RUVUMA-Serikali ya Ujerumani imeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuboresha Makumbusho ya Majimaji ili kuhifadhi kumbukumbu sahihi kwa ajili ya wakati huu na kwa vizazi vijavyo.


“Ili kuweka kumbukumbu sawa kwa sasa na kwa wakati ujao, Ujerumani tunaahidi kushirikiana na Tanzania kuboresha makumbusho hii,” alisisitiza Mhe. Rais Steinmeier.

“Mwaka 2024, Ujerumani inampango wa kufanya maonesho kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa ya Tanzania, maonesho hayo yatajulikana kwa jina la “Historia ya Tanzania”, alisema Mheshimiwa Steinmeier.
Awali Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) alisema historia ya Tanzania na Ujerumani ina sura mbili tofauti. Alifafanua kuwa sura ya kwanza ni kuhusu vita waliyopigana babu zetu na sura ya pili ni yale mazuri yaliyofanywa na Serikali ya Ujerumani Kama vile kujenga shule, hospitali na kutoa huduma nyingine za kijamii.

Dkt. Ndumbaro aliongeza kuwa Songea wanatamani kuona makumbusho ya kisasa ya ushirikiano kati ya Ujerumani na Tanzania yakijengwa Songea, “pia tunatamani Ujerumani itusaidie kuboresha chuo cha VETA Songea ili kuwawezesha vijana wetu kupata mafunzo mbalimbali,” alisema Dkt. Ndumbaro.
Waziri Ndumbaro pamoja na mambo mengine, ameiomba Serikali ya Ujerumani kushirikiana na Mji wa Songea kwa kuwawezesha kutembeleana, kushirikiana na kuendeleza utani kati ya Wangoni na Wajerumani.

Makumbusho ya Vita vya Maji Maji ni makumbusho pekee nchini Tanzania inayoonesha historia kubwa ya Vita vya Maji Maji katika harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa Wajerumani.

Tags
Foreign Tanzania
Kimataifa
Makumbusho ya Majimaji
Makumbusho ya Taifa
Maliasili na Utalii
Maliasili za Tanzania
Ruvuma Region
Tanzania na Ujerumani