PURA:Kuna mafanikio makubwa sekta ya mafuta na gesi nchini

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema, tangu kuanza kwa shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia mwanzoni mwa miaka ya 1950,Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa ufanisi ili kuwezesha upatikanaji wa rasilimali hiyo muhimu kwa maendeleo endelevu ya nchi.

Hayo yamesemwa leo Novemba 6, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Mhandisi Charles Sangaweni katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mhandisi Sangaweni amesema, kati ya hatua muhimu ambazo Serikali imeendelea kuchukuwa ni kuimarisha mifumo ya kisheria, kitaasisi na udhibiti wa shughuli hizo.

"Hii ilipelekea kuwepo kwa Sheria ya Petroli ya mwaka 1980,mikataba kifani ya ugawanaji mapato (Model PSA) kwa nyakati mbalimbali,kanuni na miongozo mbalimbali na Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, ambayo kutokana na sheria hii Taasisi ya PURA ilianzishwa."amesema Mhandisi Sangaweni.

Amefafanua kuwa,PURA ilianzishwa mwaka 2015 kupitia Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 ambapo ilianza shughuli zake rasmi mwezi Februari 2016 kupitia Kamati Maalumu iliyoundwa na watumishi kutoka iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini na kutoka TPDC.

Mhandisi Sangaweni amesema, kamati hiyo ilikuwa ikitekeleza majukumu ya kisheria ya taasisi huku ikiendelea na maandalizi ya nyaraka mbalimbali za kuwezesha taasisi kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

"Kwa sasa, PURA ina miaka nane na inatekeleza majukumu yake kama yalivyoaisnishwa kwenye Sheria ya Patroli 2015, kifungu cha 12."

Amesema, majukumu hayo yamegawanyika katika makundi makuu matatu ambayo ni pamoja na kuishauri Serikali kupitia Waziri mwenye dhamana ya nishati hususani mafuta na gesi juu ya masuala yanayohusu shughuli za mkondo wa juu wa petroli.

Pia, kudhibiti na kusimamia shughuli zote za mkondo wa juu wa petroli na kusimamia miradi ya kubadili gesi kuwa katika hali ya kimiminika (Liquified Natural Gas-LNG).

Amesema, hapo awali shughuli hizo zilikuwa zikitekelezwa na TPDC baada ya kukasimishwa na Kamishna wa Mafuta na Gesi.
Afisa Uhusiano Mwandamizi, Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), Bw. Sabato Kosuri, akiongoza kikao hicho.

"Shughuli hizi za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi nchini zinatekelezwa kwa kupitia mikataba ya ugawanaji mapato yaani Production Sharing Agreements-PSA, ambapo kampuni kubwa za mafuta duniani huingia mkataba na Serikari na kuwekeza katika nyanja hiyo.

"Kwa sasa tuna kampuni zipatazo nane ambapo mikataba iliyopo ni 11 kati ya mikataba hiyo, mitatu ipo katika hatua ya uzalishaji na uendelezaji wa gesi asilia wakati iliyobaki bado ipo katika hatua ya utafutaji."

Mafanikio

Amesema, miongoni ma mafanikio yaliyopatikana tangu shughuli hizo zianze hapa nchini ni jumla ya visima vya utafutaji wa mafuta vilivyochimbwa ni 96 ambapo kati ya visima hivyo, visima 59 vipo maeneo ya nchi kavu na visima 37 vipo maeneo ya baharini.

Mhandisi Sangaweni amesema,mafanikio mengine ni kugundulika kwa gesi asilia katika visima 44 kati ya visima 96 vilivyochimbwa.

Amesema, kati ya visima hivyo 44 vilivyogundulika gesi, visima 16 vilichimbwa nchi kavu na 28 vilichimbwa baharini vya ugunduzi, visima 16 vipo nchi kavu na visima 28 vipo baharini.

"Gesi asilia imegunduliwa katika maeneo ya Songo Songo mwaka 1974, Mnazi bay mwaka 1982, Mkuranga mwaka 2007, Kiliwani Kaskazini mwaka 2008, Ntorya mwaka 2012, Ruvu mwaka 2016 na Kina Kirefu cha Bahari kuanzia miaka ya 2010.

"Gesi asilia iliyogunduliwa nchi kavu na kina kirefu cha bahari ni Futi za Ujazo Trilioni 57.54 (nchi kavu Trilioni 10.41 na Baharini Trilioni 47.13),"amebainisha Mkurugenzi huyo.

Pia amesema, uzalishaji wa gesi asilia ulianza mwaka 2004 kwa upande wa Songo Songo na mwaka 2006 kwa upande wa Mnazi Bay.

Amesema, ugunduzi huo na uzalishaji wa gesi asilia iliyogunduliwa umewezesha kuanza ikutumikea kwa gesi asilia kama chanzo cha nishati maeneo mbalimbali, hususani kwa kuzalisha umeme, kutumika viwandani, majumbani na kwenye magari.

