Sitenganishi ndoa za watu, ninaunganisha-Mkemia Mkuu wa Serikali

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Mabaara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS) imesema kuwa, huwa haikusiki kutenganisha ndoa za watu badala yake imekuwa mstari wa mbele kuzitengeneza kuwa imara.

Hayo yamesemwa leo Novemba 30, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt.Fidelice Mafumiko katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Huwa nikijitambulisha kuwa ni Mkemia Mkuu wa Serikali wanasema wewe ndiye unayetenganisha ndoa za watu. Hapana, mimi ndiye ninayetengeneza na kwa Mkemia Mkuu huwa unakuja ukiwa na uhitaji, na sisi huwa tunafanya na ushauri pia.

Afisa Uhusiano Mwandamizi, Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), Bw. Sabato Kosuri, akiongoza kikao hicho.

"Tunakushauri kuhusu shida uliyo nayo, lakini kama nilivyosema awali kuna mamlaka ombezi. Sheria imeweka kabisa utaratibu wa kuomba kipimo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, kwa hiyo zipo mamlaka ombezi.

"Kama ni suala linahusiana na kijamii unataka ujue uhalali wa mtoto, wako wenzetu wa utaalamu wa Ustawi wa Jamii, wao wamewekwa kisheria na wapo mawakili wale walioandikishwa nao wamewekwa kisheria.

"Lakini, kama ni suala lipo mahakamani basi Mahakama watafanya hivyo, kama ni suala la jinai lipo polisi, polisi watafanya hivyo. Kama ni suala la tiba, basi madaktari wameidhinishwa kama ni suala la majanga basi wakuu wetu wa wilaya watafanya hivyo.Kwa hiyo hauji moja kwa moja kwamba mimi ninataka kupima vinasaba leo, na kuna taratibu zake,"amefafanua Mkemia Mkuu wa Serikali.
Katika hatua nyingine, Dkt.Mafumiko amesema kuwa, matokeo ya kuhakiki uchunguzi wa uhalali wa watoto kwa wazazi kupitia vinasaba (DNA) ni ya uhakika.

Amesema, gharama ya uchunguzi ni shilingi 100,000 kwa sampuli ya mtu mmoja hivyo kwa uchunguzi wa mama,baba na mtoto gharama ni shilingi 300,000 ambazo hulipwa kupitia benki.

Vile vile amesema,ili kupata huduma ya uchunguzi zipo taratibu za kuzifuata ambapo mteja haendi moja kwa moja kupima vinasaba ila anawakilishwa na taasisi zilizotajwa kisheria ili kumuombea mteja huduma ya uchunguzi.

Amesema, taasisi hizo zitaandika barua ya maombi ya kupatiwa huduma kwa niaba ya mteja husika kwenda kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Dkt.Mafumiko amesema, baada ya kulipia gharama sampuli zitachukuliwa na uchunguzi utafanyika na majibu yatatolewa kwa taasisi iliyoandika barua ambapo mteja atapata majibu kupitia taasisi hizo ndani ya wastani wa siku 27 za kazi kutegemea na aina ya sampuli.

Mamlaka ya Mabaara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS) ilianzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na.8 ya Mwaka 2016.

Pamoja na majukumu mengine, Sheria ya Mamlaka inaipa jukumu mamlaka ya kuwa chombo cha juu na Maabara ya Rufaa katika masuala yote yanayohusu uchunguzi wa sayansi jinai na huduma za vinasaba, ubora wa bidhaa na usimamizi wa kemikali.

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imepitia mabadiliko mbalimbali kutoka kuwa idara ndani ya wizara, wakala kati ya mwaka 1999-2016 na kuwa mamlaka kuanzia tarehe 5 Aprili,2017 hadi sasa.

Aidha, kihistoria mamlaka hii ilianza kama kituo cha kufanya utafiti wa magonjwa ya ukanda wa joto kwenye maabara ya taifa mwaka wa 1895 na baadae kuhamishiwa Wizara ya Afya baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1947.

Kati ya mwaka 1947-1959 maabara ilihamishiwa Wizara ya Kilimo na Maliasili na kutoka mwaka 1958 hadi sasa maabara ipo chini ya wizara yenye dhamana ya afya nchini.

Vile vile, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeimarisha utekelezaji mzuri wa majukumu yake, kufikiwa kwa malengo, dhima na dira yake, hivyo kuchangia jitihada za Serikali katika kuboresha ustawi wa watu wake na mazingira.

Dkt.Mafumiko amesema, miongoni mwa majukumu ya mamlaka hiyo ni utoaji wa ushahidi wa kitaalam unaohusu uchunguzi wa kimaabara mahakamani, mashauri ya jamii dawa za kulevya, mauaji, uabakaji, ulawiti na ujangili wa wanyama pori.

Majukumu mengine, Mkemia Mkuu wa Serikali amesema wanajishughulisha na mashauri ya madai uhalali wa wazazi kwa mtoto, utatuzi wa migogoro inayohusiana na mirathi.

Amesema, mamlaka hiyo imepata mafanikio makubwa ikiwemo ununuzi wa mitambo mikubwa minane na midogo 134 yenye thamani ya shilingi Bilioni 9.3 katika kipindi cha mwaka wa Fedha 2021/2022 na 2022/2023.

Kwa upande wa mafunzo, Dkt.Mafumiko amesema,mwaka wa Fedha 2021/2022 watalaam 28 walihudhuria mafunzo ya muda mrefu huku watumishi 147 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi ndani na nje ya nchi.

