni kuhakikisha wanasimamia mambo ya kiuwekezaji vizuri mwaka 1967 TR ikawa weakened kulikuwa na kamati ya Rais ya kusimamia mashirika ya umma baadaye busara zikasema mwaka 2002 hebu tuirudishe baada ya mabadiliko ya uchumi tuliyokuwa tunaenda nayo.

"2010 sheria ikaboreshwa na kuipa nguvu 2014, kukawa na mabadiliko madogo na sasa 2023 tunajaribu tena kufanyia reforms hii, tunataka kuchukua maono marefu ya mbele tunakoendelea ni muhimu sana kwa uchumi ili uweze kwenda.

"Tuna sheria mama, Sheria ya Msajili wa Hazina (The Treasury Registrar (Powers and Functions) Act, Cap. 370;), sheria/ instrument anzilishi za taasisi mbalimbali.
“Sheria ya Mashirika ya Umma (The Public Corporation Act, Cap. 257), Sheria ya Fedha za Umma (The Public Finance Act, Cap 348), Sheria ya Mikopo na Dhamana (The Government Loans, Guarantee and Grants Act, Cap 134), Sheria ya National Bank of Commerce (Reorganization and Vesting of Assets and Liabilities) Cap 404, Sheria ya Utumishi wa Umma (Public Service Act, Cap 298) na Sheria ya Bajeti na Kanuni zake, Cap 439

“Sababu Serikali Kuu bajeti zake zinapitishwa na Bunge na taasisi za umma bajeti zao zote zinapitishwa na Msajili wa Hazina. Sisi tunapitisha bajeti zao na mikakati yao.

"Tuna majukumu ya Ofisi ya TR ambayo ni pamoja na kumiliki au kutunza na kusimamia hizi taasisi, pili kuishauri Serikali juu ya uwekezaji,kusimamia ubinafisishaji na taasisi tunazozisimamia ni 298 na zilizoongezeka ni sekta za madini nane na hivyo kufikia 306.

Ongezeko

"Tumepanga ndani ya miezi sita tuweze kuongeza taasisi kama 50 au 70 kwa sababu tuna Sheria ya Madini ya mwaka 2017 inataka kila kampuni ya madini itakayopewa leseni kubwa asilimia 16 imilikiwe na Serikali kupitia Ofisi ya TR, yote hiyo inahitaji mabadiliko ya mindset za watu, wakuu wa taasisi, wenyeviti wa taasisi, sheria hadi fikra ili hizo rasilimali ziweze kutukomboa.

"Katika mashirika hayo 248 majority yote yako ndani ya nchi, lakini 50 tuna hisa chache 40 yaliyoko ndani ya nchi, 10 nje ya nchi ni katika geographical coverages kwa maana ya umiliki.

“213 yanajihusisha na utoaji wa huduma na 35 ya biashara. Ukija kwenye 248 yamegawanyika katika sekta mbalimbali kuna maji na mabonde, elimu ya juu na mafunzo, utafiti, taaluma, mazao, kina Muhimbili wamo humo ndani.

"Sasa katika haya, yanayotoa huduma ni asilimia 86 yako 213, na ya biashara yako 14 japo hizi takwimu zitaongezeka. Tunataka watu wabadilike wanapopata hizi kampuni mengi yanatakiwa yatoke kwenye huduma yasitegemee ruzuku ya Serikali.

"Katika kampuni chache za kisekta 50, lakini nimesema kwenye madini zinakuja kuwa 58 kwa makampuni ya wazalishaji yako 16 kwa mwaka ujao yatakuwa yametoka hapa kwa sababu tunataka kufanya uchambuzi.
"Katika huduma za kifedha yaliyoko ndani ya nchi makampuni sita ambako tuna hisa na ya nje ya nchi yote 10 mashirika ya kifedha huko tuna-shares na zinashikiliwa na Msajili wa Hazina.

