Tanzania, Finland kuendelea kuimarisha ushirikiano kumuenzi Hayati Martti Ahtisaari

HELSINKI-Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano na Finland ili kuenzi misingi mizuri ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili iliyowekwa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Hayati Martti Ahtisaari.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk alipozungumza katika hafla ya kumbumbuku ya kumuenzi Hayati Ahtisaari iliyofanyika jijini Helsinki Finland tarehe 11 Novemba 2023.

Amesema Hayati Ahtisaari ambaye dunia inamtambua kwa mchango wake mkubwa katika kutetea amani, Tanzania itaendelea kumuenzi na kutambua mchango wake mkubwa alioutoa katika kuimarisha ushirikiano na Tanzania tangu akiwa Balozi wa Finland nchini Tanzania mwaka 1973 hadi 1976 na alipokuwa Rais wa nchi hiyo mwaka 1994 hadi 2000.

Amesema kupitia misingi hiyo, Finland imekuwa mshirika mzuri wa Tanzania katika kutekeleza agenda mbamlimbali za maendeleo na kwamba mchango wa nchi hiyo kwenye sekta mbalimbali za maendeleo utaendelea kubaki kama alama ya kukumbukwa tangu Tanzania ilipotoka na ilipo sasa.

Mhe. Balozi Mbarouk akiendelea na hotuba yake, ambapo pamoja na mambo mengine alisema Tanzania itaimarisha ushirikiano na Finland kumuenzi Hayati Ahtisaari.

“Ninayo furaha kusema kwamba, Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuhakikisha uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili na watu wake unaimarika siku hata siku,” alisisitiza Mhe. Balozi Mbarouk.
Vilevile amesema kuwa, mtazamo wa Tanzania na Filand katika agenda mbalimbali za kimataifa unafanana, hivyo Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi hiyo kuhakikisha agenda hizo ikiwemo kuleta maendeleo ya kiuchumi duniani, ulinzi wa amani na mapambano dhidi ya umaskini zinatekelezwa ili kuifanya dunia mahali salama pa kila mmoja kuishi.

Kadhalika Mhe. Balozi Mbarouk amepongeza kuwepo kwa Mfuko wa Amani wa Martti Ahtisaari (CMI) ambao una jukumu kubwa la kuendelea kuenzi urithi mwema aliouacha Hayati Ahtisaari ambaye anatambulika kama mtetezi bingwa wa Amani duniani.

Mhe. Balozi Mbarouk alitoa hotuba hiyo kwa niaba ya Rais Mstaafu, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye mazishi ya kitaifa ya Hayati Ahtisaari yaliyofanyika jijini Helsiknki tarehe 10 Novemba 2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news