Pia amesema, watumishi 56 waliwezeshwa kuhudhuria mikutano ya kitaaluma na 23 waliwezeshwa kupata mafunzo ya awali ya utumishi ya umma.

Akizungumzia kwa upande wa huduma za uchunguzi wa kimaabara, Dkt.Mafumiko amesema,mwaka wa Fedha 2021/2022 wastani wa sampuli au vielelezo 155,817 sawa na asilimia 139.94 ya lengo la wastani wa kuchunguza sampuli na vielelezo 111,349 ulifanyika.

Mwaka wa Fedha 2022/2023, amesema sampuli 212,306 sawa na asilimia 133.9 ya lengo la kuchunguza sampuli 158,600 zilifanyiwa uchunguzi wa kimabaara.

Dkt.Mafumiko akizungumzia utoaji wa matokeo ya uchunguzi kwa wakati (Mkataba wa Huduma kwa Mteja) amesema,wastani wa siku 11 za kazi unatumika kubainisha uwepo wa sumu kwenye sampuli.

Amesema, pia wastani wa siku 6.5 za kazi zinatumika kukamilisha uchunguzi wa kimaabara kwa sampuli za dawa za kulevya, moto na milipuko.

Vile vile, wastani wa siku 27 za kazi zinatumika kukamilisha uchunguzi wa kimaabara kwa sampuli za vinasaba vya binadamu kwa kutegemea aina ya sampuli.

Dkt.Mafumiko amesema, kuna umuhimu wa huduma za uchunguzi wa kimaabara hususani kuleta haki, amani na utulivu wa nchi kwa kutoa ushahidi mahakamani kwenye mashauri yanayotokana na uchunguzi wake.

Umuhimu mwingine amebainisha kuwa, ni kutatua migogoro kwenye jamii hasa kuhusu uhalali wa wazazi kwa mtoto, mirathi na kuwezesha kupandikiza figo kwa wagonjwa kwa ushirikiano na madaktari bingwa.

"Na tunawezesha kutambua ubora na usalama wa bidhaa za viwandani na kilimo kwa ajili ya kulinda afya ya jamii nchini,"amesema Mkemia Mkuu wa Serikali.

Ofisi ya TR

Akizungumzia kuhusiana na vikao kazi hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR),Thobias Makoba amesema kuwa,

"Huu ni mwendelezo wa vikao vyetu kazi, sisi kama wanahabari na taasisi ambazo Msajili wa Hazina anazisimamia, malengo ni yale yale kuhakikisha umma wa Watanzania unafahamu nini hizi taasisi ambazo ziko chini ya Msajili wa Hazina ambaye anazisimamia kwa niaba ya Serikali, taasisi hizi zinafanya nini.

"Unaowaona hapa wanawakilisha sehemu ya wanahabari Tanzania, wahariri wanakuja hapa kwa malengo mawili, kwanza kujifunza kwa sababu elimu haina mwisho, kufahamu taasisi zinafanya nini.

"Lakini, kupitia uelewa wao ndiyo wanatusaidia umma wa Watanzania kujua nini ambacho hizi taasisi zinafanya, maendeleo ya taasisi hizi, lakini pia na mafanikio ambayo yamefikiwa mpaka sasa.

"Kwa sababu Serikali inavyozidi kupambana kila siku kwa mipango yake ni wajibu wa Serikali kuufahamisha umma maendeleo na mafanikio ambayo taasisi hizo zinafanya."

Amesema, Mamlaka ya Mabaara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS) ni miongoni mwa taasisi ambazo si za kibiashara ikizingatiwa kuwa Msajili wa Hazina anasimamia taasisi za aina mbili kwa maana ya zile ambazo zinafanya biashara na zile ambazo hazifanyi biashara zinatoa huduma kwa jamii.

Makoba amesema,moja ya mashirika au taasisi za kimkakati ambazo zitaendelea kutoa huduma ni Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

""Kwa nini eneo la kimkakati? Mkemia Mkuu yeye anaweza asilete faida ya fedha, lakini mmesikia kwenye utangulizi hapa, kuna maeneo matatu yamekuwa yakijirudia kwanza afya na ustawi wa jamii.

"Taifa ambalo halina afya, wote tunajua afya ndiyo kila kitu, tumeweza kufika hapa kwa sababu tumehamka salama, tumeweza kufika hapa kwa sababu tumekula vyakula ambavyo havina sumu, tumeweza kufika hapa kwa sababu jamii zetu zimelindwa kimwili na kisaikolojia.

"Moja ya kazi ambayo anaifanya Mkemia Mkuu ni kuhakikisha afya za Watanzania ziko salama. Pili kwenye kusimamia sheria na haki,kwa hiyo hata bila ya kuleta faida lakini tuna faida ya kupata haki kwenye jamii ya Watanzania.

"Lakini, tatu mazingira. Tumezungukwa na sumu za kila aina katika maisha yetu ya kila siku, anayetusimamia kuhakikisha tunajua hapa kuna sumu hapa hakuna sumu ukiacha mashirika mengine kama NEMC ni Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

"Kabla bidhaa hazijaingia, hazijatumika nani anatoa leseni, wanaosimamia kuhakikisha wanatoa endorsement ni Mkemia Mkuu wa Serikali, sasa tukasema ni muhimu na yeye apate wasaa wa kutueleza nini katika hayo maeneo anayoyafanya, amefikia wapi, faida yake kwa umma wa Watanzania na mipango yake huko mbele katika kuchangia maendeleo ya Tanzania,"amefafanua Makoba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news