"Kwenye haya mashirika ya nje tunaweza kuongeza shares kwa sababu za kimkakati zaidi, lazima shares zetu zikuwe kwenye madini yako nane kwa sasa tunapanga kuongeza zaidi tuna PUMA asilimia 50, TAZAMA asilimia 33 na TIPA asilimia 50.

Mapato makubwa

"Unapomiliki kwa asilimia 50 maana yake serikali ina stake kubwa, sasa tunajaribu kuimarisha aina ya watu wanaosimamia kwenye hizi bodi ili interests za serikali ziweze kuwa imara Airtel ni asilimia 49, na usafirishaji tuna makampuni matatu.

"Kwenye muundo wa serikali na uingizaji wa fedha ni kwamba fedha zinazalishwa kwenye taasisi, huku ndiko utakuta TANAPA na kadhalika. Na njia pekee lazima tufanye reforms kwenye taasisi kwa sababu ukifanya reforms mapato yatakuwa makubwa.

"Pia kukiwa na nidhamu mapato yataongezeka lazima kutambua nani mzalishaji, na nani pia ambaye ni mtumiaji, lakini ukweli ni kwamba mzalishaji ni taasisi. Wizara wao ni watumiaji na mzalishaji ni taasisi leo hii mapato si makubwa ukilinganisha na matumizi.

"Tunahitaji reforms ili tuwe sawa vingenevyo tutajikuta tunakopa kutekeleza miradi ya maendeleo, kumbe tulitakiwa kufanyia reforms. Na Mheshimiwa Rais amesema, anataka reforms nasi kama wasimamizi aliotupa madaraka hayo lazima tumsaidie kwenda mbele zaidi."

Thamani ya Uwekezaji

Katika hatua nyingine,Msajili wa Hazina Mchechu amebainisha kuwa, thamani ya uwekezaji wa Serikali katika taasisi, mashirika na wakala za Serikali imeendelea kupanda mwaka hadi mwaka.

Amesema, kwa mwaka 2019/20 thamani ya taasisi, mashirika ya umma na wakala za Serikali ambazo zilikuwa 237 ilikuwa shilingi trilioni 62.98 huku kampuni ambazo Serikali ina hisa chache kwa mwaka huo ambazo zilikuwa 50 thamani yake ilikuwa shilingi trilioni 2.21.

Aidha, katika mwaka huo huo wa 2019/20 jumla ya uwekezaji wa Serikali katika taasisi 287 thamani ya uwekezaji ilikuwa shilingi trilioni 65.19.

Kwa mwaka 2020/21 idadi ya taasisi, mashirika ya umma na wakala za Serikali ilikuwa 237 ambapo thamani ya uwekezaji ilifikia shilingi trilioni 65.43 huku kwa upande wa kapuni yenye hisa chache 50 thamani ya uwekezaji ikifikia shilingi trilioni 2.52 ambapo katika jumla ya taasisi 287 thamani ya uwekezaji wa Serikali ilikuwa shilingi trilioni 67.95.

Wakati huo huo, kwa mwaka 2021/22 idadi ya taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali zilikuwa 248 ambapo thamani ya uwekezaji ilifikia shilingi trilioni 70.80 huku kampuni ambazo Serikali ina hisa chache thamani ya uwekezaji ikiwa ni shilingi trilioni 2.56 ambapo jumla ya taasisi 298 katika mwaka huo thamani ya uwekezaji ilifikia shilingi trilioni 73.36.

Katika mwaka 2022/23 jumla ya taasisi, mashirika ya umma na wakala wa Serikali 248 thamani ya uwekezaji ilikuwa shilingi trilioni 72.97 huku kampuni ambazo Serikali ina hisa chache zikiwa 50 ambapo thamani ya uwekezaji ni shilingi trilioni 2.82 ambapo jumla ya taasisi zipo 298 huku thamani ya uwekezaji ikiwa shilingi trilioni 75.79.

Mwelekeo

Mchechu amesema, mwelekeo mpya wa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kubadili jina na kuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (Public Investments Authority-PIA).

Pia amesema, katika muundo huo mpya pia wataanzisha Mfuko wa Uwekezaji wa Umma (Public Investment Fund ) ambao kazi yake ni kuzisaidia taasisi kuimarisha mtaji.

