Serikali yaipa REA shilingi Bilioni 170 utekelezaji miradi ya umeme Mtwara

NA VERONICA SIMBA
REA

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Dotto Biteko amesema serikali imetoa shilingi bilioni 170 kwa ajili ya utelekezaji wa miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mkoani Mtwara.
Dkt.Biteko ameiagiza REA kufanya tathimini ya wakandarasi wanaotekeza miradi ya umeme na kuachana na wale wanaoshindwa kuendana na kasi ili ifikapo Juni 2024, miradi yote nchini iwe imekamilika.

Naibu Waziri Mkuu ameipongeza REA kwa usimamizi mzuri wa miradi ya usambaji wa nishati vijijini ili kuhakikisha utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya upatikanaji wa nishati vijijini ifikapo 2025 inatimia.

Aidha, Dkt Biteko ameitaka REA na TANESCO kutumia vifaa vya usambazaji umeme vinavyozalishwa na viwanda vya ndani badala ya kuagiza nje ya nchi .
Naibu Waziri Mkuu ameyasema hayo tarehe 15 Novemba 2023 katika wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara wakati akiwasha umeme katika vijiji vya Nachenjele na Naliendele katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema katika kukuza viwanda vya ndani, REA na Tanesco wanapaswa kuhakikisha inatumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani kuchochea ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa ajira kwa wananchi.
“REA msicheke na wakandarasi wanaokwamisha utelekezaji wa malengo yetu na hili linahitaji usimamizi wa karibu kwa kila miradi,” amesema Dkt.Biteko.

Amesema wafanye tathimini ya wakandarasi na kuahidi kurudi baada ya miezi mitatu kuhakikisha wamekamilisha kama alivyoagiza.
“Tunataka tutoke kwenye miradi ya vijiji na tuingie katika kampeni ya kitongoji kwa kitongoji baada ya uchaguzi mkuu ujao,” amesisitiza.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugezi Mkuu wa REA ambaye ni Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Jones Olotu amesema wamesambaza umeme katika vijiji 384 kati ya 785 ambapo vilivyosalia viko katika utekelezaji.
Amesema, REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unalenga kupeleka katika vijiji vyote 401 ambapo wakandarasi wanaendelea na kazi hizo. Mhandisi Olotu amesema kuwa wanatekeleza miradi ya kusambaza umeme maeneo ya pembezoni mwa mji, mradi wa kupeleka umeme kwenye migodi midogo, maeneo ya kilimo, vituo vya afya na pampu za maji na miradi ya ujazilizi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news