Ubora uwe ndiyo ajenda yetu nchini-Safari Fungo

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mtendaji wa Jukwaa la Ubora Tanzania (The National Quality Association of Tanzania (NQAT), Bw.Safari Fungo amewataka wadau wote nchini kuhakikisha wanakuwa na mikakati madhubuti ambayo itaufanya ubora kuwa ndiyo ajenda yao kuu.

Ameyasema hayo Novemba 10, 2023 jijini Dar es Salaam katika Kilele cha Wiki ya Maadhimisho ya Ubora Duniani ambayo yalifanyika katika Ukumbi wa Maktaba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huku yakiambatana na utoaji Tuzo za Ubora.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara,Bw.Sempeho Nyari.

"Ni vizuri tukakumbushana kwamba, katika nyakati hizi za mapinduzi makubwa ya sayansi na teknolojia, wale wenye maarifa ya masuala ya ubora wakazingatia na wakayatumia vizuri ndiyo watakaoendelea kuwa na ushindani mkubwa katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii katika Dunia ya leo.

"Kwa hiyo kauli mbiu ya mwaka huu ambayo inajikita katika kuangalia ni namna gani ambayo mambo ya ubora yanaweza kusaidia katika kupata hizo nguvu za kiushindani imekuja wakati sahihi,ni wito wangu kwa wadau wote kwamba, tujitahidi kuhakikisha kwamba tunaiishi kaulimbiu hii.

"Tuongeze ubora kwenye shughuli zetu ili tuweze kupata ushindani, na ni muhimu zaidi tukakumbuka kwamba, kama nchi tuna commitment katika kanda, mathalani Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kwa maana ya SADC.

"Pamoja na ukanda mkubwa wa Eneo Huru la Kibiashara katika Bara la Afrika, hatuwezi kufanikiwa endapo hatutakuwa na mikakati madhubuti ya kuhakikisha ubora unakuwa ndiyo ajenda yetu kuu,"amesisitiza Bw.Fungo.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema, jukwaa hilo limeanza kufanya kazi tangu mwaka 2019, na toka wameanza wamekuwa wakiratibu Tanzania Summit Quality.

"Mwaka huu wa 2023 kwa kushirikiana na TBS (Shirika la Viwango Tanzania) na kwa kuwa dhamira yetu ni moja tukasema kwamba, tuungane tuweze kuandaa sherehe hizi za kukidhi ile siku ya ubora duniani.

"Kwa hiyo kwa namna ya kipekee ninaipongeza Menejimenti ya TBS,vile vile ninawapongeza wadau wote kwa kujitoa kwao kuhakikisha tunaweza kuifanikisha siku hii kwa namna iliyo bora zaidi,"aliongeza Bw.Fungo.

Hata hivyo,NQAT imeendelea kujivunia juhudi ambazo Bw.Safari anaweka katika ajenda za ubora nchini Tanzania ambapo katika Tuzo za Ubora wa Kitaifa za 2023 zilizofanyika kupitia hafla hiyo, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilimkabidhi tuzo yake kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kama mtu binafsi mwenye ushawishi katika miundombinu bora ya viwango.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news