NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt.John Mduma amesema, thamani ya mfuko huo hadi kufikia Septemba, mwaka huu ilikuwa shilingi bilioni 697.5.Pia, mapato ambayo yanatokana na uwekezaji wa mfuko yanafikia zaidi ya shilingi bilioni 300.
Dkt.Mduma ameyasema hayo leo Novemba 2, 2023 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema, kwa sasa mfuko huo unatoa mafao saba ambayo yanajumuisha fao la matibabu, ulemavu wa muda, ulemavu wa kudumu, fao la utegemezi, fao la utengamao na fao la utegemezi.
Amesema, fao la utengamao limelenga kumjengea uwezo mwajiriwa ambaye anapata ajali au ugonjwa kazini uwezo ili aweze kujitegemea licha ya changamoto ambayo amepitia akiwa kazini.
“Ulemavu wa muda. Sisi tunakulipa kwa kipindi ambacho wewe unaugua na hauwezi kumzalishia mwajiri wako.
“Fao la ulemavu wa kudumu, sasa imefikia hatua madaktari wamethibitisha umepona, lakini una ulemavu wa kudumu, ulemavu usiozidi asilimia 30 fao hili linatolewa kwa mkupuo. Fao linalozidi asilimia 30 unalipwa maisha yako yote.”
Akizungumzia kuhusu fao la wategemezi, anasema pale ambapo anafariki baba au mama huwa linalipwa kuligana na mtiririko wa wategemezi.
“Fao hilo huwa linalipwa asilimia 40 ya kiasi cha mshahara wa muhusika hivyo kuendelea kupunguza umaskini.”
Amesema, vyanzo vya mapato ya mfuko huo ni michango ya waajiri na miradi yake ya uwekezaji ambayo ipo nchini.
Vile vile amesema, dhima yao ni kuwa mfano wa kuigwa katika Bara la Afrika na kutoa uhakikisho wa huduma bora kwa jamii hasa watu wanaopatwa na madhila ya ajali kazini.
Amesema, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoundwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi (Sura 263 marejeo ya mwaka 2015]).
Dkt.Mduma amesema, lengo la kuanzishwa kwa mfuko ni kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara ambao wataumia,kuugua ama kufariki kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba ya ajira zao.
Amesema, walengwa wa WCF ni waajiri na wafanyakazi wote katika sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara.
“Kwa sasa, mwajiri pekee ndiye anayechangia katika mfuko. Mwajiri hapaswi kumkata mfanyakazi kiasi chochote cha pesa, michango hii ni gharama ya mwajiri na sio mfanyakazi.”
Dkt.Mduma amesema, wakati mfuko unaanza mwaka 2015 waliweza kusajili asilimia 15 ya waajiri ambao walikuwa 5,178 katika database yao, lakini hadi kufikia Septemba mwaka huu usajili umefikia zaidi ya asilimia 93 sawa na waajiri 31,469.
Uwekezaji wa mfuko hadi kufikia Septemba 2023 umeimarika na wamefanikiwa kulipa kodi ya shilingi bilioni 62.7 kutokana na uwekezaji wake.
“Hii ni kodi ya mapato ambayo inatokana na uwekezaji tu. Mwelekeo wa mfuko siku zijazo ni kupanua huduma zetu.”
Pia, amesema wamejipanga kuimarisha huduma zao kidigitali na kufungua huduma katika mikoa ya kimkakati nchini.
Vile vile amesema, WCF imepanua wigo utoaji huduma kwa kuingia makubaliano na hospitali, watoa huduma mbalimbali za afya nchini.
Dkt.Mduma amesema,kutokana na tathimini ya uhai wa uendelevu walioyofanyiwa mara mbili mwaka 2018 na mwaka 2022 na Shirika la Kazi Dunnia (ILO) inaonesha mfuko kuwa na uwezo endelevu wa kulipa fidia mpaka mwaka wa fedha 2047/2048.
“WCF imefanya tathmini ya pili mwaka 2022 ambayo imeonesha kuwa mfuko ni himilivu na unauwezo wa kuendelea kutoa huduma bila kutetereka kwa muda mrefu kulingana na tathimini tuliyofanyiwa na ILO mwaka 2018 na mwaka 2022.
“Lakini pia uwepo wa WCF umeleta tija kazini kutokana na mahusiano mazuri kati ya waajiri na waajiriwa, lakini pia kupunguza umaskini hususani kwa wategemezi na wafanyakazi wanaopata ulemavu wa kudumu na kushindwa kurudi kazini au kufariki,” amesema Dkt.Mduma.
Mbali na hayo, Dkt.Mduma amesema,mfuko huo unachangia ongezeko la uzalishaji na maendeleo ya Taifa kupitia ongezeko la tija, ongezeko la pato la taifa na kodi ili kuiwezesha Serikali kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi
Amesema, hadi kufikia sasa wamelipa fidia zaidi ya shilingi bilioni 60 ambapo pia mfuko huo umekuwa kivutio kwa mataifa ya nje kuja kujifunza namna ambavyo wanaendesha huduma zao.
“Kwenye hiyo fidia ambayo tumelipa imegawanyika kwenye yale mafao saba, kwa hiyo.Kuna mafao mengine.
“Tunaamini kwamba kwa kuleta mfuko na kutoa mafao kulingana na wakati huu tumekidhi matakwa na changamoto ambazo zilikuwa zinajitokeza huko zamani na kupunguza umaskini katika jamii,”amesema Dkt.Mduma huku akibainisha kuwa, jukumu la kumlipa fidia kwa mtu aliyeumia kwa mujibu wa sheria ya zamani lilikuwa kwa mwajiri."
Akizungumza katika kikao kazi hicho,Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Thobias Makoba amewaomba wanahabari kuendelea kushirikiana na Serikali kwa ajili ya kuhabarisha umma kuhusu mambo mbalimbali yanayofanyika nchini.
Amesema, Serikali inatekeleza miradi mingi ikiwemo ya kimkakati ambayo inahitaji ushirikiano wa vyombo vya habari ili umma uweze kutambua yanayofanyika.
“Kuna mambo mengi mazuri ambayo Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anayafanya, kupitia miradi na mageuzi haya ya kiuchumi yanatakiwa umma uweze kufahamu kupitia vyombo vyenu vya habari."
Wakati huo huo, Dkt.Mduma ameipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina chini ya Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu kwa kuja na ubunifu huo ambao unawezesha umma kufahamu yale ambayo yanafanywa na taasisi na mashirika yao, yalikotoka, yalipo na yanapokwenda. "Ninampongeza sana Msajili wa Hazina, mwambieni ofisi yetu hii ina afya tele."
TEF
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatius Balile amewataka wanahabari kwenda kuwaeleza waajiri wao umuhimu wa kuwasajili WCF.
"Nendeni mkaidai hii haki ya kusajiliwa WCF kwa waajiri wenu. Ni suala la uamuzi, wala halihitaji gharama yoyote."
Pia, Balile ameendelea kuipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa namna ambavyo imekuwa mstari wa mbele katika kuviunganisha vyombo vya habari na taasisi za umma ili ziweze kuelezea yale ambayo wanayatekeleza kwa manufaa ya umma.
Vile vile, ameipongeza WSF kwa kuendelea kuwa mdau muhimu katika jukwaa hilo na vyombo vya habari kwa ujumla nchini.