“Katika mapendekezo ya muundo mpya, Ofisi ya Msajili wa Hazina sasa itakuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (Public Investment Authority-PIA) lengo ni kuhakisi majukumu na mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa duniani.”

Mbali na hayo, Mchechu amesema, ili kuongeza ufanisi katika taasisi hizo mambo manne lazima yazingatiwe ambayo ni kuwa na uongzi bora, taasisi kuwa huru, kuwa na rasilimali za kutosha.

Sambamba na kupima utendaji huku akisema wametengeneza vigezo vipya, zamani kulikuwa na vigezo ambavyo havijazingatia sekta.

“Unapomsimamia mfano TANESCO au Muhimbili hawa kazi ni tofauti na hadi vigezo vyao. Hivyo ni lazima vigezo viendane na sekta husika na asili ya taasisi inavyofanya kazi yake.”

Alirejea kauli yake kuwa mabadiliko katika taasisi za umma hayaepukiki na kuwataka watendaji kujipanga na kuwa tayari kwa mabadiliko hayo ambayo tayari yameanza.

“Tumeshaanza, mabadiliko mtaona tunachanganya damu changa na wale wakongwe, na inapobidi tunachukua mtendaji kutoka sekta binafsi kuja kuongoza taasisi ya umma.

"Mtarajio ya Mheshimiwa Rais ni kuona taasisi hususani zile za kibiashara zinatengeneza faida zitakazozalishwa na kuingizwa serikalini au kujiendesha pasipo utegemezi wa Serikali Kuu, hivyo ni lazima kuwepo mabadiliko ili kuongeza tija na ufanisi.

"Muundo wa mapato ya Serikali, tumekua kutoka shilingi bilioni 753 hadi trilioni moja kwenye taasisi za umma, tulikuwa bilioni 695 mwaka 2020/21 tulikuwa na athari za COVID-19 lakini 2021/2022 imeanza ukiangalia 2022/2023 tumefika bilioni 777.

"Kwa kweli si kitu kizuri tulikuwa na taasisi 236 katika taasisi 248 ambazo zilichangia leo hii taasisi zilizochangia ni 108 kwa hiyo taasisi zilizochangia zimeshuka kwa asilimia 100. Lakini taarifa njema ni kwamba zimeshuka kwa asilimia 100, lakini mapato yameongezeka kwa asilimia 100.

"Sisi changamoto yetu hapa lazima tuangalie walioshuka sababu imetokana na nini na pia kuwarudisha katika mstari kwa sababu wamepewa kusimamia kwa manufaa ya wananchi nasi TR lazima tusimamie jukumu hili kwa dhamana ya watanzania wakienda walikuwa 200 wakashuka mpaka 136 hatujaelewa labda COVID-19.

"Pili tunataka kujua kwa nini wamepungua na pia kuona hawa wanaochangia ndicho ambacho kweli kwa wakati huu? Katika kutekeleza mambo haya lazima tuwe na muunganiko na ushirikiano wa pamoja ndani ya ofisi.

"Wastani wa mchango wa taasisi za binafsi ni mkubwa sana, kumbe unaweza kusema kwamba kuwa na taasisi zenye combination ya Serikali na binafsi ndani yake ni vizuri sana. Ukiangalia benki ambazo tunamiliki kwa asilimia 100 tuna benki kama tatu, lakini zote hizi hakuna iliyofika pesa toka NMB.
"Kumbe kung'ang'ania uwe na asilimia 100 haikusaidii sana, tunachohitaji ni tufanye reforms hizi kwa ajili ya kuleta mabadiliko bora katika kuinua uchumi na maendeleo ya taifa letu,”amefafanua kwa kina Msajili wa Hazina, Nehemiah Kyando Mchechu.

TR ni nini?

Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa ofisi inayojitegemea kimuundo.

Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC), ofisi ilikabidhiwa majukumu ya shirika hilo ambapo kwa sasa wanaendelea na mageuzi makubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news