ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, ufunguzi wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha India nchini ni utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050.

Rais Dkt. Mwinyi aliyasema hayo kampasi ya Bweleo Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi alipozitundua rasmi chuo hicho.
Amesema, lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kukifunguwa chuo hicho Unguja ni kuleta mabadiliko na maugezi makubwa ya maendeleo ya nchi na watu wake, kielimu, uchumi na jamii.
Dkt. Mwinyi, alieleza ili kuifikia Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inahitaji kuwekeza zaidi na kuwatayarisha wafanyakazi wenye utaalamu na ujuzi wa hali ya juu ili kujenga uchumi na jamii iliyo bora.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa wito kwa vyuo vyengine nchini na Afrika kwa ujumla kutumia fursa ya kuwepo kwa chuo cha IIT Madrasa, Zanzibar kuanzisha ushirikiano ili kukuza uwezo na hadhi ya vyuo vyao na kueleza hadi sasa Chuo hicho tayari kimeingia makubaliano ya ushirikiano na vyuo vyengine vinne duniani, kikiwemo Chuo cha Uingereza cha Birmingham, Chuo cha Uchumi cha Afrika, chuo cha Daeakin cha Australia na chuo cha Teknolojia na Uongozi cha Nigeria.
Alisema, chuo hicho ni fursa adhimu kwa wataalamu wa ndani kubadilishana uzoefu na waataalamu wa India hasa kwenye teknolojia, utafiti na Uvumbuzi.Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa aliwahakikishia hali ya usalama, utulivu na amani, wageni, wahadhiri na wanafunzi wanaotoka nje ya Tanzania watakaosoma kampasi hiyo ya Bweleo.

Mkurugenzi Mtendaji wa chuo hicho, Prof. Preeti Aghalayam alieleza matarajio ya chuo hicho ni kutoa wataalamu waliojengeka kitaaluma na uwezo wakujikimu kwenye ubobezi wa masuala teknolojia yatakayoleta mageuzi makubwa kwenye TEHAMA na maendeleo ya uchumi wa mataifa yao.Jumla ya wanafunzi 46 wakiwemo Watanzania 21 kutoka bara na visiwani wamejiunga chuoni hapo na wengine kutoka maifa mengine ikiwemo Nepal.

Ushirikiano baina India na Tanzania ni wa historia,umeendelea kuimarika kwa fursa nyingi za maendeleo kupatikana kwa watu wa mataifa mawili hayo, Tanzania inaongoza kupata misaada wa nafasi nyingi za udhamini wa masomo nchini India kuliko nchi nyenyine yoyote barani Afrika, kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina yao.