Serikali imekusanya shilingi trilioni 9.06 robo ya kwanza-Waziri Mkuu

DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema katika robo ya kwanza ya mwaka 2023/2024, mapato kutoka vyanzo vyote vya ndani na nje yalifikia shilingi trilioni 9.06 sawa na asilimia 89.6 ya lengo la kipindi hicho.

“Kati ya kiasi hicho, mapato ya ndani yalikuwa shilingi trilioni 6.94 sawa na asilimia 96.2 ya lengo la kipindi hicho,” amesema.
Amesema hayo Novemba 10, 2023 wakati akitoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Januari 30, 2024.

Amesema kuwa ongezeko hilo ambalo limewezesha Taifa kuimarika kiuchumi limetokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita ikiwemo kuwezesha uwekezaji wa kimkakati katika sekta za uzalishaji, huduma za jamii na miundombinu.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuongezeka kwa mapato hayo, kunatokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kurahisisha ulipaji wa kodi.

“Pia kuimarika kwa mapato kumewezesha Serikali kuendelea kuwahudumia wananchi kupitia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa; mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere, miundombinu ya barabara, mpango wa Elimumsingi bila ada na usambazaji umeme vijijini.”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) iboreshe mwongozo wa uwekezaji ili kubainisha fursa kulingana na mazingira ya sasa na kuzingatia taratibu za kuwatambua na kuwasajili wanaotaka kuwekeza nchini.

Pia amekiagiza Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) kiimarishe matumizi ya TEHAMA ili kutangaza fursa nyingi za uwekezaji zilizopo nchini. “TIC ihakikishe kuwa mwongozo wa uwekezaji unapatikana kwa urahisi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news