"Hadi sasa kiasi cha gesi kinachozalishwa kinachangia karibu asilimia 70 ya umeme unaozalishwa hapa nchini,"amesema.

Vile vile amesema, hadi sasa kwa kupitia usimamizi wa PURA maeneo ambayo yamefanyiwa tafiti ni kiasi cha kilomita za mraba 534,000 ambapo kati ya hizo kilomita za mraba 394,000 ni nchi kavu na kilomita 140,000 baharini.

Hata hivyo, amesema maeneo mengi yameshafanyiwa tafiti za awali ambapo data, taarifa na takwimu zake zipo kwenye gravity/magnetic na 2D seismic.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Sangaweni amesema,hadi sasa nchi yetu ina Mikataba ya Utafutaji, Uendelezaji na Uzalishaji Mafuta na Gesi Asilia (PSA) ipatayo 11, kati ya hiyo mitatu ipo katika hatua ya uzalishaji wakati mikataba nane ipo katika hatua mbalimbali za utafutaji.

"Mafanikio mengine ni kuimarika kwa shughuli za kaguzi za gharama na matumizi katika Mikataba ya PSA ikiwemo kuimarika kwa mifumo ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaasisi nchini, ambapo kumekuwa na Sheria ya Peroli ya mwaka 1980,

"Sera ya Nishati ya mwaka 2015, Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, na Sheria ya Udhibiti wa Mapato ya Mafuta na Gesi ya mwaka 2015. Mifumo ambayo imewezesha kuanzishwa kwa PURA na EWURA,"amesema Mkurugenzi huyo.

Awamu ya Sita

Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangaweni amesema, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, mamlaka hiyo katika kutekeleza majukumu yake ya kuishauri Serikali kuhusu masuala ya mkondo wa juu wa petroli, udhibiti na usimamizi wa shughuli hizo imewezesha kupatikana kwa mafanikio mbalimbali.

Amesema, mafanikio hayo ni pamoja na kuimarika kwa shughuli za kaguzi za gharama katika Mikataba ya Uzalishaji na Ugawanaji Mapato (PSA Audit), iliyopelekea kuokoa fedha kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 189 kwa kurudishwa kwenye mfuko wa ugawanaji wa mapato kati ya Serikali na waendeshaji wa vitalu husika.

Pia, kuimarika na kuongezeka kwa ushiriki wa wazawa katika miradi ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini. Amesema, wastani wa ushiriki wa wazawa katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli kupitia ajira ni asilimia 85.

Vile vile amesema, wameshauri Serikali na kufanikisha kutolewa kwa ongezwa kwa muda wa leseni ya utafutaji awamu ya pili katika Kitalu cha Tanga, Ruvu, Mtwara na vitalu Namba 1, 2 na 4 vilivyopo baharini.

"Mafanikio mengine ni kushauri Serikali na kufanikisha utiaji saini kwa mkataba wa nyongeza wa uzalishaji na ugawanaji mapato ya gesi iliyogundulika Ntorya katika kitalu cha Ruvuma.

"Mkataba huo ambao utekelezaji wake utawezesha kuendeleza gesi asilia ya kitalu hicho ya takribani futi za ujazo Trilioni 1.6 ulisainiwa baina ya Wizara ya Nishati, TPDC na Kampuni ya ARA (Oman)."

Aidha, wameishauri Serikali na kufanikisha kutolewa kwa leseni ya utafutaji awamu ya pili katika Kitalu cha Tanga ikiwemo kutoa kibali cha utafutaji wa awali wa mafuta na gesi asilia katika Kitalu cha Eyasi Wembere kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Mkurugenzi Mkuu huyo ametaja mafanikio mengine kuwa, ni kuanza kwa kazi ya kufanikisha durusu ya Mkataba Kifani wa Uzalishaji na Ugawanaji wa Mapato (MPSA) kwa lengo la kuhuisha ili kuendana na mazingira ya uwekezaji wa sasa katika sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia.

Sambamba na kukamilika kwa mapitio ya MPSA ikiwa ni hatua muhimu kuelekea zoezi la kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia.

Amesema, pia kuna ongezeko la wastani wa uzalishaji wa gesi asilia kufikia futi za ujazo bilioni 53.19 kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Februari 2023 ukilinganisha na futi za ujazo bilioni 46.96 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2021/22, sawa na ongezeko la asilimia 14.

Nyingine ni kukamilika kwa maandalizi ya rasimu ya Ramani ya Kidijitali (Interactive Digital Petroleum Reference Map) kwenye Mfumo wa Taarifa wa Kijiografia (Geographical Information System-GIS) inayotoa taarifa za vitalu vya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini,

Amesema, pia PURA wameweza kuongeza idadi ya watumishi wake ambapo Serikali ilitoa kibali na kufanikiwa kuajiri jumla ya watumishi wapya 22, kuongoza na kushiriki kikamilifu majadiliano ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa uchakataji na usindikaji wa gesi asilia kuwa kimiminika wa LNG.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news