Rais Dkt.Samia azidi kuifungua nchi kiuchumi, Dkt.Kijaji asema Desemba kuna jambo kubwa

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt.Ashatu Kijaji amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kufungua mipaka ya nchi hatua ambayo imewezesha mazingira ya biashara ndani na nje kuimarika zaidi.
Dkt.Kijaji ameyabainisha hayo leo Novemba 29, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia kuhusiana na maandalizi ya Kongamano la Wanawake chini ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ambalo linatarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia Desemba 6 hadi 8, 2023.

“Tulipokutana mara ya kwanza, tukawajulisha kuhusu fursa zilizopo na tukawaelezea angalau tuwe na kampuni 10 ambazo tunaweza kuanza nazo.

“Leo tunapoongea hata miezi sita haijafika, tayari tuna kampuni 18 ambazo zinapeleka bidhaa zao kwenye Eneo Huru la Biashara Afrika, na tumepeleka siyo kwa nchi moja,kila kampuni tumeweza kuwaunganisha na makampuni ya nje katika nchi ambazo wanatakiwa kupeleka na tumefanikiwa kufikia nchi ya Algeria.

“Kundi lingine limepeleka nchini Morocco, na kundi lingine limeenda nchini Misri,kampuni nyingine imepeleka nchini Ghana, na tumepeleka pia nchini Nigeria, kwa hiyo tayari bidhaa zetu zimefika katika maeneo hayo kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika.

“Kwa hiyo nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufungua mipaka ya Taifa letu, kwa kusaini na kuridhia Mkataba Huru wa Biashara Afrika ambapo sasa bidhaa zetu zilizokuwa hazina masoko, sasa zinapata masoko.

“Kama mtakumbuka ndugu zetu, tulianza kulalamika miaka mitatu, miwili iliyopita kwamba bidhaa zetu za katani hazina masoko tena, wakaanza kung’oa mazao yale ya mkonge.

“Lakini sasa katika zao ambalo limepata biashara kubwa kwenye Eneo Huru la Biashara Afrika ni mazao yanayotokana na mkonge, mazao ya katani yamepata biashara kubwa nchini Nigeria, nchini Ghana, nchini Morocco na kupeleka haya mazao ya kutosha kwenye maeneo hayo."

Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA) ni utaratibu wa pamoja wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika unaolenga kuchochea uchumi na Biashara miongoni mwa nchi wanachama.

Lengo hilo litafikiwa kwa kufunguliana masoko ya biashara ya bidhaa na huduma kwa kuondoleana ushuru wa forodha (tariff) na kulegezeana masharti na taratibu nyingine zisizokuwa za kiushuru.

Aidha, utaratibu huo unalenga kufanya Bara la Afrika kuwa Soko Moja ambapo nchi hizo zitaweza kutangamanisha juhudi nyingine za mtangamano wa kibiashara na uchumi ambazo nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zimeshaanzisha.

Waziri Dkt.Kijaji amesema,kutokana na kongamano lililopita tayari kuna wanawake wanafanya biashara na matokeo ni mazuri.

"Ni wito wangu, wanawake waweze kuja kwa pamoja, pia ni matarjio yetu kuwa baada ya kongamano hilo tutaweza kufanya vizuri zaidi hususani kutumia soko linalotuzunguka.

"Mwaka jana wakati wa kongamano hili la kwanza ilionekana kuna changamoto kadhaa ambazo wanawake walikuwa wanakabiliana nazo, tayari wizara imefanya makongamano kadhaa kuwaunganisha wanawake wanaovusha biashara zao.

“Bado tunaona kuna umuhimu wa kufikisha elimu hiyo, hivyo ninachukua fursa hii kuwakaribisha sana wanawake wote wanaojihusisha na biashara kushiriki katika kongamano hili kwa kujisajili kupitia tovuti ya wizara."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news