Steve Nyerere awauma sikio wasanii kuhusu dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steve Nyerere amewataka wasanii nchini kutojihusisha na biashara au matumizi ya dawa za kulevya kwani yanadhoofisha vipaji vyao na kuwapoteza kabisa katika sanaa.

Steve Nyerere ambaye pia ni msanii wa fani ya uigizaji ametoa wito huo Novemba 22, 2023 jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea ofisi za Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na kufanya mazungumzo na Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo.

Katika mazungumzo hayo, Steve Nyerere amepongeza jitihada za Kamishna Jenerali huyo kwa kushirikiana na timu yake kwa kazi nzuri wanaoifanya ya kuhakikisha wanaokoa wasanii na watanzania dhidi ya dawa za kulevya..

"Nichukue nafasi hii kumshukuru Kamishna wetu, Kamishna Jenerali Lyimo wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, kiuweli kabisa Kamishna ana nia nzuri sana ya kuokoa kizazi chetu, Tanzania imebarikiwa kuwa na vipaji vikubwa.

"Na kutangaza utamaduni wetu ndani na nje ya nchi,lakini vipaji hivyo lazima tuhakikishe vinaendana na nidhamu, utamaduni vikiwa na ari na afya njema, afya njema inapatikana kwa msanii mwenyewe akijitambua.

"Tunajua wasanii wengi ni jambo ambalo halifichiki, ni kweli inawezekana bila kupata stimu mtu hapandi kwenye steji, bila kupata stimu mtu hachezi mpira, bila kupata stimu mtu haonekani katika muonekano anaotaka.

"Na stimu imegawanyika katika hatua mbalimbai, kuna stimu nyingine ya unga, kuna stimu nyingine ya dawa za kulevya na kuna stimu ya msuba, wenyewe watoto wa mjini wanaita msuba ya bangi, lakini kuna stimu hata ya pombe kali.

"Lakini hivi vyote vinany'ong'onyesha vipaji, hivi vyote vinamuharibu msanii wetu kutokuwa na kipaji cha kupeperusha bendera yetu ya Tanzania. Kamishna kwa kweli kwa dhati kabisa mimi nikushukuru leo, kiukweli kabisa umeonesha dhairi unawapenda wasanii wa Tanzania.

"Umeonesha dhairi nia yako ni kuhakikisha msanii wa Tanzania anafanya sanaa yake kwenye mazingira yenye afya bora,lakini kikubwa zaidi tunasema yajayo yanafurahisha ni msanii mwenyewe kujitambua na Kamishna kanielezea hapa jambo jema ambalo kwangu nimelifurahia kwamba yeye ni mpenda sanaa, na enzi zake alikuwa balaa, lakini alijilinda na ndiyo maana kafika hapa kwenye ndoto yake.

"Na sisi wasanii ni lazima tujilinde mpaka tutimize ndoto yetu, sanaa ni ajira kama zilivyo ajira nyingine. Ajira yoyote inalindwa kwa njia yoyote ili ufikie malengo.

"Niwaombe wasanii wenzangu tumuunge mkono Kamishna wetu Lyimo kwa juhudi za kuhakikisha msanii wa Tanzania havuti unga,m havuti bangi anafanya sanaa yake kwenye weledi mkubwa kusaidia familia yake, lakini vile vile kupeperusha bendera ya Tanzania,"amesisitia Steve Nyerere.

KAMISHNA

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema kuwa, "Niseme tu nikushukuru sana Steve kwa kuja ofisini kwetu, lakini pia kwa ujumbe mzuri ambao umeuleta kutoka kwa wasanii.

"Na sisi kama Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya tunatambua kwamba, msanii ni hazina, msanii ndiye anaifanya Tanzania itambulike.

"Msanii ni hazina, na msanii ni kioo cha jamii, ni lazima sasa tuilinde hii hazina kwa gharama zozote, inasikitisha sana unapoona msanii amekuwa na kipaji na uwezo wake, anatoa nyimbo nzuri ambazo zinatambulika mpaka kidunia, lakini mwisho wa siku anaingia kwenye dawa za kulevya, anapotea.

"Kwa hiyo, inakuwa sisi kama Tanzania tumepoteza kipaji,tumepoteza hazina na tumepoteza kioo cha taifa kwa hiyo, tunachotaka sisi kama Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ni kulinda hii hazina.

"Ili usanii uwe ni usanii ambao unaleta hadhi katika Taifa, unaleta hadhi kwa Serikali, lakini hata viongozi wa Serikali na Serikali kwa ujumla iwatumie katika shughuli zake mbalimbali.

"Lakini, wawe wanaheshimika na jamii na wanaheshika na Serikali, na ndiyo maana tunataka kuanzia sasa hivi wasanii waondokane kwenye matumizi ya dawa za kulevya tuwatoe huko ili tuhakikishe tunalinda hii hazina.

"Sote twende kwa pamoja tuendelee kuwa kioo cha jamii kweli na usanii uwe ni kuelimisha jamii, ni kuifanya jamii iepukane na maovu irudi kwenye hali halisi, hali nzuri, hali yenye heshima, hali yenye maadili na ndicho tunachokilenga kama Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

"Na sisi tutaendelea kuwaheshimu wasanii na tutaendelea kufanya kazi nao, lakini kuhakikisha kwamba hawajiingizi kwenye matumizi ya dawa za kulevya,"amebainisha Kamishna Jenerali, Aretas Lyimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news